Na Lulu Mussa, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mwanza
Imeelezwa kuwa Tanzania imefanikiwa kuondoa matumizi ya
kemikali zinazoharibu tabaka la Ozoni kutoka tani 254 mwaka 1999 hadi tani
35.76 mwaka 2009.
Hayo yameelezwa leo Jijini Mwanza na Bw. Ndaro Lulwijila (Pichani), Katibu
Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Mwanza katika hotuba ya ufunguzi wa warsha ya
mafunzo ya mafundi mchundo kuhusu teknolojia mbadala ya majokofu na viyoyozi.
Bw. Kulwijila ameainisha baadhi ya kemikali hizo kuwa ni
methyl bromide, halons na chloroflorocarborns ambazo hutumika kama vipozi
katika majokofu, viyoyozi, vifaa vya
kuzima moto, usafishaji chuma, ufukizaji wa mazao katika maghala na
utengenezaji wa magodoro ambazo huleta madhara kwa tabaka la ozoni na adhari
zake hutokea kwa binadamu, mimea na viumbe hai.
Amezitaja athari za uharibifu wa tabaka la ozoni kuwa ni kuongezeka
kwa magonjwa ya saratani ya ngozi,uharibifu wa macho maarufu kwa jina la mtoto
wa jicho, na upungufu wa uwezo wa mwili kujikinga na maradhi.
Athari hizi kwa kiasi kikubwa zinatokana na
shughuli za kibinadamu kama vile matumizi ya kemikali haribifu na zisizo rafiki
kwa mazingira.
Bw. Kulwijila amewataka wanahabari kutoa elimu zaidi kwa
wananchi juu ya athari hizi ikiwa ni pamoja na kuiomba Serikali kudhibiti
uingizaji wa majokofu yaliyotumika. Jitihada za Uhifadhi wa tabaka la ozoni
umetokana na utekelezaji wa Mkataba wa Montreal na Vienna ambayo Tanzania iliridhia
mwaka 1993.
Warsha hiyo imeratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais imehusisha
washiriki kutoka, Chuo cha ufundi VETA - Mwanza na Kigoma, wanahabari, Maafisa
mazingira wa Mkoa wa Mwanza na mafundi mchundo kutoka viwanda mbalimbali vya Jiji la Mwanza.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269