Breaking News

Your Ad Spot

May 15, 2012

JK: SINA WASI WASI NA UWEZO WA WAJUME WA TUME YA KUKUSANYA NA KURATIBU MAONI YA KATIBA MPYA

Rais Jakaya Kikwete
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa yeye, kama walivyo Watanzania wengine, hana wasiwasi na uwezo wa wajumbe wa Tume ya Kukusanya na Kuratibu Maoni ya Katiba kuifanya kazi hiyo vizuri na kwa ufanisi mkubwa.
     Aidha, Rais Kikwete amewataka wajumbe wa Tume hiyo kuwa huru kabisa katika kuifanya kazi yao bila kuruhusu kuingiliwa na mtu yoyote.
Rais Kikwete amesema hayo jioni ya leo, Jumanne, Mei 15, 2012 wakati alipote mbelea Ofisi za Tume hiyo zilizoko Mtaa wa Ohio, mjini Dar es Salaam, akakagua ofisi hizo na kuzungumza kwa ufupi na wajumbe wa Tume hiyo ambayo iko chini ya uenyekiti wa Jaji Joseph Sinde Warioba na Makamu Mwenyekiti Jaji Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhan.
     Akizungumza na wajumbe wa Tume hiyo, Rais Kikwete amesema kuwa ana uhakika kuwa wajumbe wa Tume hiyo watatimiza matarajio ya Watanzania katika kuifanya vizuri kazi ya Kukusanya na Kuratibu maoni ya wananchi kuhusu Katiba mpya.
    “Nimefurahi kusikia kuwa mumeianza kazi yetu vizuri. Nawaombeni muwe huru kabisa katika kuifanya kazi yetu. Na kwa ubora wa sifa za wajumbe, binafsi, kama walivyo Watanzania wengine sina wasiwasi juu ya uwezo wenu kuifanya kazi hii vizuri,” Rais Kikwete amewaambia wajumbe waTume hiyo na kuongeza:
    “Kilichobakia kwetu ni lini milango itafunguliwa ili tuanze kutoa maoni yetu …. huo ndiyo mchango wetu katika mchakato huu.”
    Mapema akimkaribisha Mheshimiwa Rais, Jaji Warioba amesema kuwa Tume hiyo ilianza kazi kama ilivyotakiwa kisheria Mei Mosi mwaka huu na kuwa kazi ambazo zimefanyika mpaka sasa ni wajumbe kujielimisha kuhusu Sheria yenyewe ya Katiba na kuorodhesha Hadidu za Rejea za Tume.
    “Mheshimiwa Rais tumetumia wiki hii ya kwanza ya kazi yetu kujielimisha kuhusu Sheria yenyewe iliyounda Tume hii na pia tumeorodhesha Hadidu za Rejea za Tume.
    Tumeanza pia maandalizi kwa ajili ya utoaji wa elimu kwa umma na baada ya hapo tutatengeneza ratiba ya kazi yetu,” amesema Jaji Warioba na kuongeza:
    “Tumeanza kuona kuwa kazi hii itakuwa siyo rahisi na muda ni mfupi lakini itafanyika. 
    Tunakushukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ya uteuzi wa Tume na imani ambayo umeionyesha kwetu kwa kutuchagua kutumikia katika Tume hii.”
     Rais pia amejulishwa kwa kazi ya kuajiri watumishi wa Tume hiyo imeanza na mpaka sasa wameajiriwa watumishi 29 kati ya 173 wanaotakiwa kufanya kazi kwenye tume hiyo ambayo itaifanya kazi ya Kukusanya na Kuratibu maoni kwa miezi 18 kuanzia Mei Mosi mwaka huu.

1 comment:

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages