Breaking News

Your Ad Spot

Jun 28, 2012

MGOMO WA MADAKTARI: MBEYA NA DODOMA WATIMULIWA

TANZANIA
BODI ya hospitali ya Rufani Mbeya, imewatimua kazi madaktari 54 waliokuwa katika mazoezi ya vitendo, na wengine 18 waliokuwa wameajiriwa ambao walikuwa wanaendelea na mgomo usio na kikomo.
    Kaimu mkuu wa mkoa wa Mbeya, Dk.Norman Sigalla, aliyasema hayo leo kwa waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mikutano uliopo katika ofisi hiyo, mjini hapa.
    Dk.Sigalla alisema Juni 25, mwaka huu Bodi ya hospitali ya Rufani Mbeya, ilifanya kikao cha dharula kujadiri hali ya utendaji kazi na utoaji huduma hospitalini hapo.
   Alisema baada ya kikao hicho iliamuliwa Mwenyekiti wa Bodi (ambaye ni Mkuu wa mkoa), akutane na madaktari ambao hawakufika kazini ili awasikilize sababu za kutofika kazini na kujadiri namna ya kumaliza matatizo hayo.
   Aidha, iliamuliwa madaktari wote ambao hawakufika kazini waandikiwe barua za kujieleza kwa nini wasichukuliwe hatua za kinidhamu kwa kuvunja mkataba walioingia na hospitali hiyo na pia kukiuka kanuni za utumishi wa umma toleo la 2009, kifungu namba F. 16-17 na F.27.
   Dk.Sigalla aliongeza kuwa hivyo leo, madaktari 54 wamepewa barua zao za kuwaeleza kuwa Bodi ya hospitali ya Rufani Mbeya imesitisha Internship yao hospitalini hapo na kuwarudisha kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa hatua zaidi zinazostahili.
   "Madaktari 18 ambao ni waajiriwa nao wamekabidhiwa barua zao za kusimamishwa ajira yao hospitali ya Rufani Mbeya na kurudishwa Wizarani ya Afya kwa Katibu Mkuu kwa hatua stahiki za kinidhamu" alisema Dk.Sigalla.
   Aliongeza kuwa ni kwa mujibu wa mkataba waliokuwa wameingia nao madaktari hao wa mazoezi ya vitendo, walitakiwa kuwepo kazini kwa mwaka mzima, hivyo kwa kuwa wameshindwa kutekeleza hilo, Bodi ambayo ndio iliingia nao mkataba imeamua kuuvunja.
   Kwa mujibu wa Kaimu Mkuu wa mkoa, ili kukabiriana na upungufu wa madaktari hospitalini hapo, tayari Bodi imefanikiwa kuazima madaktari wengine sita kutoka halmashauri ya jiji la Mbeya, ili kuongeza nguvu hospitali ya Rufani Mbeya.
   Kutoka Dodoma Inaripotiwa kwamba, Madaktari 11  wa mafunzo kwa vitendo katika Hospital ya Mkoa wa Dodoma wamesimamishwa kazi kutokana na kuendelea na mgomo.
   Mwenyekiti wa Kamati Jumuiya ya Madaktari Mkoa wa Dodoma Dk. Cassian Mkuwa tukio la kufukuzwa kwa madaktari hao ilitokea leo asubuhi wakati wakiwa hospitalini hapo wakiendelea na mgomo wao.
   Amesema baadaye Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Dk Ezeliel Mpuya aliwaita madaktari wote waliopo katika mafuunzo kwa nia ya kuzungumza nao kisha alitoa barua kwa madaktari 11 za kuwasimamisha kazi kuanzia leo kutokana na mgomo.
  Hata hivyo madaktari hao walikataa kupokea barua hizo lakini wakatakiwa kuondoka katika eneo la Hopsitali
Dk. Mkuwa akiwa mmoja kati ya waliofukuzwa, alisema anashindwa kuelewa ni vigezo gain vilitumika kuwapata madaktari hao 11 na kuwasimamisha kazi kwani walikuwa wakigoma ni zaidi ya madaktari 20.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages