.

MJADALA KUHUSU WANAUME KUZUIA VVU KWA WATOTO KUFANYIKA DAR

Jul 15, 2012

 Mkutano wa wazi kwa watu wote  kuelimisha  umma kuhusu wajibu wa wanaume katika kuzuia maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI (VVU) kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto utafanyika jijini Dar es salam wiki hii.

taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) Ananilea Nkya, imesema mkutano huo utafanyika katika viwanja vya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) vilivyoko Mabibo  Dar es Salaam  Jumatano tarehe 18 Julai, 2012 kuanzia saa 9 hadi saa 11 jioni.

Imesema taarifa hiyo kwamba mkutano huo  umeandaliwa na  TGNP kwa kushirikiana na shirika linalohamasisha wanaume kushiriki  kikamilifu katika mabadiliko ya jamii linalojulikana kama MenEngage.

Dkt. Katanta Simwanza wa shirika la CHAMPION linalojishughulisha na harakati za kuzuia maambukizi ya VVU katika nchi za Afrika ndiye atakayetoa mada kuu kuhusu nafasi ya wanaume kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Watoto wachanga kupata VVU wakiwa tumboni mwa mama yao, wakati mama anapojifungua na kutokana na kunyonya maziwa ya  mama yao ni miongoni mwa namna virusi vya ukimwi vinavyoenea   barani Afrika.

Mkutano huo lengo lake ni kuuelimisha umma ni mambo gani wanaume wanaweza kufanya ili kuepusha mama mjamzito mwenye VVU kuambukiza mtoto wake anayezaliwa. 

Wataalamu wa afya wanasema wanawake wajawazito walioambukizwa VVU wanahitaji matibabu maalumu na uangalizi ili kuepusha wasiambukize watoto wao wanaozaliwa.

Utafiti uliofanywa na mpango wa Taifa ya Kudhibiti UKIMWI  (NACP) mwaka 2009 unaonyesha kuwa watoto 120 hapa nchini wanaambukizwa VVU kila siku.

Aidha utafiti huo pia umeonyesha kuwa kiwango cha maambukizi ya VVU kwa wanawake wajawazito hapa nchini  kimefikia asilimia 8.2.

0 Comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

ª