* Adai wana njama za kuuza nchi kwa mataifa tajiri
* Awataka wataje mabilioni yanayopewa nje na mikataba yake.
* Asema harambee zao ni changa la macho
* Ahofia tamaa ya mataifa makubwa kwa rasilimali za nchi masikini
Nape Nnauye akizungumza leo |
DAR ES SALAAM, TANZANIA
CCM imesema imesikitishwa na iliouita usanii mkubwa unaofanywa na Chadema, kuwahadaa Watanzania kwa kufanya harambee kwa lengo la kuhalalisha mabilioni ya chama hicho yanayodaiwa kutolewa na wafadhali kutoka mataifa tajiri duniani.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye aliyasema hayo leo, Agosti 12, 2012, wakati akizungumza na waandishi wa habari, kwenye Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, mtaa wa Lumumba jijijni Dar es salaam.
“Itakumbukwa mara kadhaa Chadema wamekuwa wakiitisha harambee za kisanii kwa kujaribu kuwahadaa baadhi ya Watanzania kwa kuwaomba wakichangie chama hicho huku viongozi wa chama hicho wakijua kuwa tayari wameshapata mabilioni toka kwa wafadhili wao. Mfano mzuri wa usanii huu ni juzi siku ya Jumamosi, Agosti 10, 2012, kwenye hoteli ya Serena ambapo walifanyika kiini macho cha harambee na kurushwa moja kwa moja na kituo kimoja cha televisheni." alisema Nape.
Alisema ,umekuwa ni utamaduni wa Chadema kuhadaa watu kwa kuitisha harambee za kisanii kina wanapokuwa wameshapewa mabilioni ya fedha na wafadhili wao, ili mradi wahalalishe kuwa fedha wanazotumia zimetokana na michango ya watanzania wakati si kweli.
Nape alisisitiza kuwa CCM wanao ushahidi kuhusu zinakotoka fedha na mikataba wanayoingia Chadema na wafadhili hao na kudai kuwa kama hawatasema wenyewe basi yeye (Nape) ipo siku atawasaidia kwa kutaja wafadhili hao na kuanika hadarani mikataba hiyo.
“Tunao ushahidi wa kutosha unaoonyesha mabilioni waliyopewa Chadema juzi na wafadhili kutoka nje ya nchi kwa lengo la kuendeleza operesheni zao mbalimbali nchini. Cha kushangaza badala ya kuwaambia wanachama wao na Watanzania kwa jumla mikataba na wanakoyapata mabilioni haya, wanawahadaa kwa kuwachangisha na kugeuza mapato hayo mtaji wa baadhi ya watu binafsi ndani ya chama”, Alisema Nape
Nape alidai kwamba, siri kubwa inayofichwa kuhusu mikataba na mabilioni wanayopewa Chadema ni kwa sababu wanaotoa fedha hizo wana ajenda ya kunyemelea rasilimali za nchi hii zinazoanza kuonyesha matumaini ya kuwepo kwa wingi ili wapate kizikwapua kwa urahisi kupitia mgongo wa chama hicho.
"Kwanini mabilioni hayo yanatolewa kwa Chadema wakati huu ambapo sasa Tanzania imo katika kufanya utafiti na ugunduzi wa rasilimali mbalimbali zikiwamo gesi na mafuta? Na Je ufadhili huu kwa Chadema licha ya kufichwa sana na kufanywa siri, una nia njema kwa nchi yetu na rasilimali za nchi yetu? Kwanini ufadhili huu wa mabilioni unafanywa siri ya watu wachache hata ndani ya chama chenyewe?", Nape alihoji.
Alisema, hatua hiyo ya Chadema itaitumbukiza Tanzania katika machafuko yasiyoisha, kama ambavyo inashuhudiwa katika baadhi ya nchi zenye rasilimali kama madini ambako nchi zenye utajiri wa fedha zilijipenyeza kupitia walioitwa wapambanaji wa uhuru na haki katika nchi hizo na hadi sasa hakuna amani.
"Migogoro mingi tunayoshuhudia hasa katika nchi zinazoendelea pamoja na kuwepo sababu zingine lakini moja ya chanzo kikubwa ni uwepo wa utajiri wa rasilimali mbalimbali ambapo mataifa makubwa huzitamani na njia pekee ya kuzipata kwa urahisi ni kuchochea migogoro ya ndani na hivyo kuwa rahisi kupora rasilimali hizo wakati wenye nchi wanahangaika katika migogoro na kuachwa wakiwa masikini wa kutupwa huku waadhirika wakubwa wa migogoro na vita hivi vikiwanufaisha wakubwa.” Alisema Nape.
Nape alitoa mwito kwa Watanzania kuwa ni muhimu macho na ulaghai huo wa Chadema na wafadhili wao na kukitaka chama hicho na wafadhili wao kama kweli wana nia njema na Tanzania, waweke wazi mashariti ya ufadhili huo wa mabilioni ya fedha ili Watanzania wote wajue kama yana manufaa kwao au la hasa ikizingatiwa kuwa vyama vya siasa hapa nchini vinaendeshwa kwa fedha za walipa kodi, hivyo Watanzania wana haki ya kujua.
Pamoja na kuwataka kuweka wazi mashariti yanayoambatana na mabilioni hayo Nape aliwataka Chadema waseme hadharani wenyewe kwamba wamepewa mabilioni hayo, na kuwataka waache mara moja kuwahadaa Watanzania na kujaribu kujipachika kuwa ni Chama cha wanyonge kinachotegemea kujiendesha kwa michango ya watanzania huku wakiendelea kuchukua mabilioni kwa siri kutoka nje.
“ Wasipowaeleza watanzania ukweli , tutawasidia kuwaeleza watanzania ukweli wa kiasi halisi cha mabilioni haya, walikozitoa na mikataba waliyoingia. Lengo la hili ni kuhakikisha kuwa nchi yetu haiwekwi rehani kwa uroho wa madaraka wa baadhi ya wana siasa.” Nape alisema.
Nape akawaasa wanasiasa, kuendesha siasa za nchi kwa kuzingatia uzalendo na kukwepa kudumbukia kwenye tamaa za madaraka kujisahau na kuwa tayari hata kuweka nchi rehani, hasa kipindi hichi ambapo ugunduzi wa rasilimali mbali mbali hasa madini, gesi na mafuta vikiwa vinashika kasi nchini na kwamba ugunduzi huo uwe baraka kwa nchi badala ya laana na kuwa chanzo cha kuiuza nchi.
Watanzani ni vema tukafahamu kuwa kila sisemwalo lipo, kama hatuzingatia hili analolisema Nape kuna siku maneno hayo tutakuja kuyakumbuka.
ReplyDeleteTuogope mtu anayefanya jambo kwa siri kwani siku ikijakufahamika tutakuwa tumeshaumia kwa kiasi kikubwa.
Hivyo ni vema tukawa makini na namna mikakati na mipango iliyopo Chadema inavyotekelezwa, Jamani tujifunze kutoka kwa nchi jirani.
Nimekaa chini kwa muda mrefu kuhusu mikutano inayoendeshwa na Chadema, Nikajiuliza hivi hizi gharama ni hizo harambe kweli au? Leo nimepata jibu. Ahsante sana Nape nimeamini jambo usilolijua ni sawa na usiku wa kiza.
ReplyDeleteChadema acheni huo uhuni/Utapeli wenu tumeshawagundua janja yenu. Nawaapieni hamtoweza kuturaghai kwa mbinu chafu zenu