Na Hamis Shimye |
TAALUMA ya uandishi wa habari nchini kila kukicha imeendelea kudharauliwa na wanasiasa na baadhi ya viongozi ambao wanajiona taaluma zao ndio bora na zenye uwezo wa kuhoji na kuakisi mambo.
Mfumo huo umeendelea kuota mizizi huku hata zile klabu, majukwaa na mabaraza ya uandishi wa habari yakiwa kimya na badala yake kuzungumzia mambo mengine ambayo hayana faida kwa mwandishi wa habari.
Uandishi wa habari Tanzania unakumbukana na changamoto lukuki ambazo zilipaswa kuwa sehemu ya mjadala kwa vyama vilivyopewa dhamana ya kuwaongoza waandishi wa habari ambao maisha na mfumo wa kazi zao umekuwa kama mchezo wa bahati nasibu.
Kitendo ambacho kinafanya thamani na hadhi ya mwandishi kila kukicha kupotea huku majina ya dharau nayo yakizidi mara 'watu wamshiko', 'makanjanja' au 'vihiyo'. Yote haya yanasababishwa na ubinafsi na ukasuku wa kukariri matamko.
Kauli ya kashfa na Mbunge Tundu Lissu (Singida Mashariki - CHADEMA) kuhusiana na wajumbe wa tume walioteuliwa na serikali kuhusiana na kifo cha Mwandishi wa habari Daud Mwangosi kuwa baadhi yao hawana uwezo ni fedheha kubwa kwa wajumbe hao na tasnia nzima.
Mbunge huyo aliitisha mkutano na waandishi wa habari kuelezea msimamo wa chama chake kutokuwa na imani na tume hiyo hasa kutokana na kuwa na wajumbe baadhi aliodai wasiokuwa na ueledi wa mambo wanaochunguza.
Katika mkutano huo, Lissu alizungumza mambo mengi juu ya tume hiyo, lengo likiwa kuaminisha umma kuwa tume hiyo haifai na ndiyo maana chama chao wanaikataa huku akitaja majina ya wajumbe wa tume hiyo ambayo kimtazamo wake yeye anasema hawana uwezo.
Hata hivyo, muktadha wa hoja hii hautakuwa kuzungumzia uwezo wa kila mjumbe ndani ya tume hiyo, bali ni udhaifu wa vyama vyetu ambavyo navyo vinapotezwa katika mlengo wa kusimamia maslahi ya waandishi na kuanza kuwa watoa sauti ya wanasiasa kushindana kuikataa tume.
Kuchaguliwa kwa Mwenyekiti wa tume hiyo Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Stephen Ihema na wajumbe wengine wakiwemo mahiri katika tasnia ya habari kama Theopil Makunga (Jukwaa la Wahariri) na Pili Mtambalike (Baraza la Habari Tanzania) ilikuwa ni sehemu ya waandishi na klabu za habari kufurahia na kuipongeza serikali.
Kufurahia huko kunatokana na kifo cha Mwangosi ambaye ni mwenzetu kuwa kinachunguzwa na waandishi wenyewe, hivyo kutolewa kwa kauli za dharau kuwa waandishi wa habari hawawezi kuchunguza kifo ni tusi kubwa ambalo lilipaswa kukemewa na si kuachwa kama inavyotaka kufanywa.
Nakumbuka katika jali ya MV Bukoba, mmoja wa wana habari mahiri nchini Jenerali Ulimwengu alikuwa mjumbe wa tume iliyochunguza chanzo cha ajali hiyo. Mbona mambo yalikwenda sawa au kwa kuwa Lissu alikuwa hajapata umaarufu?
Japokuwa katika suala zima kuhusiana na tukio hilo waandishi walitofautiana kimtazamo na kifikra, lakini linapokuja suala la kudharauliwa, tunapaswa kuwa pamoja na kukemea. Kinyume chake baada ya kunang'wa na Lissu tunatakuja kupewa tusi kubwa zaidi.
Mwenye uwezo na ueledi wa kuchunguza kifo si mwanasheria pekee? Lisu anapaswa kutambua hilo na kuachana na mawazo ya Mfalme Jua, juu ya kile anachokiamini kuwa ni sahihi na hapaswi kupingwa au kukatazwa na mtu.
Jamii inaelimishwa na kufundishwa kupitia mifumo tofauti ya maisha na ndiyo maana wanasaikolojia wanaamini tabia ya mtu ni rahisi kuifahamu kupitia matamshi na matendo yake kuwa ni makuzi gani aliyapata utotoni.
Sitaki niamini kuwa klabu, jukwaa na hata baraza lenyewe halijasikia maneno ya kejeli ya Lissu, bali naamini yapo makundi ndani ya waandishi wa habari likiwemo la wale walio tayari kwa lolote ili mradi wawanufaishe wengine na hasa wanasiasa au watwana wao.
Hilo litapongezwa kwa matamko au hata kwa kujitokeza na kusukuma magari yao kuwa hawa kwa mtazamo wao kuwa hao ni mashujaa na wazalendo wa nchi hii .
Hivyo, ningetamani nguvu iliyotumika kutoa tamko la kuwataka polisi wakae meza moja na CHADEMA kumaliza tatizo, ingetumika kutoa tamko juu ya dharau ya Lissu na chama chake kwa waandishi wa habari nchini.
mtazamo wako ni dhaifu katika masuala yaliyoongelewa na mheshimiwa Tundu Lisu.! Pamoja na kuanzisha blog hii ya kijamii bado hujawa na uwezo wa kuchambua hoja kwa fikra za kijamii zaidi ya kujionyesha wazi kuwa ni mnazi wa utawala dhalimu
ReplyDeleteUnapotoa maoni uwe makini kidogo usitekwe na jazba! Mtazamo huu siyo wangu ila ni maoni ya mdau kama wewe ambaye kwa bahati nzuri ameweka jina na picha yake. Tatizo lako unadhani kuwa kama mtu anaunga mkono serikali unamuona hana fikra za kijamii, huo ni upofu mkubwa. Maana mitandao hii ipo kwa ajili ya maoni ya watu wenye itikadi na fikra tofauti katika jamii. Karibu tena
ReplyDeleteKwanza nakukumbusha akwamba unapojibu hoja, usitekwe na jazba! Maoni hayo siyo ya Mtayarishaji wa Blogu hii kama unavyonishutumu, aliyeandika maoni jina na picha yake vipo hapo. Tafadhali mjibu yeye. Tatizo lenu mnadhani ndio mnaojua kufikiri vizuri na wanajamii bora kuliko wengine wenye fikra zinazokinzana na ninyi. Blogu hii ni kwa ajili ya kila mtu kutoa maoni yake bila kujali itikadi au fikra zake. KARIBU TENA
ReplyDelete