Breaking News

Your Ad Spot

Sep 17, 2012

WAJUMBE WA BARAZA LA WAWAKILISHI WAITEMBELEA TUME YA KATIBA


NA MWANDISHI WETU
Tume ya Mabadiliko ya Katiba imesisitiza umuhimu wa wadau mbalimbali wakiwemo wanasiasa, asasi za kiraia na kidini kuwaacha wananchi kutoa maoni yao binafsi kuhusu Katiba Mpya.

Akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar leo (Jumatatu, Septemba 17, 2012), Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Joseph Warioba alisema  katika mikutano ya ukusanyaji wa maoni  inayoendelea, na kukusisitiza kuwa makundi na taasisi mbalimbali vitapata nafasi ya kukutana na Tume na kutoa maoni yao.

Aidha Jaji Warioba alisema kuwa changamoto kubwa  ambayo Tume hiyo  inakabiliana nayo  ni wananchi kupewa mawazo ya kuzungumza  na watu wengine, jambo ambalo haliwasaidii wananchi .

“Makundi ya watu, Taasisi za kirai na hata vyama vya siasa vimekuwa  mstari wa mbele kuwalisha wananchi mambo ya kuzungumza “  alisisitiza  Jaji Warioba.

Mwenyekiti huyo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba aliwataka  wawakilishi hao kuisaidia Tume kuwaelimisha wananchi  kuwa tayari kutoa maoni yao  ya moyoni na kukataa kabisa  kupokea mawazo ya  watu wengine ili  katiba itakayopatikana iwe  inawakilisha mawazo yao.

Jaji Warioba alikuwa akijibu swali la Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Ali Abdalla Ali ambaye alitaka kujua changamoto ambazo Tume inakutana nazo katika utekelezaji wa majukumu yake.

Jaji Warioba amesisitiza kuwa viongozi wa makundi mbalimbali na vyama vya siasa wana wajibu wa kuwaelimisha wananchi kutoa maoni yao binafsi badala ya kuwaelekeza aina ya maoni wanayopaswa kuyatoa.

Akizungumzia kuhusu muda uliopangwa katika kutekeleza kazi hiyo, Jaji Warioba  alieleza kuwa  pamoja na changamoto  hiyo  lakini Tume imejipanga kumaliza  kazi yake ndani  ya muda iliopewa kisheria.

“Tume imejipanga kuhakikisha ifikapo  April 26 2014 katiba mpya inakuwa tayari. Kimsingi  mazingira ya hali ya kisiasa  nchini yanalazimisha kuwepo na katiba mpya kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ili  kuweka maelewano  ya kitaifa” alifafanua.

Wajumbe hao wa Baraza la Wawakilishi wapo katika ziara ya taasisi mbalimbali za Muungano zilizopo Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Ali Abdallah Ali amesema Wajumbe wa Kamati watatumia uzoefu na elimu waliyoipata katika ziara yao ili kuisaidia Tume kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Wajumbe hao walipata nafasi ya kutembelea  vitengo  vya Utafiti  na  Taarifa Rasmi (Hansard)   ambapo waliweza kuona  jinsi maoni yanavyopokelewa na  na  kufanyiwa kazi .

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages