Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba (pichani), amesisitiza umumihu wa wananchi kutoa maoni maoni yao kuhusu Katiba Mpya badala ya kukimbilia kuwasilisha maoni waliyolishwa na viongozi wa vyama vya siasa, asasi za kiraia na kidini.
Jaji Warioba ameyasema hayo leo (Jumanne, Oktoba 16, 2012) katika mkutano kati ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala na uongozi wa Tume hiyo uliofanyika katika ofisi za Tume jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Mstaafu huyo baadhi ya viongozi hao na wadau wengine wanadhani maamuzi ya kazi ya kukusanya maoni inayofanywa kwa sasa na Tume yatamuliwa kwa kura na hivyo kuwalisha wananchi maoni ili wayatoa kwa Tume kwa wingi.
“Wengine wanafikiri huu ni wakati wa kupiga kura…hapana, sisi tunatafuta hoja,” alisema Mwenyekiti huyo na kuwataka wadau mbalimbali kuwaacha wananchi watoe maoni yao binafsi.
Awali akiongea katika mkutano huo, Mjumbe wa kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Muhambwe, Bw. Felix Mkosamali alipendekeza Tume iwe inagawa kwa wananchi fomu maalum za kujaza maoni yao siku kadhaa kabla ya Tume kufika ili kuwapa wananchi fursa ya kuandika maoni kwa kina tofauti na sasa ambapo Tume hutoa karatasi hizo kabla ya kuanza mkutano.
Akifafanua kuhusu hilo, Jaji Warioba amesema uamuzi wa Tume kugawa fomu hizo mkutanoni unalenga kupata maoni binafsi ya wananchi na kuongeza kuwa fomu hizo zikigawiwa mapema kuna uwezekano mkubwa kwa wananchi kujaziwa maoni na watu wengine.
“Uzoefu wetu umeonyesha hili la watu kuelekezwa nini cha kusema ambacho kwa kwli hawavijui kwa kina,” alisema katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Angellah Kairuki, Katibu wa Tume hiyo Bw. Assaa Rashid na Naibu Katibu Bw. Casmir Kyuki.
Pamoja na ufafanuzi kuhusu utoaji maoni binafsi ya wananchi, Mwenyekiti huyo pia aliwaeleza Wajumbe wa Kamati hiyo kuwa lengo la Tume ni kuhakikisha kuwa mchakato wote wa uandikaji wa katiba unakuwa wazi na wananchi wanashiriki kikamilifu.
“Tukimaliza kukusanya maoni, tutaingia hatua ya pili ya Mabaraza ya Katiba katika kila wilaya na baadhi ya taasisi ambapo tunataka wananchi wenyewe katika maeneo husika wachague nani awawakilishe katika mabaraza hayo,” alisema Mwenyekiti huyo.
Ufafanuzi huu ulifuatia swali la Mjumbe wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Kawe, Bi. Halima Mdee aliyeomba ufafanuzi kuhusu upatikanaji wa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ambayo yanapitia rasimu ya Katiba itakayowasilishwa na Tume.
Akifafanua zaidi, Jaji Warioba alisema Tume imepanga kufanya mikutano miwili katika kila wilaya ambapo wawakilishi wa wananchi watajadili rasimu ya Katiba itakayowasilishwa na Tume baada ya kukusanya maoni yao katika awamu ya kwanza.
“Ni hatua ambayo tunadhani itahitaji fedha nyingi hasa katika kuwasafirisha hao wawakilishi wa wananchi kuja katika mikutano…hatutaki kuona wananchi wanapata sababu ya kutoshiriki hatua hii muhimu,” alisema na kuwaomba Wajumbe wa Kamati kuzingatia hoja hizo pale Tume itakapoomba fedha zaidi.
Pamoja na maoni hayo, Wajumbe hao pia waliieleza Tume umuhimu wa kuongeza utoaji elimu kwa umma kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu Tume na Katiba.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Kairuki alisema Serikali itaendelea kuipa Tume hiyo kila aina ya ushirikiano ili itekeleze majukumu yake kwa ufanisi na kuwaomba Wabunge hao kuendeleza ushirikiano wanaoipa Tume hiyo.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269