Breaking News

Your Ad Spot

Oct 22, 2012

MARTHA: WANAOTUMIA FEDHA KUSAKA UONGOZI HAWAITAKII MEMA CCM

Martha Mlata

NA MWANDISHI WETU
MATUMIZI makubwa ya fedha katika uchaguzi ndani ya CCM na Jumuia zake yanayofanywa na baadhi ya wanachama wasio waaminifu, yameendelea kulalamikiwa ambapo, kwa sasa mikakati ya kuwadhoofisha wagombea wengine imebainika.

Miongoni mwa wagombea wanaodaiwa kuwa wako kwenye mtego wa kudhoofishwa ni Martha Mlata, ambaye anawania nafasi ya Mwenyekiti wa Wazazi Taifa.

Habari zilizopatikana zinadai kuwa, baadhi ya vigogo wanaohusishwa na mbio za urais katika uchaguzi mkuu wa 2015, wametenga fungu kubwa la fedha kuhakikisha mgombea wao anachukua nafasi hiyo.

Pamoja na Mlata, wanaowania Uenyekiti wa Wazazi Taifa, ni John Barongo na Abdallah Bulembo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya wajumbe walisema kuwa wanachama wanaotumia fedha kwa ajili ya kupanga safu ya uongozi hawana mapenzi mema na Chama na kwamba, wamelenga kukitumia kwa maslahi binafsi.

Hata hivyo, wamesema kuwa kamwe hawatakubali kuona hilo likifanyika na kwamba, wataingia kwenye chumba cha kupiga kura na kumchagua kiongozi bora na mwenye mapenzi mema na CCM.

"Mambo yanayoendelea ni machafu na hatutakubali yapite kama wanavyotaka, CCM ni ya Watanzania wote hivyo mambo ya watu wachache kupanga safu za uongozi hatutakubaliana nayo. Wameanza katika uchaguzi ngazi za wilaya, mikoa na sasa wanakuja taifa kwenye jumuia kuharibu," alisema mwanachama mmoja ambaye hakupenda kutajwa jina.

Mwana-CCM huyo alidokeza kuwa, uchaguzi wa UWT uligubikwa na vitendo vichafu na ukiukwaji wa taratibu ikiwa ni pamoja na matumizi makubwa ya fedha na kwamba, hata kuangushwa kwa Martha na Namelok Sokoine kulipangwa mapema.

Martha alikuwa akichuana na Namelok katika kuwania nafasi ya uwakilishi wa UWT katika Jumuia ya Wazazi, ambapo nguvu kubwa ya fedha ilitumika kumwagusha ili kutengeneza mazingira ya kumdhoofisha katika kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Wazazi Taifa.

Kwa upande wake Martha alipoulizwa, alisema ni muda mrefu amekuwa akifanyiwa kampeni chafu kwa lengo la kumwangusha katika harakati zake za kuwania nafasi hiyo, lakini hatimaye wajumbe ndio watafanya maamuzi.

"Mimi namwachia Mungu na waamuzi wa mwisho ni wajumbe wa mkutano mkuu wa Wazazi, kila kukicha nafanyiwa kampeni chafu ili nishindwe. Nia yangu ni kuitumikia jumuia na CCM na watanzania ili kusukuma gurudumu la maendeleo, sasa kama wengine wanatumia fedha kuharibu basi viongozi wataamua la kufanya," alisema Martha.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages