KILIMANJARO, TANZANIA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumatatu, Oktoba 29, 2012 ameendelea na ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika siku ya pili ya ziara yake ya siku nne katika Mkoa wa Kilimanjaro ambako amesimamishwa mara tisa na wananchi waliokuwa na hamu ya kumwona na kumsikiliza.
Mradi wa kwanza ambao Rais Kikwete ameukagua ni ujenzi wa nyumba za kisasa kwa ajili ya wahanga wa maporomoko ya ardhi ya mwaka 2006 katika kijiji cha Goha kilichoko Mamba Miamba katika Jimbo la Same Mashariki, Wilaya ya Same.
Katika kijiji hicho, Rais Kikwete amezindua ujenzi wa nyumba nane kwa ajili ya wahanga hao ambazo aliahidi kuwa Serikali ingewajengea wahanga hao wakati alipotembelea eneo hilo Desemba 18, 2006, kuhami msiba wa waliofariki na kuwafariji wafiwa.
Katika maporomoko hayo, watu 24 walipoteza maisha baada ya kufukiwa na ardhi ya maporomoko na wengine 25 waliumia.
Kiasi cha sh. milioni 150 zinatumika katika ujenzi wa nyumba hizo ambazo imepangwa kukamilika na kukabidhiwa kwa wenyewe Februari 5, mwakani, 2013.
Miongoni mwa wafadhili waliochangia ujenzi huo na huduma nyingine kwa ajili ya ujenzi wa nyumba hizo zenye vyumba vitatu, sebule na baraza ni pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu iliyotoa kiasi cha sh milioni 162, Kampuni ya Barrick Gold inagharimia uunganishaji wa maji kwa kiasi cha sh. milioni 38 na Benki ya National Micro-Finance Banki ilitoa sh milioni 9.7.
Mradi mwingine mkubwa wa maendeleo ambao Mhe Rais Kikwete amezindua ni Kiwanda cha Kisindika Tangawizi cha Mamba Miamba ambacho kinamilikiwa na Wana-Ushirika wa Wakulima wa Tangawizi katika Wilaya ya Same – Mamba Ginger Growers Cooperative ambacho ujenzi wake ulianza 2008.
Kiwanda hicho ambacho ujenzi wake na mitambo yake tayari imegharimu sh. milioni 348 kitakuwa na uwezo wa kuajiri watu 300, kitachangia kupunguza umasikini kwa kuongeza kipato cha wananchi na pia kitawapa wananchi zao la kudumu la biashara.
Kiwanda hicho ambacho michango ya ujenzi wake na kazi ya kukijenga ulisimamiwa kwa karibu na Mbunge wa Same Mashariki, Mheshimiwa Anna Kilango Malecela kina uwezo wa kusindika tani kati ya nane na 10 za tangawizi kwa siku na tani 2,220 kwa mwaka
Rais Kikwete alitoa mchango wake katika ujenzi wa kiwanda hicho kwa kuendesha harambee ya kuchangia ujenzi wa kiwanga hicho uliofanyika Oktoba 16, mwaka 2009 kwenye Hoteli ya New Africa, mjini Dar es Salaam. Kiasi cha sh milioni 287 zilipatikana kwenye harambee hiyo.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara baada ya kuzindua kiwanda hicho, Rais Kikwete amesisitiza umuhimu wa uongezaji thamani kwenye mazao ya wakulima nchini. Aidha, Rais Kikwete ameitaka Benki ya Raslimali Tanzania (TIC) kuongeza kasi katika kushughulikia maombi ya kiwanda hicho kwa ajili ya fedha za kufanya kazi (working capital).
Rais Kikwete pia ameweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa Hosteli kwenye shule ya wasichana ya Dkt. Asha Rose Migiro iliyoko mjini Mwanga katika Wilaya ya Mwanga.
Ujenzi wa Hosteli hiyo umegharimu kiasi cha sh.milioni 367 ambao umechangiwa na Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu iliyotoa sh. milioni 130, wafadhili wa shule hiyo kutoka Canada ambao mpaka sasa wametoa kiasi cha dola za Canada 200,000 na Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga ambayo mpaka sasa imetoa sh milioni 7.5.
Ujenzi wa shule hiyo ambayo ni wasichana na inafundisha masomo ya sayansi ulianza mwaka 2006 kama mradi uliobuniwa na Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Wilaya ya Mwanga lakini baadaye shule hiyo ilichukuliwa na Halmashauri ambayo iliendeleza ujenzi huo kama shule ya kata.
Shule hiyo ambayo ujenzi wake pia umekuwa unachangiwa na aliyekuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, Mheshimiwa Cleopa Msuya tokea mwaka 2009 mpaka sasa imefikia kidato cha tatu na wanafunzi 232. Shule ina wanafunzi 13.
Rais Kikwete anaendelea na ziara yake Mkoani Kilimanjaro kwa kufungua Barabara ya Mkuu-Tarakea wilayani Rombo na baadaye atafungua Jengo la Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269