Breaking News

Your Ad Spot

Dec 29, 2012

DIWANI CHADEMA AACHIA NGAZI SINGIDA


SINGIDA, Tanzania
SERA ya Mbunge wa Jimbo la Ikungi mashariki (CHADEMA) Tundu Lissu, ya kudaiwa kukataza wananchi kuchangia maendeleo yao, imesababisha  diwani wa chama hicho Kata ya Iseka Tarafa ya Ihanja, Amos Rubein Mughenyi, jimbo la Singida magharibi, kujiuzulu nafasi hiyo, Mwandishi Nathaniel Limu anaeleza kutoka Singida.

Akitangaza uamuzi huo mzito, mbele za waandishi wa habari, Amosi (Pichani) alisema amejiuzulu nafasi ya udiwani huo kuanzia Desemba 21 mwaka huu.

Alisema uamuzi wake huo ambao haujatokana na kushawishiwa wala kulazimishwa na mtu au chama cho chote cha siasa, umetokana na CHADEMA kumzuia kushirikiana na viongozi wa serikali ngazi ya wilaya na mkoa katika kusimamia shughuli za maendeleo.

Amosi alisema amekuwa akishinikizwa asikubaliane na changizo (michango) ya aina yo yote ya maendeleo ya Kata yake, kwa madai kuwa jukumu la kuwaletea maendeleo wakazi wa kata ya Iseka, ni la serikali pekee.

 “Hivi sasa Kamati ya maendeleo ya Kata ya Iseke (WDC), imeazimia kufanya harambee kwa ajili ya kutafuta fedha za ujenzi wa madarasa na maabara katika shule yetu ya sekondari. Tunapendekeza waziri wa ujenzi Dk. John Pombe Magufuli awe mgeni rasmi katika harambee hiyo, CHADEMA wamenigomea”,alisema Amosi kwa masikitiko makubwa.

 Alisema viongozi wa CHADEMA wilaya wamemtaka akae pembeni asijihusishe na harambee hiyo, na kama atalazimika ashiriki, basi mgeni rasmi awe ni askofu ye yote na sio kiongozi wa chama cho chote cha Siasa au wa serikali.

 “Nimeamua kwa ridhaa yangu mwenyewe kujiuzulu wadhifa huu, ili wananchi wangu wawe huru kujipangia shughuli zao za maendeleo bila kuzuiwa na itikadi ya CHADEMA baada ya mimi kuwa sio Diwani tena wa Kata hiyo”, alisema Amosi kwa kujiamini.

 Aidha ametumia fursa hiyo kuwaomba viongozi wa serikali na  hasa mkuu wa Wilaya ya Ikungi Manju Msambya, aendelee kuwaunga mkono wananchi wa Iseke, wafanikishe zoezi lao la harambee, ili waweze kujenga vyumba vya madarasa.

Kuhusu ni chama ngani anatarajia kujiunga,alisema ni mapema mno lakini muda si mrefu atatoa uamuzi wake kama ni kubaki kuwa mwanachama wa kawaida wa CHADEMA au atahama chama hicho,atatoa uamuzi wake.

Wakati huo huo,mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Singida,Illuminata Mwendwa,amekiri kupokea barua ya Amos kujiuzulu udiwani kata ya Iseke na kwamba wameishaijulisha TAMISEMI ili iweze kupanga tarehe ya uchaguzi mdogo wa kata hiyo.

Tundu Lissu mara kwa mara amekuwa akisikika  kuwa wananchi wa Jimbo lake watakuwa na likizo ya kutochangia maendeleo yake, hadi hapo Ubunge wake utakapokoma.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages