Breaking News

Your Ad Spot

Dec 2, 2012

HARAMBEE YA M4C YA CHADEMA HOI MWANZA


MWANZA, TANZANIA
WAKATI Chadema wamekuwa wakivuna kati ya sh. milioni 36 na milioni 52 katika harambee zao mkoani Mwanza, kiasi hicho kimeporomoka hadi kufikia sh. milioni 6 tu, katika harambee ya chama hicho iliyofanyika Novemba 30, mwaka huu jijini humo.

Hali hiyo inatafsiriwa na wadadisi wa maswala ya siasa hapa nchini kwamba, hiyo ni moja ya dalili za kuporomoka mvuto wa chama hicho uliokuwa umeanza kutanda katika baadhi ya maeneo nchini.

Habari kutoka ndani ya chama hicho hapa jijini Mwanza na kwa watu mbalimbali wakiwemo maarufu na baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa wamealikwa kwenye harambee hiyo ni kwamba wananchi wamepunguza morari kwa Chadema kutokana na ubabaishaji wa viongozi wengi wa chama hicho.

Katika harambee hiyo ya Mwanza, iliyofanyika kwenye Hotel ya Gold Crest, ikiongozwa na John Mnyika ambaye ni Mbunge wa Ubungo, kinyume na matarajio yake Chadema kiliambulia fedha taslimu sh. 6,180,000 tu.

Hiyo ni harambee ya tatu ya chama hicho kufanyika hapa jijini Mwanza na pekee kuambulia fedha kidogo , ya kwanza iliyofanyika katika hoteli hiyo kwa ajili ya kuchangia mfuko wa madawati, zilipatikana zaidi ya sh. Milioni 38 kati yake Milioni 10 zikitolewa na rais Jakaya Kikwete na ya pili iliyokuwa ya kuchangia madawati ambayo ilifanyika mwanzoni mwa mwaka huu, kwenye uwanja wa Sahara zikapatikana sh. milioni 52.

Wakati Chadema wakiambulia kiasi hicho cha sh. milioni sita, walikuwa wamekusudia kukusanya sh.Milioni 100 kutokana na maandalizi ya  harambee hiyo ambayo inasemekana yaligharim sh. milioni 15 hivyo kuonekana kuwa ni hasara kulingana na kiasi cha fedha kilichopatikana.

“Hii yote ni kwa sababu ya ubabaishaji, mkanganyiko, kauli na lugha za viongozi wetu akiwemo Mbunge wa jimbo hili (Nyamagana) Ezekia Wenje.” Alisema mwanachama mmoja wa chama hicho, ambaye alidai wakati wowote atatimka kwenye chama hicho.

“Mbunge wetu alikuwa akijiita mtoto wa mama ntilie lakini sasa naye amekuwa mfanyabiashara mkubwa wa madawa ya binaadamu, labda harambee zetu ndizo wanafungulia maduka huko Dar es Salaam, wanakon’gan’gania kuishi na kuwacha mama zao huku.”

Kwa mujibu wa viongozi wa M4C, wageni walialikwa kwenye harambee hiyo walitoka katika mikoa ya kanda ya ziwa ambayo ni Shinyanga, Simiyu, Mara, Kagera, Geita na Mwanza.

Viongozi hao walidai kuwa lengo la changizo hilio ni kukiwezesha Chadema kupata fedha za kuendesha kampeni katika uchaguzi mkuu ujao ili kiweze kushika dola mwaka 2015.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages