MOROGORO,Tanzania
ASKARI wawili wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wamekufa papo hapo baada ya kugongwa na gari mkoani Morogoro.
Kamanda wa polisi mkoani Morogoro Faustine Shilogile amesema leo kuwa tukio la kwanza la ajali ilitokea jana, saa 12 asubuhi katika eneo la Kambi ya Jeshi ya Mikumi iliyopo wilayani Kilosa.
Amesema ajali hiyo ilihusisha gari lisilofahamika namba wala dereva wake, kutokana na dereva kutimka na gari lake baada ya ajali hiyo wakati gari likitokea Ruaha kwenda Mikumi.
Kamanda amesema gari hilo lilimgonga askari MT 76810 Koplo Deogratius Lulakuze (37) ambaye alikuwa ni askari wa JWTZ kikosi namba SUUK-KJ mikumi na kufariki dunia papo hapo.
Katika tukio la pili askari wa JWTZ Boniface Nathaniel (29) mkazi wa jijini Dar es salaam, aligongwa na gari wakati akiendesha pikipiki kwenye barabara Mikumi iendayo Kilombero mkoani hapa.
Kamanda Shilogile amesema, ajali hiyo ilitokea juzi, saa 3 asubuhi katika daraja la Jeshi la wilaya ya Kilosa mkoani hapa.
Alisema kuwa askari huyo aligongwa na gari T 233 CDT lililokuwa na tela lenye namba T 687 CGE aina ya Scania lililokuwa likitokea Kilombero kwenda Mbeya likiendeshwa na Ismail Kunga (53) mkazi Tabata jijini DSM.
Alisema, gari hilo liligongana na pikipiki lenye namba T424 BYU aina ya Lantic lililokuwa likiendeshwa na askari huyo na kusababisha kifo chake papo hapo na kwamba chanzo cha ajali hiyo ni mwendesha pikipiki huyo kuzidi upande wa kulia zaidi wa barabara hiyo.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269