MAMA SALMA KIKWETE |
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ameagiza wafanyabiashara waliouza mahindi ya njaa nje ya mkoa wa Lindi wachukuliwe hatua kali ikiwemo kunyimwa vibali vitakavyotolewa hivi karibuni kwa ajili ya uingizaji wa mahindi mengine.
Pamoja na kunyimwa vibali, Mama Salma ameagiza uongozi wa mkoa uwaite wafanyabiashara hao na kuwahoji kwa nini waliamua kutoyaleta mahindi mkoani Lindi na badala yake kuyauza mkoani Dar es Salaam baada ya kuyanunua kwenye ghala la Taifa la hifadhi ya Chakula.
Mama Salma alitoa maagizo hayo, leo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kitumbikwela, Kata ya Msinjahili mkoani hapa, baada ya mwananchi mmoja, Dedani William kulalamikia mbele yake kwamba serikali ilitoa vibali ya ununuzi wa tani 400 za mahindi kwa ajili ya kupunguza mfumuko wa bei uliosababishwa na maeneo kadhaa kukumbwa na njaa, mwaka jana lakini waliopata vibali hawakuyafikisha kama ilivyotakiwa.
Alisema, ni tani 20 tu zilizofikishwa Lindi na mfanyabiashara mmoja aliyemtaja kwa jina moja la Rada ambaye alikuwa amepewa kibali cha kununua tani 100 lakini tani 80 kati ya hizo inadaiwa aliziuza Dar es Salaam.
Mwananchi huyo aliendelea kudai kwamba wafanyabiashara wengine waliopewa vibali lakini wakauza mahindi yote Dar es Salaam badala ya kuyaingiza Lindi aliwataja kwa jina moja moja kuwa ni, Faridi tani 70, Hadela tani 100 na Ramadhani Machelu ambaye hakutaja kiwango alichotakiwa kununua.
Alisema vibali vilikuwa vinatolewa na Ofisi ya Ofisa Tawala wa mkoa wa Lindi na kwamba yeye ni miongoni mwa wananchi walioomba vibali lakini wengi walinyimwa.
"Kitendo hiki cha kuuza mahindi Dar es Salaam ni kosa kubwa, kama watu hawa wanajulikana waitwe na kuhojiwa kisha wachukuliwe hatua kali, na pia hawa watu wasiwe miongoni mwa watakaopewa vibali vya ununuzi wa tani nyingine 176 za mahindi ya njaa yanayotakiwa kufikishwa Lindi wiki mbili zijazo", alisema Mama Salma na kuongeza;
"Baada ya wafanyabiashara hao kuhojiwa viongozi wahakikishe wanatoa majibu kwa wanannchi kuhusu ubadhirifu huo kwa kuwa dawa ya moto ni maji, si moto".
Kwa mujibu wa utaraibu, vibali hutolewa kwa wafanyabiashara kwa ajili ya kununua bidhaa kama mahindi kwa bei nafuu ili kwenda kuwauzia wananchi kwa bei nafuu zaidi kuliko bei za kawaida kutokana na hali halisi inayokuwa imekuba eneo husika.
Katika ziara hiyo ya Mama Salma, yamejitokeza malalamiko kutoka kwa wananchi kukabiliwa na njaa kutokana msimu uliopita wa kilimo kutopatikana mavuno ya kutosha katika maeneo mbalimbali mkoani Lindi.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269