DODOMA, Tanzania
Kamati ya Maadili, Kinga na Madaraka ya Bunge imewatia hatiani wabunge wanne wa Chadema kuhusiana na vurugu zilizotokea bungeni wiki iliyopita.
Wabunge hao ni pamoja Joshua Nassari Arusmeru Masharuiki), Tundu Lissu (Singida Mashariki), John Mnyika (Ubungo) Pauline Gekul (viti maalum)
Akitoa taarifa ya uchunguzi bungeni leo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Brigedia Hassn Ngwilizi amesema kamati yake, ilipewa kazi ya kuchunguza chanzo cha vurugu zilizotokea bungeni Februari 4 mwaka huu, wakati Mnyika alipowasilisha hoja binafsi ambayo aliitaka Serikali kuchukua hatua za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar es Salaam.
Ngwilizi alisema Kamati hiyo ilitumia picha za televisheni za TBC kuwatambua wabunge waliohusika na vurugu hizo.
Alisema kwa mujibu wa Kanuni za bunge za 60 na 68 zinaeleza mchakato wa majadiliano bungeni huku ikitoa nafasi kwa mbunge kutoa taarifa bungeni na kwamba wakati wa hoja ya Mnyika kanuni hizo hazikuzingatiwa.
“Wakati wa hoja ya Mnyika kanuni hizo hazikuzingatiwa, kanuni ya 60 (2) inamtaka mbunge asizungumze hadi atakaporuhusiwa na Spika, lakini siku hiyo wabunge walisimama bila kuruhusiwa na kuwasha vipaza sauti na kuanza kuzungumza.” alisema.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo kanuni ya kumtaka mbunge kukaa chini wakati Spika anazungumza haikufuatwa.
“Kumbukumbu zinaonyesha Mnyika alisimama kutaka kuhusu utaratibu ingawa Naibu Spika, Job Ndugai alikuwa amesimama, hatua hii inaonyesha utovu wa nidhamu. Wabunge wengine walioonesha utovu huu wa nidhamu ni Tundu Lissu, Joshua Nassari na Pauline Gekul, wabunge hawa walisimama na kuzungumza maneno kama kanuni ‘zifuatwe’ ‘unabaka kanuni hali iliyoamsha ari kwa wabunge wengine kupiga kelele,” alisema
Ngiwilizi alisema Nassari pia alikiuka kanuni ya 5(4) kwa kubishana na Naibu Spika kwani kanuni hiyo inamtaka Mbunge asiyeridhika na uamuzi wa Spika kukata rufani.
Akielezea kama kanuni zilivunjwa wakati wa hoja hiyo, Ngwilizi alisema Naibu Spika alivunja kanuni kwa kukubali muongozo wa Lissu kuwa Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe asijadili hoja ya Mnyika kwa dakika 30 kwa kuwa hakuwa mtoa hoja.
Alisema kwa mujibu wa kanuni ya 62 (1) na 53 (6c) inatoa muda kwa waziri kuchangia kwa muda wa dakika 30 na sio kuchangia kama mbunge mwingine kwa dakika 15, aidha, alisema dhana ya Profesa Maghembe ya kuondoa hoja ya Mnyika haikuwa sahihi kwa mujibu wa kanuni mtoa hoja ndiye anapaswa kuondoa hoja yake.
Alisema hata hivyo azimio la Profesa Maghembe lilikuwa kulitaka Bunge kukubali Serikali iendelee utekelezaji wa miradi ya maji inayoondelea katika Jiji la Dar es Salaam.
“Kwa hiyo hoja ya Waziri haikulenga kuondoa hoja ya Mnyika bali ililenga kulitaka bunge kuazimia azimio jipya,” alisema Ngwilizi.
Kuhusu uamuzi wa Naibu Spika kusitisha mjadala na kuwahoji wabunge juu ya hoja husika, Ngwilizi alisema Ndugai alikuwa sahihi kwa mujibu wa kanuni.
“Kamati imejiridhisha kuwa hoja za kukosekana kwa utulivu hazikusababishwa na ukiukwaji wa kanuni kama ilivyodhaniwa na wabunge,” alisema.
Kwa upande wake Spika wa Bunge, Anne Makinda alisema kwa kuzingatia haki ya asili ya binadamu ya kusikilizwa,wabunge walioonyesha kufanya uchochezi hawakupata nafasi ya kukutana na kamati na kuhojiwa.
Alisema hatua ya kutoa adhabu kwa wabunge hao itafikiwa mara tu baada ya kuhojiwa na Kamati hiyo.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269