DAR ES SALAAM, Tanzania
Wanaharakati wanaojumuika katika kupinga unyanyasaji wa kijinsia kesho, tarehe 7, Februari, 2013 watakutana na waandishi wa habari ili kuwaarifu na kubadilishana mawazo juu ya matokeo ya taarifa za awali kuhusu hali ya ukatili wa kijinsia katika wilaya 10 za Tanzania bara na Zanzibar. Mkutano huo utafanyika katika Ofisi za Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania, (TAMWA), Sinza Mori, Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa TAMWA, Valerie Msoka, inasema kuwa taarifa hizo zilizokusanywa miezi miwili iliyopita zilikuwa na lengo la kuangalia mitizamo ya watu na hali ya upambanaji dhidhi ya unyanyasaji wa kijinsia katika ngazi za vijiji na wilaya.
Alisema taarifa za utafiti huo zitasaidia mashirika hayo kupanga mikakati ya pamoja ya kukabiliana na vitendo hivyo ambavyo vinaathiri zaidi wanawake na watoto.
“Mashirika haya yana dhamira zinazokaribiana za kufahamisha na kujenga uelewa, kuzuia na kutetea haki kwa waathirika kwa hiyo tukiungana nguvu tunaamini tutaleta mabadilko makubwa sana”, alisema.
Mashirika yanayohusika katika mpango huu ni Chama cha Wanasheria wanawake (TAWLA), Chama cha Wanasheria wanawake Zanzibar (ZAFELA), Shirika la Usuluhishi wa Migogoro (CRC), Mtandao wa Kijinsia wa Wanawake (TGNP) na Chama cha Wanahabari wanawake Tanzania,bara na Zanzibar (TAMWA).
Alisema mashirika ya TAWLA, CRC na ZAFELA yatahusika na kusimamia masuala ya kisheria, wakati TGNP itatoa elimu ya kijinsia na TAMWA itatoa taarifa kwa jamii kupitia vyombo mbali mbali vya mawasilano.
Wilaya 10 zitakazofaidika na mpango huo unaojulikana kwa jina la Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake (GEWE) ni pamoja na Wete(Pemba kaskazini), Magharibi (Unguja), Kusini Unguja (Kusini Unguja), Kisarawe (Pwani), Newala (Mtwara), Lindi vijijini (Lindi), Mvomero (Morogoro) na wilaya mbili za Kinondoni na Ilala,(Dar es Salaam).
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269