Breaking News

Your Ad Spot

Feb 10, 2013

WAZIRI KABAKA KUZINDUA KAMPENI YA KUZUIA UNYANYASAJI


NA MWANDISHI WETU, DODOMA
SERIKALI imeshauriwa kuangalia upya adhabu zinazotolewa kwa watu wanaofanya vitendo vya unyanyasaji kwa wanawake na watoto nchini.

Ushauri huo umetokana na kuendelea kushamiri kwa vitendo vya unyanyasaji huku vyombo na mamlaka husika vikishindwa kutoa adhabu kali kwa lengo la kukomesha.

Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka (pichani kulia), aliyasema hayo mjini hapa jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa Kampeni ya Okoa Mtoto wa Kike Tanzania.

Kwa kuanzia kampeni hiyo itazinduliwa Wilaya ya Tarime mkoani Mara, na baadaye kusambaa kwenye maeneo mbalimbali nchini hasa yaliyoshamiri kwa vitendo vya unyanyasaji kwa wanawake na watoto.

Gaudentia, ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, alisema licha ya kuwepo kwa sheria lakini bado vitendo vya unyanyasaji vimezidi kushika kasi, jambo linaloashiria kuwa adhabu zinazotolewa bado ni ndogo.

“Unyanyasaji umekuwa kwa kiwango kikubwa mno na umekuwa ukirudisha nyuma maendeleo ya wanawake nchini. Sheria zipo na watu wanapewa adhabu, lakini tunadhani kuna kila sababu ya kuangaliwa upya ili kukomesha kabisa vitendo hivi,” alisema Gaudentia.

Alisema zaidi ya moja ya tatu ya wanawake nchini wameshakabiliana na ukatili wa kijinsia na kwamba, mgawanyo wa unyanyasaji ni mkubwa zaidi kwa wanawake hasa waliotalikiwa na wajane.

“Hili ni tatizo kubwa kwani, utafiti unaonyesha asilimia 23 ya wasichana wenye umri kati ya 15 hadi 19 tayari wamejifungua, hivyo kushindwa kuendelea na masomo kwa ajili ya kuajiandaa na maisha yao ya baadaye,” alisema.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Nyumbani Kwanza Media Group (NMG), Mossy Magere (kushoto pichani), alisema kampeni hiyo itazinduliwa rasmi Machi 3, mwaka huu.

Alisema wameamua kushirikiana na Gaudentia kutokana na kuwa mstari wa mbele kutetea haki za wanawake na kwamba, tatizo hilo la unyanyasaji limekuwa kubwa mkoani Mara.

Mossy alisema kampeni hiyo itakuwa endelevu na kwamba, itakwenda sambamba na uanzishwaji wa klabu za kupinga unyanyasaji katika shule mbalimbali kwa lengo kuleta usawa.

“Unyanyasaji wa kijinsia unaumiza wanawake na watoto wengi nchini, ni lazima jamii ikubali kubadilika ili kila mtu awe na furaja katika maisha badala ya wengine kufikia hatua ya kujuta kuzaliwa,” alisema Mossy

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages