JAJI WARIOBA |
Na Hussein Makame na Genofeva Matemu-Maelezo
TUME ya Mabadiliko ya Katiba inajiandaa kutengeneza rasimu ya Katiba Mpya itakayozingatia maoni ya wananchi ambayo inatarajiwa kutolewa Juni mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Joseph Warioba wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusu mchakato wa uundwaji wa katiba mpya.
Aidha Jaji Warioba amesema wakati utakapofika anawaomba wananchi waipitie rasimu hiyo, waijadili na kutoa maoni bila ya woga kama walivyofanya wakati wa kukusanya maoni.
Jaji Warioba alitoa wito kwa viongozi wa vyama vya siasa, jumuiya na taasisi nyingine kuwaachia wananchi watoe maoni yao kuhusu rasimu hiyo bila ya kuwaingilia.
Alisema, tume hiyo iko tayari kufanya maamuzi magumu ya kuainisha mambo muhimu yaliyopendekezwa katika mchakato wa kukusanya maoni, mfano masuala ya Muungano, Madaraka ya Rais na majimbo ambayo kila mwananchi amependekeza kwa jinsi anavyotaka yeye, lakini ni lazima tume ichague moja kati ya maoni hayo na kuyaacha mengine.
“Tumefanya uchambuzi wa maoni ya wananchi, kwa kweli ni mengi sana, hivyo tume iko tayari kufanya maamuzi magumu ya kuweka maoni ambayo ni ya msingi, hivyo tunaomba wananchi wawe tayari kuyakubali kwa kuwa haiwezekani kila maoni ya mwananchi yakachukuliwa”, alisema Jaji Warioba.
Aliongeza kuwa baada ya rasimu hiyo kutengenezwa, tume hiyo itaunda mabaraza ya katiba ya watu wenye ulemavu ili kuwapa fursa walemavu kutoa maoni yao kuhusu rasimu hiyo.
“Walemavu hawakusahaulika, lakini tuliona tufanye utaratibu maalum wa kupata wawakilishi kutoka makundi 10 ya walemavu kupitia vyama vyao vya Tanzania Bara na Zanzibar”, alibainisha Jaji Warioba.
Akizungumzia uchaguzi wa wawakilishi wa mabaraza ya katiba ya kata na shehia, Jaji Warioba alisema jumla ya kata 3,331 kati ya kata 3,339 zimekamilisha vizuri mchakato wa kuwapata wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya.
Alisema kwa upande wa Zanzibar, shehia 323 kati ya 335 zimekamilisha vizuri mchakato wa kuwapata wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya.
“Hivyo kuna shehia 12 za Zanzibar na kata 3 za Tanzania hazijakamilisha uchaguzi wake kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mivutano ya kisiasa, kidini na rushwa” alifafanua Jaji Warioba.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269