Breaking News

Your Ad Spot

Jun 18, 2013

POLISI: MBOWE NA LEMA WALETE USHAHIDI HARAKA, WASIPOFANYA HIVYO TUTAWAKAMATA

MBOWE
NA LILIAN JOEL, ARUSHA.
MKUU wa operesheni na mafunzo wa jeshi la polisi nchini Kamishna Paul Chagonja amewataka Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na mbunge wa Arusha mjini Godbles Lema kuhakikisha kesho wanawasilisha ushahidi kwake kuhusu tuhuma zao kuwa mtu aliyelipua bomu katika mkutano wao ni askari wa jeshi hilo wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) mkoani Arusha, vinginevyo watakiona cha moto.

Pia alimtaka mbunge wa jimbo la Arumeru Mashariki Joshua Nassari kuondoka katika hospitali ya Selian alikolazwa akidai kuumuizwa kwa kipigo kutoka kwa vijana wa kimasai (Morani) jambo ambalo limekanushwa na madaktari wa hospitali hiyo kwakua hana jeraha wala uvimbe wowote ili akabiliane na kesi ya kutishia kuua kwa silaha inayomkabili.

Aidha Kamishna Chagonja alisema kufuatia tukio hilo tayari jeshi lake limeshawakamata watu watatu toka ndani na nje ya nchi wanaohisiwa kuhusika na tukio la ulipuaji wa bomu na kwamba wanaendelea kuhojiwa kuhusiana na tukio hilo.

Kamishna Chagonja ametoa kauli hiyo leo alipokua akizungumza  na vyombo vya habari kuhusu tukio la mlipuko wa bomu jijini hapa katika viwanja vya Soweto katika kata ya Kaloleni mwishoni mwa wiki katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema.

Chagonja alisema jana jumatatu Mbowe na Lema walifika katika makao makuu ya jeshi la polisi mkoani Arusha na kudai kuwa wanaushahidi wa kutosha kuhusu tukio la mlipuko wa bomu katika mkutano wao na kusema kuwa walipiga picha za tukio zima na kusema kuwa bomu hilo lilirushwa na askari.

Pia kamanda Chagonja alisema anashangazwa na kauli za viongozi hao zinazokinzana maana siku ya jumapili Lema alifika katika makao hayo makuu ya polisi mkoani Arusha na kulishukuru jeshi hilo kwa namna lilivyoonyesha ushirikiano wa kina katika kuwanusuru wao,washabiki wao pamoja na majeruhi watukio hilo na kukiri kwamba jeshi hilo halihusiki kwa namna yoyote na tukio hil.

“Namshangaa Lema maana alifika katika makao haya makuu na kunikuta mimi binafsi ambapo alinieleza kuwa analishukuru jeshi la polisi kwa jinsi lilivyoonyesha ushirikiano katika kuwanusuru wao, wafuasi wao pamoja na mjeruhi na kusisitiza kuwa polisi haiusiki katika tukio hili lakini leo hii anakuja na Mbowe wanasema polisi ndiyo walihusika kwa askari wake kurusha bomu lile”alisema Chagonja.

“tunawataka Freeman Mbowe na Lema wawasilishe ushahidi wanaodai kuwa wanao wa mtu aliyerusha bomu katika mkutano ule, na kama wautawasilisha ushahidi huo utafanyiwa kazi bila kuangalia itikadi lakini kinyume na hapo chamoto watakiona maana tutawakamata pamoja na huyo mwenzake aliyeko honeymoon Selian’ alisema na kuongeza.

Aliongeza kuwa mwananchi ambae alikua wakala wa CCM katika uchaguzi huo Hussein Warsama aliyedai kutishiwa kuuawa kwa bastola na mbunge Nassari tayari ameshafika katika kituo hicho cha polisi kushitaki juu ya tukio hilo hali ambayo ni lazima mbunge huyo akamatwe ili kujibu tuhuma zinazomkabili.

“sasa yeye anadai kupigwa lakini hajatoa malalamiko yake rasmi sisi tuna jalada moja tu linalomtuhumu yeye na kumpiga na kumtishia kumuu kwa bastola wakala wa CCM sasa sisi tunasema tunashughulika na jalada lililotufikia yeye atoke pake aje apambane na kesi yake”alisema Chagonja.

Aidha Kamishna Chagonja alisema kufuatia tukio hilo tayari jeshi lake limeshawakamata watu watatu toka ndani na nje ya nchi wanaohisiwa kuhusika na tukio la ulipuaji wa bomu na kwamba wanaendelea kuhojiwa kuhusiana na tukio hilo.

Akizungumzia kuhusu tukio hilo kaimu mganga mkuu wa hospitali ya Selian iliyo na majeruhi wengi wa tukio hilo Paul Kisanga alisema majeruhi wote waliopatiwa matibabu hospitalini hapo wametolewa katika miili yao vipande vidogovodogo vya chuma hali inayoashiria kuwa walilipuliwa kwa bomu na sio risasi kama inavyodaiwa.

Dk.Kisanga alisema pamoja na uelewa wake mdogo katika masuala ya utambuzi wa mambo ya mlipuko hadhani kama watu hao walipigwa kwa risasi ila anaamini sampuli zilizochukuliwa kwaajili ya uchunguzi zitatoa majibu yaliyo sahihi kuhusu nini kilichowalipukia majeruhi hao.

“mi naomba niseme tulichokiona katika miili ya majeruhi hawa ni vipande vidogovidogo vya chuma sasa sijui kama ni bomu au risasi lakini kwa uelewa wangu nahisi kama ni bomu ila tusubiri majibu ya wataalamu wa mambo hayo”alisema Dk.Kisanga.

Pia aliishukuru serikali kwa msaada wa hali na mali waliowapatia ambao unawawezesha kuendelea kutoa huduma zilizo bora kwa majeuhi kwakua hadi sasa tayari wana madaktari wawili wataalamu wa mifupa kutoka kiteno cha MOI Muhimbili pamoja na madaktari kadhaa wataalamu wa mabomu kutoka hospitali ya jeshi ya Lugalo jijini Dar es salaa wanaoendelea kushirikiana katika kazi ya huduma kwa amjeruhi.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages