Breaking News

Your Ad Spot

Jul 30, 2013

NDEGE YA MADAKTARI YAPATA AJALI ARUSHA, SITA WANUSURIKA KIFO

NA LILIAN JOEL, ARUSHA
Watu sita wamenusurika kifo baada ya ndege ndogo ya madaktari maalum (Flying doctors), wanaotoa huduma katika vijiji vya jamii ya wafugaji wa Kimaasai imeanguka leo katika eneo la kijiji cha Kipenjiro, wilayani Ngorongoro.
Habari zilizopatikana kutoka Ngorongoro na kuthibitishwa na Mbunge wa Ngorongoro, Saning’o Telele zimeeleza kuwa ndege hiyo iliyokuwa na abiria saba ilianguka kati ya Saa 9:00 na 10:00 alasiri.
“Ni kweli ndege ndogo ya Flying doctors wa Kanisa Katoliki inayotoa huduma za kitabibu katika vijiji kadhaa wilayani Ngorongoro imeanguka leo ila ni bahati nzuri hakuna taarifa ya vifo hadi hivi sasa,”alisema Mbunge Telele kwa njia ya simu.
Mbunge huyo alitaja baadhi ya vijiji ambavyo madaktari hao hutoa huduma kuwa ni Naiyobi, Ngarasero, Olitatiro na Endulen.
Kwa mujibu wa Telele, majeruhi wote waliokuwepo ndani ya ndege hiyo walikimbizwa hospitali ya Seliani Jijini Arusha kwa matibabu baada ya shirika linalomiliki ndege hiyo kutuma ndege nyingine kuwachukua kutoka eneo la ajali.
Taarifa zilizopatikana kutoka hospitali ya Endulen inayomilikiwa na Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Arusha zinasema ndege hiyo ilikuwa na daktari mmoja na wauguzi wawili kutoka hospitali hiyo ambao majina yao hayakupatikana mara moja.
Pamoja na daktari na wauguzi, ndege hiyo pia ilikuwa na marubani wawili na wagonjwa wawili ambao ni mama na mtoto wake.
Vijiji ambavyo Flying doctors hufika kutoa huduma kwa ndege hiyo ni vile visivyokuwa na huduma ya kitatbibu na hazifikiki kirahisi kwa njia ya barabara.
Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Lebaratus Sabas alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo lakini hakuwa tayari kuizungumzia kwa undani kwa maelezo kuwa hajapokea taarifa rasmi za kutosha kutoka kwa maafisa wake walioko wilayani Ngorongoro kutokana na mazingira halisi ya jiografia ya wilaya hiyo kimawasiliano.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages