Breaking News

Your Ad Spot

Aug 4, 2013

WASHIRIKINA WAMUUA KIKONGWE MBEYA

MBEYA, Tanzania
KIKONGWE mwenye umri wa miaka 70, mkazi wa kijiji cha Lumbela, wilayani Mbozi, ameshambuliwa na kuuawa na watu wasiofahamika, kwa kukatwakatwa kwa shoka
 
Katika tukio hilo, linalohusisha imani za kishirikina, mkewe aitwaye Esther Mgala (60), alijeruhiwa sehemu za mkono wa kulia na kichwani, wakati akijaribu kumsaidia mumewe.
 
Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya,Diwani Athuman, alisema tukio hilo la mauaji lilitokea Agosti 2, mwaka huu saa 1:00 usiku katika kijiji cha Lumbila, wilayani humo na kumtaja marehemu kuwa ni Msawile Halinga (70).
 
Alisema katika kufanikisha mauaji hayo, wauaji hao walitumia mbinu ya kumuita marehemu sehemu za gizani na kisha kuanza kumshambulia kwa shoka na hatimaye kumuua.
 
Athuman alisema: “Chanzo cha mauaji hayo ni imani za kishirikina na juhudi za kuwasaka watuhumiwa waliohusika na tukio hili la kinyama zinaendelea kufanyika ili kuwafikisha mbele ya sheria” alisema Athuman.
 
Alitoa wito kwa jamii mkoani Mbeya, kuacha mara moja tabia ya kuwaua wazee na vikongwe kwa dhana ya kishirikina kwani ni kinyume cha sheria na kutumia fursa hiyo kutoa rai kwa mtu yeyote mwenye taarifa juu ya waliohusika na tukio hilo.
 
Aliwataka kutoa taarifa hizo kwa mamlaka zinazohusika ili wakamatwe na hatua zaidi za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.
 
Wakati huo huo, mkazi wa Mpumbuli wilayani Rungwe, Lucas Mwakyoma (50), ameuawa na mdogo wake kwa kupigwa fimbo sehemu za kichwani na kuvunjwa shingo, wakigombea mashamba.
 
Athuman alisema tukio hilo lilitokea kati ya Julai 30 na 31, mwaka huu na kuwataja watuhumiwa wa mauaji hayo kuwa ni Ramadhan Mwakyoma (45) akishirikiana na mwanafunzi wa kidato cha pili, sekondari ya Mpumbuli, Godwin Mwakyoma (16).
 
Kwa mujibu wa Kamanda Athuman, baada ya watuhumiwa hao kumuua Mwakyoma, walimfukia kwenye shimo la urefu wa futi mbili na mwili huo uligunduliwa na kufukuliwa Agosti 3, mwaka huu saa 10:00 alasiri, kisha kuzikwa upya baada ya uchunguzi wa daktari.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages