MWENYEKITI wa Jumuia ya wazazi
mkoani Tanga, Dk. Edmund Mndolwa (pichani), amesema kuna mikakati ya haraka ya
kuboresha shule za jumuia hiyo ili ziweze kutoa elimu bora.
Alisema
shule za Jumuia ya wazazi zilikuwa kimbilio la wazazi na Watanzania kwa
jumla, lakini kwa sasa zinakabiliwa na soko la ushindani kutokana na
shule nyingi za kata na binafsi.
Akizungumza katika ziara ya
kutoa shukrani katika mkoa wa Tanga kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa
Jumuia hiyo, Dk. Mndolwa alisema shule za wazazi zote nchini
zinakabiliwa na uhaba wa walimu, vitendea kazi na vitabu.
Alieleza
kuwa shule hizo zimekuwa na tatizo la mfumo wa uendeshaji wake, kitu
kinachochangia kujiendesha kiholela na wakuu wa shule kuzichukulia kama
zao.
“Tunatakiwa kubadilika na kuzirejesha shule zetu katika
hali yake ya zamani. Kwa kufanya hivyo, tutawafanya Watanzania waendelee
kuzikimbilia shule hizo ambazo zilikuwa mkombozi kwao,
“Tushirikiane
kuanzia wazazi kwa kulipa ada ili walimu wapate mishahara mizuri na
wakipata mishahara mizuri watafundisha kwa ari na moyo, hivyo hata
watoto wetu watapata elimu nzuri,”alieleza Dk. Mndolwa.
Dk. Mndolwa alisema kuwa mkoa wa Tanga una shule za wazazi sita huku nchi nzima kukiwa na shule za wazazi 71.
Aidha,
akizungumza katika wilaya za Mkinga, Muheza na Pangani, Dk. Mndolwa
aliwataka viongozi wa jumuia hiyo kuwa watumishi wa watu kwa kwenda
kusikiliza kero zao katika ngazi za chini badala ya kujifungia ofsini.
Vilevile,
aliwataka viongozi hao kuachana na dhuluma kwa wanachama wanapokuwa
wanaomba nafasi ya uongozi, kwani kwa kuendeleza dhuluma kunachangia
kupunguza nguvu ya chama.
“Unakuta mwanachama anakubalika na
wananchi lakini kwa sababu ya chuki na dhuluma anapewa mtu mwingine
ambaye hakuongoza kura za maoni, hali ambayo hujenga chuki kwa wanachama
na kuamua kuwapigia kura wapinzania,
“Ukiangalia, nafasi
nyingi tulizopoteza katika ngazi mbalimbali kuanzia wenyeviti wa
serikali za mitaa, udiwani na ubunge, nafasi nyingi zimetokana na
dhuluma, na waliowachagua wapinzania ni wanaCCM wenyewe kwa sababu ya
kuchukizwa kwa mtu waliyempenda kutorudishwa jina lake,”alieleza.
MWENYEKITI wa Jumuia ya wazazi mkoa wa Tanga, Dk. Edmund Mndolwa, wa nne kulia, akiwa na baadhi ya viongozi wa bodi ya Shule ya Sekondari Shemvua iliyoko wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, wanafunzi wa shule hiyo na viongozi wa jumuia hiyo mkoani Tanga. shule hiyo inamilikiwa na jumuia ya wazazi.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269