KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL), kupitia kinywaji chake cha Ndovu Special Malt, imeanzisha kampeni maalumu kwa ajili ya kusaidia usambazaji habari na elimu juu ya uhifadhi wa tembo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Meneja wa Ndovu Special Malt, Pamela Kikuli alisema, kampeni hiyo maalumu itafanyika Jumapili hii ambayo ni siku ya Taifa ya Uhifadhi wa Tembo.
“Kwa siku wastani wa tembo 30 wanauawa na majangili, hivyo kasi ya kutisha ya kutekekezwa kwao inayofanywa kwa wanyama hawa wapole na wakubwa, inahitaji jitihada zetu sote,” alisema.
Pamela alisema, wanataka kutumia mitandao ya kijamii katika kufanikisha hilo na watatumia njia iitwayo ‘Ndovu Defender app’ katika kuhakikisha wengi wanapata taarifa sahihi na kushiriki katika kampeni ya kuwahifadhi wanyama hao.
Alifafanua kuwa mpango huo wa ‘Ndovu Defenders’, utapatikana katika kurasa ya facebook ya kinywaji cha Ndovu, ambao utakuwa ni mchezo maalumu, ambapo kila mshiriki mpya atalazimika kuchangia Sh 1,000 ambazo zitakusanywa na kutumika katika kampeni ya uhifadhi wa Tembo.
“Wapenzi wa bia ya Ndovu wanaweza kutoa mchango wao katika kampeni hii kwa kutembelea kurasa ya facebook ya Ndovu na kushiriki mchezo huo, kumbuka kurasa yetu ina mashabiki zaidi ya 44,000 hivyo itakuwa njia rahisi zaidi ya kuwapa ujumbe.
“Mbali na hilo, tutatumia njia nyingine za ukusanyaji wa fedha na katika hili bia ya Ndovu inaamini itafanikiwa kuwalinda na kuwatetea wanyama hawa,” alisema Pamela ambao pia walikabidhi fulana na kofia zitakazotumika kwa washiriki siku hiyo.
Naye Meneja Habari na Mawasiliano wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Editha Mushi alisema, mkakati huu wa kuelimisha jamii juu ya uhifadhi wa Tembo ambapo bia ya Ndovu Special Malt inashirikiana na wadau wengine kufanikisha mpango huo.
Akiongelea umuhimu wa maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Taifa ya Tembo, Mwenyekiti wa Kamati ya Siku ya Taifa ya Tembo, Profesa Mng’ongo alisema, kwa sasa Tembo wanateketea mno, hivyo siku hiyo ni muhimu zaidi.
“Siku hiyo ni muhimu zaidi kwetu, kwani mnyama huyo kwa sasa anawindwa kila siku, hivyo ni muhimu kutambulishana taratibu na mikakati ya jinsi ya kulinda idadi ya tembo waliobaki hapa nchini kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Tathimini ya Rasilimali ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (IRA), Profesa Amos E. Majule, alisema, kwa sasa tembo wanateketea mno, hivyo siku hiyo ni muhimu zaidi kwa Watanzania kuungana katika hili.
Siku hiyo inatarajiwa kutanguliwa na maandamano yanayotarajiwa kuanza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kuishia katika Ukumbi wa Mlimani City, ambapo wadau wa uhifadhi watatoa hotuba na kutafanyika maonyesho ya kuifahamisha jamii umuhimu wa uhifadhi wa tembo walio hatarini kutoweka.
UDSM ndio walioandaa siku hiyo kwa kushirikiana na kituo chake cha IRA, pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii, World Wide Fund for Nature (WWF), Wildlife Conservation Society (WCS), Tume ya Sayansi na teknolojia Tanzania (COSTECH) pamoja na wadau wengine.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269