Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Ijumaa, Septemba 20, 2013, ametunukiwa Shahada ya Uzamivu (PHD) na Chuo Kikuu cha Guelph katika jimbo la Ontario nchini Canada kwa kutambua mchango na uongozi wake katika kuleta mageuzi ya kilimo katika Afrika. Taarifa iliyotokewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, imesema.
Taarifa hiyo Imesema, viongozi wa Chuo hicho wanasema kuwa wamefanya uamuzi wa kumtunuku Rais Kikwete kutokana na jitihada zake za kukabiliana na changamoto zinazokabili kilimo, jitihada zake za kuleta usalama wa chakula na pia majaribio makubwa ya kuongeza matumizi ya technolojia katika kilimo cha Tanzania na Afrika.
Rais Kikwete ambaye amewasili Canada usiku wa Alhamisi, Septemba 19, 2013 akitokea Washington, D.C., Marekani ambako alikuwa kwa siku mbili akitokea Jimbo la California amekuwa Mtanzania wa kwanza kutunukiwa shahada ya juu kabisa katika historia ya Chuo hicho.
Chuo cha Guelph ni moja ya vyuo vikuu vinavyoheshimiwa zaidi katika Canada na duniani katika Nyanja za kilimo na kilianzishwa rasmi kama Chuo cha Kilimo cha Jimbo la Ontario Mei Mosi, mwaka 1874.
Chuo hicho ambacho kimejipatia umaarufu kutokana na ubora wa shughuli zake za utafiti kimekuwa katika mstari wa mbele kutafuta majawabu ya changamoto zinazoikabili dunia katika masuala ya kilimo, raslimali za maji, matatizo makubwa ya magonjwa ya mimea, matatizo ya ukuaji haraka wa miji duniani na changamoto za biashara za kimataifa.
Katika miaka ya karibuni kufuatia tishio kubwa kimataifa la ongezeko la bei za vyakula duniani na hasa katika nchi masikini, mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la uchafuzi wa hali ya hewa, uharibifu wa mazingira, changamoto za upatikanaji wa maji safi na salama duniani, kazi ya Chuo hicho imeongezeka sana.
Chuo hicho kimeichagua Tanzania kama nchi ya kufanya nayo kazi katika Afrika kukabiliana na changamoto hizo na kimemtambua Rais Kikwete kutokana na mchango wake mkubwa katika sekta ya kilimo katika miaka yote ya uongozi wake na mipango yake ya kuboresha kilimo katika Tanzania kama ASDP, Kilimo Kwanza na SAGCOT ambayo yote inasifiwa sana kimataifa.
Chuo hicho kina mahusiano ya karibu na Vyuo Vikuu vya Dar es Salaam, Sokoine cha Mzumbe - Morogoro na UDOM - Dodoma. Kati ya mwaka jana na mwaka huu, Chuo hicho kimetiliana saini Makubaliano ya Ushirikiano (MOU) na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine cha Mzumbe - Morogoro na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Mara nne kati ya Januari, mwaka jana, 2012 na Juni, mwaka huu, 2013, uongozi wa Chuo hicho ukiongozwa na Rais na Makamu Mkuu wa Chuo, Dkt. Alastair Summerlee na Makamu wa Rais wa Utafiti Dkt. Kevin Hall umetembelea Tanzania na kukutana na viongozi wa Serikali pamoja na wale wa Vyuo Vikuu vya Dar Es Salaam na Sokoine cha Mzumbe, Morogoro.
Mbali na ujumbe ambao unaongozana na Rais Kikwete, sherehe za kutunukiwa kwa Kiongozi Mkuu huyo wa Tanzania pia zimehudhuriwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe Bernard Membe, Jumuia ya Watanzania wanaoishi Canada pamoja na maofisa wa Ubalozi wa Tanzania nchini humo. Picha kadhaa za tukio hili>BOFYA HAPA
Your Ad Spot
Sep 21, 2013
Home
Unlabelled
RAIS KIKWETE ATUNUKIWA SHAHADA YA UZAMIVU CHUO KIKUU CHA GUELPH JIMBONI ONTARIO, CANADA
RAIS KIKWETE ATUNUKIWA SHAHADA YA UZAMIVU CHUO KIKUU CHA GUELPH JIMBONI ONTARIO, CANADA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Your Ad Spot
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269