Pinda akizindua Bwalo la Shule ya Sekondari ya Weruweru jana |
WERUWERU, Tanzania
WAZIRI MKUU Mizengo
Pinda amewataka Watanzania kuiga mfano wa shule ya Sekondari ya Weruweru ambao
wahitimu wake wa zamani (Alumnae) wameamua kuchangisha fedha na kukarabati
shule yao ya zamani.
Ametoa kauli hiyo
jana jioni wakati akizungumza na mamia ya wanajumuiya
waliohitimu katika shule hiyo (Alumnae), wanafunzi waliopo pamoja na wageni
mbalimbali waliohudhuria sherehe za Jubilei ya miaka 50 ya Shule ya Sekondari
ya Wasichana ya Weruweru.
Waziri Mkuu ambaye
alikuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo alisema: “Watanzania wengi tuna nafasi
za kuchangia shule zilizotusomesha. Tuige mfano wa wenzetu wa Weruweru,
tukutane na kusaidia shule tulizosoma,” alisema.
Baadhi wa
wanafunzi waliohitimu katika shule hiyo ni Dk. Asha-Rose Migiro, Dk. Mary Nagu,
Balozi Mwanaidi Maajar, Bi. Anna Kilango Malecela, Dk. Mwele Malecela, Dk.
Hellen Kijo-Bisimba, Hajat Amina Mrisho na wengine wengi ambao wameshika nafasi
mbalimbali za uongozi katika mashirika, taasisi na Serikalini.
Alisema yeye
alisoma sekondari ya Pugu kati ya mwaka 1965 na 1967 lakini kumekuwa na juhudi
mbalimbali za kuwakutanisha wahitimu wa shule hiyo ambazo hazijawahi
kufanikiwa. “Ninawataka mtembee kifua mbele kwa sababu shule yenu imeza yunda
zuri sana,” alisema huku akiwasifia wana Weruweru waliohitimu zamani kwa kuamua
kuja na wazo hilo jema la kukarabati shule yao ya zamani.
Mapema, akisoma
taarifa ya shule hiyo, Mwalimu Mkuu wa Weruweru, Bibi Rosalia Frimini alisema
shule hiyo iliyoanzishwa Oktoba 22, 1963 hivi sasa ina wanafunzi 570 wa kidato
cha tano na sita tu wanaosoma michepuo ya PCB, EGM,ECA, HGE, HGK na HKL.
Alisema shule
hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo uchakavu wa maabara, madarasa,
mabweni na mifumo ya umeme. Alisema shule hiyo ina upungufu wa watumishi
wakiwemo manesi, wapishi, mkutubi na walinzi.
“Shule pia
inakabiliwa na tatizo la usafiri.
Landrover 110 iliyopo shuleni ni ya tangu miaka ya 80 na matengenezo yamekuwa
makubwa, tunaomba utusaidie kutatua tatizo la usafiri... tunapata shida hasa
ikitokea watoto wanaumwa na wanatakiwa kupelekwa hospitali ya mkoa,” alisema.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dk. Maria Kamm
ambaye aliongoza shule hiyo kwa miaka 22 kuanzia mwaka 1970 hadi 1992, aliiomba
Serikali irudishe mfumo wa kidato cha kwanza hadi cha nne kwa shule kongwe
ambao ulifutwa na Serikali. Alisema katika kujenga maadili kwa watoto, inabidi
waanze tangu wanapoingia sekondari.
“Hawa wa kidato
cha tano na cha sita ni wa kupita tu.. umri wa kuumba binti ni kuanzia kidato
cha kwanza hadi cha nne. Tunahitaji kuumba mabinti wa Taifa hili kama ambavyo
tulikuwa tukifanya huko nyuma,” alisema.
Alisema Sera ya
Taifa ya Elimu ya Kujitegemea ilikuwa ndiyo siri kubwa ya kuwaumba wasichana
waliopitia shuleni hapo na kwamba ilileta usawa na kuondoa ubaguzi. “Sera hii
ilifanya watoto wote wawe sawa, iliondoa ubaguzi shuleni kwa sababu wanafunzi
wote walijifunza kazi na kujiamini. Na yote hii ni katika kujenga nidhamu kwa
watoto wetu,” alisema.
“Elimu ya
Kujitegemea siyo siasa kama wengi wanavyodhani, ni jadi ya mwafrika, ni jadi ya
mwanamke. Kujitegemea ndiyo msingi wa maendeleo ya Taifa lolote ulimwenguni,
tunaomba Serikali irudishe elimu ya kujitegemea shuleni ili tuwasaidie watoto
wetu.”
Naye Naibu Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asha-Rose
Migiro ambaye ni mhitimu wa shule hiyo alisema Jubilei ya miaka 50 ya Weruweru
ni sehemu ya kusherehekea ndoto iliyotimia na ndoto iliyokuwa kweli kwa
wanafunzi wengi waliosoma kwenye shule hiyo.
“Shule hii ni ya
pekee kwa sababu ilitoa fursa kwa mtoto wa kike pale ambapo hapakuwa na
fursa... ilikuwa ni mchanganyiko wa watoto wa viongozi, wafanyakazi na
wakulima”.
Akimnukuu Rais
wa zamani wa China, Mao tse Tung, aliyesema wananwake wanashikilia nusu ya
anga, Dk. Migiro alisema kutokanana usemi huo haiwezekani watu wanaoshikilia
nusu ya anga wakaendelea kubaki nyuma.
Alisema shule
hiyo imetoa wataalamu mbalimbali wakiwemo wanadiplomasia, wanasiasa, viongozi
mbalimbali wa mashirika, taasisi na serikali na pia imetoa rubani wa kwanza
mwanamke hapa nchini. PICHA NYINGI ZA MAADHIMISHO HAYO:BOFYA HAPA
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269