Breaking News

Your Ad Spot

Nov 12, 2013

CCM: ZIARA ZA KINANA MIKOANI ZIMEANZA KUZAA MATUNDA

JUMAA HII KUANZA ZIARA YA SIKU 22, RUVUMA NA MBEYA 
NA BASHIR NKOROMO
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema ziara ambazo zimekuwa zikifanywa na Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana, zimeanza kuzaa matunda hasa upande wa utatuzi wa kero zinazowakabili wananchi.

Hayo yamesemwa leo, Novemba 12, 2013, na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye wakati akitangazakuanza kwa ziara ya Kinana ya siku 22, katika mikoa ya mikoa ya Ruvuma na Mbeya itakayoanza, Novemba 15, 2013, ambayo ni mwendelezo wa ziara za kuimarisha chama, kukagua utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi  ya CCM ya mwaka 2010, kusikiliza kero za wananchi na kushirikiana nao kuzitafutia ufumbuzi.

Nape alisema miongoni mwa mafanikio yanayoonekana kutokea ni mwitikio ulionyeshwa na serikali katika kutekeleza maagizo yaliyotolewa kupitia ziara zilizopita za Kinana, na vikao vya Chama kuhusu kushughulikiwa kwa kero au hoja mbalimbali.

Alisema, baadhi ya kero ambazo zimeshuhudiwa zikichukuliwa hatua na serikali ni pamoja na kufufua viwanda nchini.

Nape alisema baada ya ziara kadhaa za Katibu Mkuu, uchambuzi na vikao kadhaa vya CCM, Chama kiligundua kuwa viwanda vingi vilivyo binafsishwa havifanyi kazi kama ilivyokusudiwa na vingine kufungwa kabisa na kugeuzwamagodauni.

Alisema pamoja na athari kubwa kwa uchumi wa nch, kufungwa na kutofanya vizuri kwa viwanda hivyo kumechangia sana tatizo la ajira kuwa kubwa, hivyo Chama kiliagiza serikali kufanya tathimini ya viwanda vyote vilivyo binafsishwa na hali yake kwasasa na vile visivyofanya kazi kama ilivyokusudiwa vichukuliwe na serikali na kutafuta njia sahihi ya kuvifufua upya.

Nape alisema, baada ya chama kuagiza kupitia ziara za Kinana na vikao vya Chama, serikali imechukua hatua kadhaa katika hili, ikiwemo kufanya tathimini na mapendekezo kadhaa yamewasilishwa na timu iliyoundwa na serikali kwa serikali kwa ajili ya kufanyia uamuzi na kuchukua hatua.

Alisema, CCM inatambua kwamba zipo hatua kadhaa ambazo imechukuliwa na serikali katika jitihada za kufufua viwanda vya kubangua korosho kama sehemu ya utatuzi wa tatizo la soko na zao la korosho na kwamba  na sasa serikali ipo katika hatua kadhaa za kushughulikia viwanda vingine nchini.

Nape alisema, kutokana na mwitikio huo, CCM inaipongeza serikali kwa hatua hizo muhimu za kutekeleza agizo la Chama, ingawa pamoja na pongezi hizo CCM imeitaka serikali ikamilishe kazi hiyo mapema iwezekanavyo ili nchi ifaidike na ufufuaji huo wa viwanda nchini.

Changamoto kwa wakulima wa pamba
Nape alisema, katika ziara ya Katibu Mkuu mikoa kadhaa ya kanda ya ziwa, alitumia muda mrefu kujifunza na kuzungumza na wakulima wa zao la pamba wa mikoa hiyo. Pamoja na tatizo kubwa la soko na bei ya pamba,
pamekuwa  na changamoto kubwa ya mfumo unaosimamia zao la pamba ikiwemo upatikanaji wa pembejeo.

Alisema, kufuatia ziara hiyo, hatua kadhaa zimeanza kuchukuliwa na serikali ikiwa ni pamoja na kuvutia uwekezaji kwenye viwanda vya kutengeneza nyuzi, nguo na kukamua mafuta ya pamba. Tulishuhudia ujenzi wa viwanda kadhaa mjini Shinyanga, vingi vikijengwa na wawekezaji kutoka China.

"Lakini wakati wa bunge la juzi, serikali imeamua kutoa ruzuku ya asilimia hamsini kwa mbegu bora za pamba ili kuwawezesha wakulima kumudu bei ya mbegu hizo na hivyo kuboresha zao la pamba nchini na maisha ya wakulima kuwa bora zaidi", alisema Nape

Alisema Katika suala hilo la mbegu bora na kilimo cha mkataba CCM inaitaka serikali na hasa wakuu wa wilaya na mkoa kuacha mara moja kutumia nguvu kuwalazimisha wakulima kulima kwa mkataba na kutumia mbegu bora badala yake wawaelimishe na kuwashawishi badala ya kutumia nguvu.

"Tunaipongeza serikali kwa kuanza kuchukua hatua za kutekeleza baadhi ya mapendekezo ya CCM ya namna ya kutatua matatizo yanayowakabili wakulima wa pamba nchini. Tunaitaka serikali kuongeza kasi ya utatuaji wa changamoto hizo ili wakulima wa pamba wafaidike na uchumi wa nchi kukua kwa kasi nzuri", alisema Nape.

Migogoro ya wakulima na wafugaji na hifadhi juu ya matumizi ya aridhi.
Kuhusu suala la migogoro ya wakulima na wafugaji na hifadhi juu ya matumizi ya ardhi, Nape alisema katika ziara mbalimbali za katibu mkuu kwenye mikoa kama ya Morogoro, Njombe, Simiyu, Mara alishuhudia migogoro mingi sana juu ya wakulima, wafugaji na hifadhi  mbalimbali nchini ambavyo vimegharimu sana maisha ya watu na mali zao na hata uchumi wa nchi.

Nape alisema baada ya Kinana kutoa maagizo, migogoro hiyo kushughulikiwa mapema ili kupata ufumbuzi wa kudumu, Chama kinalipongeza bunge na hasa wabunge wa CCM na serikali yake kwa uamuzi wa kuunda Kamati teule ya bunge kuchunguza na kutoa mapendekezo ya hatua kadhaa za kuchukuliwa katika kufikia suluhisho la kudumu kwa migogoro hiyo.

Nape alisema CCM inawaomba wananchi watoe ushirikiano wa kutosha kwa kamati teule ya bunge ili kazi hii ya kamati iwe na matokeo mazuri yatakayosaidia kumaliza tatizo hilo nchini.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages