Breaking News

Your Ad Spot

Dec 21, 2013

BASI LA ALLYS LAUA TISA, KUJERUHI 15, BUNDA NALO LAUA MMOJA

MWANZA, Tanzania
WATU kumi wamekufa, wanane kati yao papo hapo na wengine 16 kujeruhiwa katika ajali mbili tofauti zilizohusisha mabasi ya kampuni ya Bunda na Ally, mkoani Mwanza.

Ajali hizo zilitokea juzi katika barabara kuu ya Mwanza-Shinyanga katika maeneo ya Mitindo wilayani Misungwi na eneo la Buhongwa Dampo wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza.

Ajali mbaya zaidi iliyosababisha vilio kuugubika mji wa Usagara wilayani Misungwi, ilitokea majira ya saa 1:40 Buhongwa, ambapo Basi la Allys lenye namba za usajiri T.691 AGP liligonga Daladala (Toyota Hiace) na kusabaisha vifo vya watu tisa ambao kati yao, saba walikufa palepale.

Kamanda wa polisi mkoani Mwanza, Valentine Mulowola akithibitisha ajali hiyo, alisema basi hilo lililokuwa na hitilafu ya taa za mbele, lilikuwa likitoka Arusha kwenda jijini Mwanza wakati daladala hiyo ikitoka Buhongwa kwenda Usagara wilayani Misungwi.

Baadhi ya abiria waliokuwa katika ajali hiyo akiwemo Shija Francisco ambaye alijeruhiwa mkono wa kulia, basi hilo liliwagonga sehemu ya ubavu wa kulia na kusabisha Hiace hiyo ipinduke na kuviringika mara tatu nje ya barabara, wakati likijaribu kulipita roli moja lililokuwa mbele yake, kwenye kona.

“Ilikuwa ghafra mno tulipojikuta uso kwa uso na basi hilo ambalo halikuwa na taa, dereva akajaribu kulikwepa lakini hakufanikiwa, lilitugonga na kufanya gari letu lipinduke na kuviringika mara tatu.” Alieleza Franchisco mkazi wa Usagara huku akimlilia mkazi mwenzake Juma Basu (27) aliyekufa papo hapo.
 

Kwenye tukio hilo usiku huo, imeshuhudiwa miili ya watu hao ambayo baadhi ilikuwa imepondeka vibaya na kukatika viungo akiwemo mtoto wa miaka mine, Raphael Simon waliokufa pamoja na baba yake Saimon Paschal (35), wakazi wa Usagara.

Kamanda Mulowola aliwataja wengine waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni Eriakim Fredrick mkazi wa Igogo Mwanza, Stephen Mungisa (hatambulika makazi), Dismas Mpange (Usagara)na wanawake wengine wawili ndugu Shobo Lumecha na Gaudensia Lumecha, wakazi wa Geita.

“Abiria 15 walijeruhiwa katika ajali hiyo akiwemo dereva wa Hiace Anthony Maige (52) na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando lakin dereva wa Basi la allys Elias Charles alikimbia tunamsaka.” Alieleza Kamanda huyo na kubainisha kuwa daladala hiyo ilikuwa imejaza watu kupita kiasi.

Alisema katika ajali nyingine iliyotokea saa 11 jioni katika eneo la Mitindo Misungwi, Basi la Bunda T.234 BZK aina ya Scania likiendeshwa na Emmanuel Mashauri, liligonga mwendesha baiskeli Shilaga Thomas (20) na kusabaisha kifo chake palepale na kumjeruhi abiria wa baiskeli hiyo Machwenda Komanya.

Kamanda Mulowola alidai chanzo cha ajali hiyo ya basi la Bunda lililokuwa likitoka Dodoma kwenda Musoma, ni mwendo kasi na ametoa wito kwa madereva kuwa waangalifu na wazingatie sheria za usalama barabarani wanapotumia vyombo vya moto.

Kufuatia ajali hiyo, Mbunge wa jimbo la Misungwi Charle Kitwanga, ametuma salamu za rambirambi kwa ndugu jamaa na marafiki wa familia za marehemu hao hususan wakazi wa mji wa Usagara ambao umegubikwa vilio na simanzi kutokana na misiba ya watu wanne iliyosabaishwa na ajali hizo.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages