Breaking News

Your Ad Spot

Feb 19, 2014

MAMIA JIMBO LA KALENGA WASIMAMISHA SHUGULI ZAO KWA MUDA KUMSINDIKIZA MGOMBEA WA CCM KUREJESHA FOMU

Na Tumaini Msowoya, Iringa
MAMIA ya wakazi wa Jimbo la Kalenga mkoani Iringa, jana walisimamisha shughuli za uzalishaji kwa muda, kwa ajili ya kumsindikiza mgombea ubunge wa CCM, Godfrey Mgimwa alipokuwa akirejesha fomu ya kuomba kuteuliwa na Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC).

Mgimwa alirejesha fomu hiyo baada ya kushinda kura za maoni ndani ya CCM na baadaye kupata baraka za vikao vyote vya Chama.

Akizungumza baada ya kurejesha fomu, Mgimwa alisema ana imani kuwa CCM itashinda kwa kishindo katika uchaguzi huo kutokana na mshikamano uliopo.

Aliwataka wakazi wa Kalenga kutobabaishwa na kelele za vyama vya upinzani ambavyo haviwezi kuwaletea maendeleo kama vitapata nafasi ya kuingia madarakani.

Alisema jimbo hilo linapaswa kubaki mikononi mwa CCM ili yale yaliyoanza kufanywa tangu mwaka 2010, yamaliziwe.

    “Sikutarajia kuona watu wengi namna hii, nashukuru kwa kunisindikiza naamini safari ndiyo imeanza, utu huu mlionifanyia nitaulipa kwenu nawaomba sana mtulie wala msibabaishwe na vyama vya upinzani ambavyo haviwezi kutuletea maendeleo wana-Kalenga,” alisema.

Aliiponda CHADEMA kwa matumizi mabaya ya fedha kwa ajili ya kampeni ikiwemo kutumia magari ya kifahari na helkopta.

Alisema ufujaji huo hauwasaidii wananchi, bali unazidi kuwakandamiza kwani fedha hizo zingiweza kutumiwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo jimboni humo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Iringa, Delfina Mtavilalo, aliwataka wakazi hao kutokuwa wanyonge kama alivyotoa wito Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, badala yake wahakikishe wanajibu hoja kwa hekima na busara.

Godfrey Mgimwa - Mgombea Ubunge CCM Jimbo la Kalenga
    “Ili tuendelee kudumisha amani iliyopo tusiwe wanyonge, tujibu hoja kwa busara kama alivyotuasa Rais Kikwete, kwa kufanya hivyo, tutapata ushindi wa kishindo na tutajihakikishia usalama,” alisema.

Awali, Katibu wa CCM wa wilaya ya Iringa vijijini, Amina Imbo, alisema tayari maandalizi ya kampeni za ubunge kwenye jimbo hilo yamekamilika kinachosubiriwa ni kipenga cha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Aliwataka watu wote kuiunga mkoani CCM katika uchaguzi wa jimbo hilo kwa madai kuwa ndicho chama pekee chenye uwezo wa kuwasaidia wananchi wake.

    “Maandalizi ya kampeni yamekamilika, nawaombeni sana tuiunge mkono CCM ili ituletee maendeleo,” alisema Imbo.

Alisema CCM ni chama makini ambacho kimeweza kuwaletea maendeleo Watanzania kwa utekelezaji wake mzuri wa ilani ya Uchaguzi.

Alisema iwapo itaendelea kuongoza jimbo hilo, utekelezaji wa Ilani ambao ulikuwa ukiendelea utakamilika.
Naye msimamizi mkuu wa uchaguzi wa Jimbo la Kalenga, Pudensiana Kisaka, alimpongeza mgombea wa CCM kwa kuwahi kurejesha fomu.

Alisema baada ya masaa 24 kupita lisipotokea pingamizi, atatangazwa rasmi kuwa mgombea.

    “Hongereni kwa kufuata kanuni na sheria za uchaguzi, tumepokea fomu hii, tunaibandika hapo nje na baada ya masaa 24, kusipokuwa na pingamizi, atatangazwa rasmi kuwa mgombea,” alisema.

Alisitiza vyama vyote kuhakikisha vinafuata sheria na utaratibu wa uchaguzi ili kuepusha migongano isiyo ya lazima.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages