Breaking News

Your Ad Spot

Feb 4, 2014

TANZANIA MJUMBE WA BODI TENDAJI UNDP, UNFPA NA UNOPS

Na Mwandishi Maalum, New York
Tanzania kupitia Uwakilishi wake wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa, imeshiriki kikamilifu katika vikao vya kawaida  vya Bodi Tendaji ya  Mashirika na Mifuko inayosimamia Maendeleo ya Umoja wa Mataifa.

Tanzania  imeingia katika Ujumbe wa Bodi Tendaji ya UNDP (United Nations Development Program), UNFPA ( United Nations  Population Fund ) na UNOPS ( United Nations for Project Services) kwa kipindi cha mwaka 2014- 2016.

Licha ya kuwa mjumbe, Tanzania pia ni  Makamu   Rais  wa Bodi  nafasi inayoifanya Tanzania  kuziwakilisha  za Afrika  na  kupitia umakamu huo wa Rais, Tanzania inakuwa pia   mjumbe wa  Ofisi  ya mtedaji wa  Bodi(Bureau)  yenye jukumu la kuratibu na kusimamia  shughuli za vikao vya Bodi.

Bodi  Tendaji   ya UNDP, UNFPA na  UNOPS yenye  wajumbe 36  iliundwa kwa mujibu wa  Azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la  mwaka  1993.

Mgawanyo wa wajumbe   hao  ni kama  ifuatavyo,  wajumbe 8 hutoka   mataifa ya Afrika, wajumbe 7 hutoka mataifa ya  Asia na Pacific, wajumbe  5 ni  kutoka Amerika ya Kati na Visiwa vya  Karibiani,  wajumbe  4 hutoka  mataifa ya Ulaya  Mashariki na  wajumbe 12 kutoka Mataifa ya  Ulaya Magharibi na  Mataifa mengine.

Kwa  mujibu wa kanuni  zinazosimamia utendaji kazi wa Bodi, wajumbe wake  huhudumu kwa mzunguko wa  kupokeza .

Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania  ukiongozwa na  Kaimu Muwakilishi ,  Bi. Maura Mwingira,  na kwa  kushirikiana  na Maafisa wa Uwakilishi, umeshiriki kikamilifu   katika vikao hivyo  kwa kuogoza baadhi  ya   majadiliano na kuchangia mijadala.

Ujumbe wa Tanzania katika Vikao hivyo vilivyodimu kwa wiki moja,  ulitumia ushiriki wake  kusimamia  na kutetea   maslahi ya  Tanzania. Na katika  nafasi yake ya Makamu Rais   kutetea maslahi ya  Afrika.

Miongoni mwa  masuala yaliyotiliwa mkazo na  Tanzania katika  michango yake ni pamoja  na  kusisitiza   fursa na nafasi ya  nchi zinazoendelea  kuanisha, kuibua  na kumiliki  miradi ya maendeleo kwa kuzingatia vipaumbele  ambavyo nchi yenyewe imejiwekea.

Tanzania pia ilitambua mchango wa Mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa,  katika usimamizi na utekelezaji wa mipango ya maendeleo na miradi mbalimbai ikiwamo  ile inayosimamia  na kutetea fursa sawa za kijinsia  hususani kwa wanawake na watoto wa kike.

Yakiwamo pia masuala ya kilimo,  lishe, elimu na afya, vita dhidi ya umaskini na maendeleo shirikishi. 
 
Ikizungumza kwa  kwa niaba ya nchi za  Afrika,  Tanzania pamoja na masuala mengine, imetoa wito kwa  washirika wa maendeleo kuongeza michango yao katika Mfuko wa  Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNCDF).

Mfuko huu wa Maendeleo ( United Nations Capital Development Fund) unatoa mchango mkubwa  katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa nchi zinazoendelea na Tanzania ni mmoja wa wanufaika wa  mfuko huo.

Tanzania imebainisha katika  vikao hivyo kuwa licha ya  kazi  nzuri iniayofanywa  na UNCDF),  bajeti ya   Mfuko huo imeendelea kupungua  ikilinganishwa na mahitaji yaliyopo. Ni kwa sababu hiyo   imeomba wadau wa maendeleo hususani wale wenye uwezo na nia   kuangalia uwezekano wa kutunisha Bajeti ya mfuko kutoka bajeti ya sasa ya dola za kimarekani 16 milioni angalau ifikie dola milioni 25.

Bodi   Tendaji  ya  Mashirika na Mifuko ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa, (UNDP, UNFPA na UNOPS)  imekamilisha vikao vyake vya  kawaida  kwa  wajumbe wa Bodi kupitisha maazimio na mapendekezo mbalimbali.

Vikao vya Bodi, ambavyo vilifunguliwa na Bi. Helen Clark  Mkuu wa  Shirika la   Maendeleo la Umoja wa Mataifa, ( UNDP)  ambaye aliainisha  na  kuelezea  mafanikio na changamoto za utekelezaji wa  taasisi hizo kwa  mwaka uliopita.

Katika  ufunguzi wake,  Mkuu  huyo wa    UNDP   pamoja na kuelezea shughuli za  taasisi hizo  pia alielezea ushiriki wa UNDP katika utoaji wa misaada ya kibinadamu  katika nchi ambazo zimekubwa na  machafuko  kama vile Sudan ya Kusini, Syria na  Afrika ya Kati.

Aidha   alitoa taarifa ya  kuanza kwa  utekelezaji wa   Mpango  Mkakati  mpya wa UNDP utakaotekelezwa  kwa kipindi cha 2014-2017.

Kwa  mujibu wa  Bi.  Clark,  mpango  mkakati huo mpya unalenga pamoja na mambo mengine,  katika   kuratibu na kuboresha  utendaji kazi wa   taasisi  hiyo ,  pamoja na  kuleta uwiano, usimamizi na  matumizi bora  na yenye tija ya  raslimali zake ikiwamo raslimali watu.

Pamoja na   Mtendaji Mkuu wa UNDP kuanisha  shughuli zake,  Wakuu wa  UNFPA, UNOPS , UN- Women na  UNICEF nao  waliwasilisha taarifa za  Taasisi zao na kujadiliwa na wajumbe.

Wajumbe wa Bodi walipata fursa pia ya   kupitia na kujadili nafasi na mchango wa  Taasisi hizo   kuelekea ukingoni mwa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya  Milenia ( MDGs) na wajibu wa  taasisi hizo katika maandalizi ya malengo mapya ya maendeleo endelevu baada ya 2015 (SDGs).

Vile vile wajumbe wa Bodi walipokea taarifa za utendaji na vipaumbele vya  taasisi hizo,  ikiwa ni pamoja na  bajeti zao  na mapendekezo  yaliyotolewa na  wakaguzi wa  Bodi.
 Baadhi ya Maafisa wa Uwakilishi wa Kudumu, Bw. Noel Kaganda na Bi. Ellen Maduhu wakifuatilia moja  ya vikao vya Bodi ambapo Tanzania ilishiriki.
 Wajumbe wakifuatilia majadiliano

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages