Breaking News

Your Ad Spot

Mar 11, 2014

BAN KI MOON AWACHAGIZA WANAWAKE KUENDELEA KUTETEA FURSA SAWA


Katibu  Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban  Ki  Moon, akifungua mkutano wa 58 wa Kamisheni kuhusu Hali ya Wanawake ( CSW) Mkutano huu  wa wiki mbili  unafanyika hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa,  na unawakutanisha wanawake wa kada mbalimbali kutoka Serikali  Kuu na Asasa za Kiraia. Akifungua mkutano,  Katibu Mkuu, pamoja na mambo mengine amewataka wanawake kuendelea  kutetea fursa za kijinsia,  kupinga ubaguzi wa aina zote  na kuhakikisha kwamba sauti ya wanawake na watoto wa kike inaendele kusikika katika ajenda  mpya za maendeleo baada ya 2015. Kulia  kwake ni  Muwakilishi wa Kudumu wa Ufilipino katika Umoja wa Mataifa, Balozi Libran Cabactulan ambaye pia ni  Mwenyekiti wa  Mkutano .

Na  Mwandishi Maalum, NEW YORK
 Ikiwa  imebakia miezi michache  kufikia kilele  cha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya  Millennia ( MDGs), Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon amewataka wanawake kuendelea kupigania haki zao pamoja na za mtoto wa kike.
Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa,  ametoa wito huo  siku ya jumatatu,  mbele ya  mamia ya wanawake kutoka mataifa mbalimbali duniani kote ambao wapo  hapa Makao Makuu ya  Umoja wa Mataifa kuhudhuria mkutano wa 58 wa   Kamisheni kuhusu Hali ya Wanawake  ( CSW).
Tanzania inawakilishwa katika mkutano huu ambao ni wa wiki mbili na wajumbe kutoka pande zote za Muungano – Tanzania Bara na  Tanzania Visiwani.
“Mnajukumu kubwa mbele yenu” akasema Katibu Mkuu. Na  kuongeza, imebakia miezi michache kufikia hitimisho la  MDGs, na katika kipindi hiki lazima pia tubainishe ajenda za maendeleo baada ya 2015. Ninategemea  sana busara zenu na  kujituma kwenu katika kuwasilisha kwenye meza, sauti za wanawake na watoto wa kike”.
Ban Ki Moon, amewaeleza wanawake hao kutoka makundi mbalimbali ya jamii kuanzia Serikalini  hadi Asasai za kiraia kuwa, alikuwa pia anawategemea katika  kupigania na kutetea haki za binadamu  kwa wote.
“Hatutawezi  kufika mahali pakuwa na dunia yenye hadhi kwa  wote mpaka  pale tutakapotokomeza tofauti zote za kijinsia. Nipo pamoja nanyi” akabainisha  Katibu  Mkuu  huku akisisitiza kwamba   usawa wa kijinsia na uwezeshwaji wa wanawake ni  moja ya vipaumbele vyake.
Ajenda kuu itakayojadiliwa katika  mkutano huu wa 58 wa CSW ni mafanikio  na changamoto za utekelezaji wa  MDGs. Pamoja na   ajenda washiriki wa mkutano huu pia watakuwa na  mikutano ya pembezoni yenye maudhui tofauti lakini yote  ikilenga katika utekelezaji wa MDGs.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Katibu Mkuu  alianisha baadhi ya mafanikio ya utekelezaji wa MDGs, kama vile  ongezeko la watoto wanaokwenda shule hasa wa kike,  kupungua kwa vifo vya watoto wachanga muda mfupi baada ya kuzaliwa na kupugua kwa pengo la ajira kati ya wanawake na wanaume.
Hata hivyo akasema, katika eneo la ajira, bado wanawake ni wahanga wa malipo duni,  mazingira magumu ya kazi, huku wakikosa fursa  ya pensheni, bima ya afya na sheria za kazi zinazowalinda.
“Tumetoka mbali, lakini bado tunasafari ndefu tunahitaji vitendo  zaidi na sera zinazowajengea  uwezo Zaidi wanawake,  tunahitaji kuwaona wanawake wengi zaidi serikalini. Nafasi za wanawake  katika mabunge zimeongezeka katika  mataifa mbalimbali ingawa bado kuna tofauti kubwa za uwakilishi katika ngazi zote” akasisitiza.
Eneo ambalo amelitaja  kuwa bado  halijatekelezwa  vizuri   ni eneo la   usafi. Akasema  kila mwaka watoto 800.000 chini ya miaka mitano hupoteza maisha kwa ugonjwa wa kuharisha. Zaidi ya watu 2.5 bilioni wanakosa  huduma sahihi za usafi.
Kama hiyo haitoshi zaidi ya watu bilioni moja wanajisaidia matika maeneo ya wazi. “ tukiongeza  utoaji wa huduma za usafi , na kuacha kujisaidia maeneo ya  wazi. Hapana shaka tutapunguza sana magonjwa na uchafuzi wa mazingira na kuboresha zaidi usalama wa wanawake na watoto wa kike  ambao mara nyingi wamo katika hatari  kubakwa kwa sababu tu ya ukosefu wa vyoo safi na salama”.
 Ujumbe wa Tanzania  katika  Mkutano huu,  unawahusisha washiriki kutoka pande zote za Muungano, Tanzania Bara na Visiwani.  Pichani ni  Bi. Asha Ali Abdulla,  Katibu Mkuu,  Wizara ya  Uwezeshaji,  Maendeleo ya Jamii,  Vijana, Wanawake na Watoto, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Tuvako Manongi, Muwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,  Mhe. Jaji Imani Daud Aboud  kutoka Mahakama ya Rufaa ya  Tanzania, na Bi. Joyce Mlowe,  kutoka Wizara ya Katiba na Sheria wakifuatilia hotuba ya ufunguzi.
Baadhi ya Ujumbe wa Tanzania kutoka kulia   Bi.  Halima Abdulrahman Omar,  Mtaalamu wa  Masuala ya  Jinsia,  Wizara ya Uwezeshaji,  Maendeleo ya Jamii,  Vijana, Wanawake na Watoto- Zanzibar, Bi Mhaza Gharib Juma, Mkurugenzi wa Mipango,  Sera na Utafiti, Wizara ya  Uwezeshaji,  Maendeleo ya Jamii,  Vijana, Wanawake na Watoto- Zanzibar, na  Bi. Ellen Maduhu,  Afisa wa Uwakilishi wa Kudumu anayeshughulikia Kamati ya  Tatu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa inayohusika na  Masuala ya  Maendeleo ya Jamii na  Haki za Binadamu

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages