Breaking News

Your Ad Spot

Mar 19, 2014

TANZANIA INAFANYA VIZURI KATIKA UTEKELEZAJI WA MDG’s – WAZIRI SIMBA

Na Mwandishi Maalum, NEW YORK
Wakati Mkutano wa 58 wa Kamisheni  kuhusu Hali ya wanawake, ukiwa umeingia wiki yake ya pili,  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  imeeleza kwamba imejitahidi na imefanikiwa  kufikia  baadhi ya   Malengo ya Maendeleo ya Millenia  hata kabla ya  mwaka 2015.


Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto,  Mhe. Sophia Simba ( Mb) ameyasema hayo siku ya  jumatatu wakati Tanzania ilipopata fursa ya kuielezea jumuiya ya kimataifa uzoefu wake katika utekelezaji wa  MDGs na changamoto  ambazo bado inaendelea kukabilina nazo katika baadhi ya  malengo.


Mhe. Sophia Simba,  amesema Tanzania  imefanya vizuri katika  malengo nane kati ya  nane ingawa bado inakabiliwa na changamoto katika baadhi ya maeneo ambayo alielezea pia namna serikali inavyojipanga kukabiliana nayo.


Kwa wiki mbili sasa,   wawakilishi wa kutoka nchi mbalimbali duniani  zinazohudhuria mkutano huu hapa Umoja wa Mataifa,  wamekuwa  wakipashana habari na wakubadilishana  uzoefu  kuhusu masuala  yahusuyo haki za wanawake, za mtoto wa kike na ustawi wao na maendeleo yao.


Aidha wawakilishi  hao  wamekuwa  pia  wakiijadili mada kuu ya mkutano huu ambayo ni mafanikio na changamoto za utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya  Millennia,  ambapo kile nchi imekuwa ikitoka uzoefu wake.


Baadhi ya malengo  aliyoeleza kwamba Tanzania imefanya vizuri ni pamoja na lengo   namba mbili linalohusu fursa ya elimu ya msingi kwa  watoto wote na kwa kuzingatia uwioano wa kijinsia.


Aidha akabainisha pia kwamba   Tanzania  imefanya vizuri katika  lengo  la tatu kuhusu fursa sawa za  kijinsia na uwezeshwaji wa wanawake ambapo alitolea mfano ongezeko la wanawake katika vyombo vya utoaji  maamuzi kama vile  Bunge na Baraza la  Wawakilishi. Na  katika  sekta ya elimu ya sekondari ingawa  uwiano huo unapungua   kuelekea elimu ya juu.


Waziri wa  Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto akielezea zaidi mafanikio ya  utekelezaji wa MDGs, ameeleza pia kwamba kumekuwa na mafanikio ya kuridhisha katika upunguzaji wa  vifo vya watoto wachanga chini ya miaka mitano kwa pande zote mbili za  Muungano.


Hata hivyo licha ya mafanikio  ya kuridhisha katika eneo hilo, Waziri Simba anasema  bado watoto wanaendelea kupoteza maisha kwa maradhi yanazulikia kama vile  malaria na  kuharisha.


Kuhusu lengo namba tano   kuhusu   upunguzaji wa  vifo vya wanawake wajawazito,  Waziri anasema, eneo hilo bado linachangamoto nyingi na kwamba kasi yake ni ndogo.


Ametaja baadhi ya changamoto zinazolikabili eneo hili kuwa ni  uhaba wa  wataalamu, eneo ambalo anasema tayari serikali inalitafutia ufumbuzi,  ukosekanaji wa huduma za upasuaji wa dharura eneo ambalo amesema serikali pia inalifanyia kazi kwa kujaribu kuviwezesha vituo vya afya kuwavipatia vifaa na wataalam.


Kuhusu lengo la sita linalohusu  huduma za afya,  Tanzania, kwa mujibu wa Mhe, Waziri,  bado inachangamoto  nyingi katika  kukabiliana na maambukizi ya virusi vinavyosambabisha ugonjwa wa ukimwi, malaria na Kifua kikuu magonjwa ambayo yanagusa sehemu kubwa ya  jamii.


 Akasema  serikali imejitahadi sana katika kuyadhibiti magonjwa haya ,  kiasi kwamba kumekuwapo na   udhibiti wa maambukizo  miongoni mwa watu wazima.


Kuhusu lengo  namba saba linalohusiana na  Mazingigira endelevu,  pamoja na  huduma za maji safi na salama,  Waziri anasema,  bado kuna tatizo kubwa la  upatikanaji wa maji safi na salama hasa maeneo ya vijijini.


Mhe. Waziri Simba anabainisha kwamba   changamoto kubwa  kwa Tanzania iko katika utekelezaji wa lengo namba moja, linalohusu utokomezaji wa umaskini  uliokidhiri na  njaa.


Pamoja na kuelezea mafanikio na changamoto za utekelezaji wa  MDGs,  Waziri Simba,  amesema Tanzania  inaunga mkono  msimamo wapamoja wa   Umoja wa Afrika,  unaosisitiza kwamba  usawa wa jinsia na uwezeshwaji wa wanawake,  uwe lengo linalojitegemea  katika  Malengo Mapya ya Maendeleo Endelevu baada ya  2015 ( SDGs)

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages