Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu , Dkt. Albina Chuwa akiwasilisha hoja na mchango wa Afrika wakati wa majadiliano ya ajenda kuhusu Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) katika Mkutano wa 45 wa Kamisheni ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa unaoendelea hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.
Na Mwandishi Maalum, New York
Wajumbe wanaoiwakilisha Tanzania katika Mkutano wa 45 wa Kamisheni ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa na Mkutano wa wazi wa Tisa wa Kikosi Kazi kuhusu mapendekezo ya ajenda za malengo mpya ya maendeleo endelevu baada ya 2015 ( SDGs), wamendelea kutetea maslahi ya Tanzania kwa kushiriki na kuchangia majadiliano ya mada mbalimbali zinazohusiana na mikutano hiyo.
Akichangia katika mada iliyohusu Technolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) ambayo ilikuwa kati ya Mada kumi na moja, zilizojadiliwa katika siku ya pili ya Mkutano wa 45 wa Kamisheni ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dkt. Albina Chuwa amesema, Tanzania na Afrika kwa ujumla mwaka hadi mwaka imeendelea kupiga hatua katika eneo hilo licha ya changamoto mbalimbali.
Amezitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni kutokuwapo kwa uratibu kati ya wazalishaji wa takwimu za ICT na watumiaji na kati ya wazalishaji na watoaji wa data ambao ni chanzo muhimu cha taarifa.
Na kwa sababu hiyo anasema, tatizo hili kama halitarekebishwa linaweza kusababisha uchapishaji usio sahihi wa takwimu kuhusu ICT , jambo ambalo linaweza kupelekea utoaji wa maamuzi ya kisera wenye makosa.
“Uboreshaji na Uratibu kati ya wazalishaji, wauzaji na watumiaji wa takwimu, utaepusha kujirudia kwa makosa yakiwamo ya matumizi ya raslimali fedha na watu, raslimali ambazo ni haba katika Afrika. Akasema Mkurugenzi Mkuu ambaye pia ndiye aliyewasilisha hoja za Afrika katika mada hiyo ya ICT.
Aidha akasema kipengele cha takwimu za ICT kinapashwa kuingiza katika mikakati ya kitaifa kwaajili ya maendeleo ya takwimu na katika mipango ya kazi ya Kikanda.
Akielezea zaidi mchango wa ICT katika eneo zima la ukusanyaji wa Takwimu na umuhimu wake katika utekelezaji wa malengo mbalimbali ya maendeleo Barani Afrika, Dkt. Albina Chuwa anasema ukusanywaji wa takwimu katika ngazi za kitaifa lazima uimarishwe kwa kuweka utaratibu wa uratibu kati ya taasisi husika pamoja na Ofisi za Taifa za Takwimu.
Kuhusu uwezeshaji, Mkurugenzi Mkuu amesema, Afrika inahitaji kuimarisha uwezo wake wa kutafuta rasilimali ndani ya Afrika , ili hatimaye Afrika ijijengee uwezo wa kuboresha ukusanyaji, uchambuzi na usambazaji wa viashiria vya msingi vya ICT katika Afrika.
Aidha kutokana na ongezeko la matumizi ya ICT katika Afrika, Afrika imeutaka Umoja wa Mataifa, kupitia Kamisheni yake ya Takwimu, kurekebisha taarifa ilizonazo ili ziweze kutoka picha halisi ya maendeleo ya ukuaji wa ICT katika Afrika ikiwa ni pamoja na hatua ambazo zimefikiwa na Bara hilo katika eneo la ICT.
Katika hatua nyingine, Dkt. Albina Chuwa akichangia katika ajenda iliyohusu utekelezaji wa mfumo wa mazingira ya uhasibu wa kiuchumi ( SEEA) alipendekeza kwamba nchi za Afrika , Tanzania ikiwamo, zitahitaji kuwezeshwa kimafunzo na kiutaalamu ili zijenge uwezo wa kuutumia mfumo huo.
Akasema Tanzania ingependa kuona wataalamu walioandaa mfumo huo wanakuja na mkakati wa utoaji mafunzo na uwezeshaji kwa nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania na hasa ikizingatiwa umuhimu wa Takwimu katika utekelezaji wa malengo mbalimbali ya maendeleo baada ya 2015.
Hajjat Amina Mrisho Said, Kamishna wa Sensa, na Bw. Wilfred Mwingira, Meneja wa Shughuli za Takwimu wakifuatilia majadiliano ya Mkutano wa 45 wa Kamisheni ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa, Mkutano huu unawakutanisha wataalamu wa takwimu kutoka nchi 24 ambazo ni wajumbe wa Kamisheni pamoja na wawakilishi wa Taasisi za Kimataifa. Mkutano huu unafanyika katika kipindi ambacho tayari kuna majadiliano ya wazi yanayoendelea ya kikosi kazi kinachoandaa ajenda mpya za maendeleo endelevu baada ya 2015. Nafasi na umuhimu wa suala la Takwimu katika utekelezani wa malengo ya maendeleo ni jambo ambalo limekuwa likijitokeza mara kwa mara katika majadiliano hayo.
Mjumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Tisa wa majadiliano kuhusu ajenda mpya za maendeleo endelevu baada ya 2015, Dkt. Lorah Madete akijiandaa kutoa mchango wa Tanzania katika mkutano wa pamoja kati ya wajumbe wa kikosi kazi k uhusu ajenda mpya za SDGs baada ya 2015 na Kikundi cha Wataalam ambao wamekuwa wakijadiliana na kuangalia namna gani au ni kwa vipi malengo hayo mapya ya maendeleo endelevu baada ya 2015 yatafadhiliwa au kuwezeshwa kwa maana ya rasilimali fedha
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269