Breaking News

Your Ad Spot

Mar 23, 2014

WENYE ULEMAVU SHINYANGA WAOMBA KUPEWA BURE HUDUMA YA MAJI

Na Chibura Makorongo, Kahama
Chama cha watu wenye ulemavu katika wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga kimeiomba serikali kuiangalia upya sera ya maji hapa nchini ili ikiwezekana watu wenye ulemavu wapewe kipaumbele na kupatiwa huduma ya maji bure.

Ombi hilo limetolewa jana na mwenyekiti wa Chama cha walemavu katika wilaya ya Kahama Michael Mukanjiwa akizungumza kwenye kilele cha Maadhimisho ya wiki ya maji katika mkoa wa Shinyanga kilichofanyika katika kijiji cha Kagongwa,kata ya Kagongwa wilayani Kahama ambapo mgeni rasmi alikuwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga Ally Nassoro Rufunga.

Mukanjiwa alisema serikali haiwatendei haki watu wenye ulemavu kwa kuwatoza gharama za maji kama wanavyofanya watu wasio na ulemavu hivyo kuiomba iangalie namna ya kuwasaidia ikiwezekana wapatiwe huduma ya maji bure.

Mbali na kutaka watu wenye ulemavu wapatiwe huduma ya maji,Mukanjiwa pia aliitaka serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria wazazi na walezi wasiopeleka shule watoto wenye ulemavu  kwani kufanya vile ni kuwanyima haki watoto hao.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara katika kijiji cha Kagongwa wilayani Kahama,mkuu wa mkoa wa Shinyanga Ally Nassoro Rufunga alisema hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika mkoa huo kwa sasa ni asilimia 51.6 vijijini,Shinyanga mjini asilimia 58.5,Kahama mjini asilimia 63,Isaka asilimia 16 na Mhunze wilayani Kishapu asilimia 45.

Aidha Rufunga alisema takwimu zinaonesha kuwa hali ya huduma kwa wananchi wa manispaa na miji midogo bado siyo nzuri kutokana na mkoa kuwa nyuma ya malengo ya MKUKUTA 2 ya kuwapatia wananchi asilimia 95 ya maji ifikapo mwaka 2015.

Hata hivyo Rufunga alisema katika mwaka wa fedha 2013/2014 serikali imetenga jumla ya shilingi 3.61 bilioni katika kutekeleza mpango wa kusambaza huduma ya maji katika vijiji 100 kwa kushirikiana na mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Kahama na manispaa ya Shinyanga(KASHWASA).

“Katika upanuzi huu wa mtandao wa usambazaji maji kutoka mradi wa maji wa Ziwa Victoria ,ambao unalenga kupitia maeneo ya vijiji vya wilaya ya za Misungwi,Kwimba mkoani Mwanza na Shinyanga hadi Msalala,jumla ya vijiji 64 vyenye jumla ya watu 245,000, viatanufaika na mpango huu,kati ya vijiji hivyo 46 ni vya Shinyanga vijijini na 18 ni katika halmashauri ya Msalala”,aliongeza Rufunga.

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa mkoa aliwataka wananchi kutunza vyanzo vyote vya maji ikiwa ni pamoja na kupanda miti ili kutunza uoto wa asili ambao mara nyingi huathiriwa na ukame sambamba na kuwataka wakandarasi wote kukamilisha miradi yote inayoendelea kulingana na mikataba.

“Lakini pia niwakumbushe wateja wa maji safi mijini na vijijini kulipa ankara zenu kwa wakati ili mamlaka za maji na jumuia husika ziweze kutoa huduma zeney ufanisi na endelevu,na kwa upande wa halmashauri ziendelee kutoa elimu kwa wananchi ili watambue kuwa wana jukumu kubwa la kusimamia miradi ya maji kwa kushirikiana na kamati za maji”, alisema Rufunga.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages