Breaking News

Your Ad Spot

May 7, 2014

BALOZI MANONGI: TUNAWEZA KUJIFUNZA KUTOKA UHISPANIA

Na Mwandishi Maalum, NEW YORK
 Tanzania  inaweza kuongeza zaidi kasi yake ya ukuaji  wa uchumi na maendeleo ya wananchi wake,  kwa kujifunza  uzoefu wa nchi nyingine  marafiki kama vile  Uhispania.


Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi,  ameyasema hayo  siku ya jumanne, wakati alipokuwa akichangia  majadiliano  ya  mada kuhusu    “Kuendelea kwa Pamoja: misaada ya  maendeleo ( ODA),  biashara na uwekezaji”.


Muwasilishaji wa  mada hiyo alikuwa ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Uhispania, Bw. Jose Manuel Garcia- Margallo Y Marfil, alipokutana na  kubadilishana  mawazo na  Balozi wanaoziwakilisha nchi zao katika Umoja wa Mataifa.


Balozi Manongi amesema katika majadiliano hayo,  kwamba  Tanzania  kama  nchi  inaaamini kuna maeneo ambayo inaweza  kujifunza zaidi  na kutumia uzoefu wa  Hispania katika kusukuma mbele kasi ya  ukuaji wa uchumi wake na maendeleo.


 Akabainisha kuwa maeneo ambayo Tanzania kwa kushirikiana na Uhispania inaweza kujifunza na kubadilishana  uzoefu  ni  uwekezaji,  biashara na uvutiaji wa   misaada ya maendeleo.


“Tanzania inapenda kukushukuru kwa kuadaa mkutano huu na fursa hii ya kubadilisha mawazo kuhusu  dhana nzima ya  maendeleo ya  pamoja,  misaada ya maendeleo, biashara na uwekezaji”
Na  kuongeza  “Maeneo haya ni muhimu sana kwetu na nina amini tunaweza kubadilisha uzoefu na kujifunza namna  ambavyo nyinyi mumefanikiwa” akasema Balozi.


Na kuongeza kwamba  hata  katika majadiliano yanayoendelea hivi sasa kuhusu ajenda mpya za  maendeleo endelevu baada ya 2015,  maeneo yanayotiliwa mkazo  mkubwa  pamoja na mambo mengine , ni hayo ya  uwekezaji,  biashara na  misaada ya maendeleo.


“  Ni kwa kutumia fursa  zilizopo za uhusiano  baina ya nchi na nchi na ushirikiano katika ngani ya kimataifa, tunaweza  kuendelea   kwa pamoja”. Akaongeza Balozi Manongi.


Aidha   Mwakilishi huyo wa Tanzania  kama ilivyokuwa kwa wawakilishi wengine waliochangia majadiliano yao,  akatumia fursa hiyo kuishukuru Uhispania,  kwa uamuzi wake wa  kuanzisha  Mfuko wa Maendeleo Endelevu  kwa ubia na Shirika   la Maendeleo la Umoja wa Mataifa ( UNDP).


Akiwasilisha  mada hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Uhispania,  pamoja na  mambo mengine, aliwaeleza mabalozi kwamba,  nchi yake ambayo  ilikumbwa na mtikisiko mkubwa wa kuyumba kwa uchumi  angalau imeanza kutengemaa kwa kuchukua hatua kadhaa wa kadhaa, ingawa amekiri kwamba safari bado ni ndefu.


Baadhi ya mambo ambayo anasema serikali yake iliamua kuyafanyia kazi kwa kuyapa umuhimu ni pamoja na,   kufungua milango ya uwekezaji ndani na nje ya nchi  yake,  kukuza na kupanua biashara na  upatikanaji wa ajira kwa vijana wao.


Akabainisha kwamba   kama si kupanua wigo wa biashara, kuongeza kasi ya  uwekezaji ndani na nje,  Uhispania isingeweza kujifunia mafanikio   iliyonayo hivi sasa ikiwa ni pamoja na kuyatafsri mafanikio hayo  katika ushirikiano wa  kimaendeleo.


 Na kwa sababu hiyo akasema nchi  yake imekuwa mstari wa mbele katika  utoaji wa misaada ya maendeleo kwa nchi mbalimbali yenye uhusiano nao  ikiwa ni pamoja  Umoja wa Mataifa.


Akatoa mfano kwa kusema kati ya 2007 na 2012  nchi yake  imechangia zaidi ya dola za kimarekani 30 billion kwenye eneo la maendeleo, misaada ambayo ilitolewa kupitia uhusiano baina yake na  nchi nyingine  na katika  ngazi ya kimataifa. Ambapo Afrika  Kusingi mwa Jangwa la Sahara  ilipata jumla ya dola 4 billioni kama msaada wa maendeleo.


Kuhusu uwekezaji akasema nchi yake  inamtaji wa dola bilioni 640. Vile vile Uhispania ni nchi ya saba kama msafirishaji wa huduma katika nchi mbalimbali na ni ya 17 kama msafirishaji  mkubwa  bidhaa.


Akasema ni katika  kuamini kwake katika dhana nzima ya ushirikiano wa kimaendeleo ndio maana  nchi yake  licha ya kutoa misaada kwa nchi moja moja na katika ngazi ya Umoja wa Mataifa,  ndiyo maana  imeamua kwa kushirikiana na UNDP kuunda mfuko wa maendeleo endelevu kama ilivyofanya kwa  Malengo ya Maendeleo  Endelevu ya Millenia ( MDGs).


Akasisitiza kwamba nchi yake imeamua  kuunda mfuko huo kwa kile inachoamini kwamba  utakuwa daraja au kiungo kati ya  Malengo ya Maendeleo ya Millenia ambayo  yanaishia ukiongoni,  na malengo mapya ya maendeleo endelevu.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages