Dar
es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu Tanzania, (Chawata), Shida
Salum, yuko katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu
(ICU) katika Hospitali ya Ami, Masaki, Dar es Salaam akisumbuliwa na
maradhi ya saratani.
Shida ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na mama mzazi
wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe amelazwa tangu juzi. Alianza
kusumbuliwa na maradhi hayo mapema Agosti mwaka jana lakini hali yake
ilibadilika mapema mwaka huu akiwa mjini Dodoma akisubiri kuapishwa
pamoja na wajumbe wengine wa Bunge Maalumu la Katiba.
Akizungumza hospitalini hapo jana, Zitto alisema baada ya
hali ya mama yake kuwa mbaya alishindwa kuendelea kukaa Dodoma kusubiri
kuapishwa na alipelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH),
ambako aligundulika kuwa na saratani ya shingo ya kizazi na kupatiwa
tiba kwa mwezi mmoja kabla ya kupelekwa India kwa matibabu zaidi.
Alisema kabla ya kupelekwa hospitalini hapo, alikuwa
akiendelea kupata matibabu akiwa nyumbani, lakini hali yake ilibadilika
juzi.
Zitto alisema hali ya mama yake haijatengemaa tangu aanze
kusumbuliwa na maradhi hayo. Alisema kutokana na maradhi hayo ya mama
yake, ameshindwa kuhudhuria Bunge la Bajeti linaloendelea mjini Dodoma.
“Hali ya mama kwa kweli siyo nzuri, lakini nina imani itakuwa
nzuri na kuendelea na shughuli za ujenzi wa taifa kama zamani,” alisema
Kabwe.
Tangu kuanza kwa Bunge la Bajeti, Zitto alionekana Dodoma
mara moja tu, siku ilipowasilishwa Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG).
-Mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269