Breaking News

Your Ad Spot

May 2, 2014

MATUMIZI SALAMA YA NYUKILIA YASIZUIWE- TANZANIA

Na Mwandishi Maalum, New York
Tanzania  imeendelea kusisitiza kwamba,   nchi ambazo hazina mpango wa kuwa na silaha za nyukilia basi ziwe na haki ya kutumia  nyukilia kwa matumizi salama, na pia kupewa misaada ya kiufudi na uwezeshwaji katika eneo hilo.

Hayo yameelezwa na  Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,  Balozi Ramadhan Mwinyi wakati alipokuwa akitoa  maoni ya  Tanzania katika  mkutano wa  Kamati ya Maandalizi kwaajili ya mkutano  utakaofanyia tathmini   utekelezaji wa Mkataba wa kuzuia usambazaji holela wa silaha za  nyukilia ( NPT).

 Tanzania inashiriki kikamilifu katika Mkutano huo wa maandalizi ambao ni wa wiki mbili  na  unafanyika  Hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.  Wanaoshiriki  mkutano huu ni  nchi wanachama wa NPT pamoja na wawakilishi wa  mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs).

Dhumuni la mkutano huu wa maandalizi, ni kuaanda dondoo na mapendekezo    yatakayojadiliwa  katika mkutano wa tathmini kuhusu NPT. Mkutano huo unatarajiwa kufanyika  mwakani (2015).

Akizungumza kwa  niaba ya  Tanzania,  Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Ramadhan Mwinyi, amesema, kama  Tanzania na kama ilivyo kwa mataifa mengi ingepeda kuona  silaha za nyukilia zinatoweka katika  uso wa dunia. Lakini inaamini kwamba kila nchi Tanzania ikiwamo  inayo haki ya  kuwa na fursa ya kutumia nyukilia kwa masuala  salama.

Mwakilishi huyo wa Tanzania, amebainisha kwamba, hakuna asiyetambua  madhara ya silaha  za nyukilia kutokana matukioa kadhaa mbayo  yametokea huko nyuma yakiwamo ya   Hiroshima.

Akatahadharia kwamba kuna dalili  za wazi ya kujirudia kwa madhara hayo kwa kile alichosema  Jumuiya ya kimataifa  na hasa kwa nchi ambazo zimejilimbikizia silaha hizo hazitaki konyesha nia ya kweli ya kuachana nazo.

Akasema,  inasikitisha kwamba yale mataifa ambayo yana malimbikizo ya silaha hizo, yameendelea kushikilia misimamo yao na hata kufikia mahali  pa  kutetea uhalali wa kuwa na silaha hizo.

Tanzania ikaeleza kwamba,  silaha za nyukilia si tisho kubwa kwa nchi za Afrika, kwani   tishio  kubwa na ambalo linachangia katika  uvunjifu wa Amani na upotevu wa  maisha ya watu ni silaha ndogo ndogo na  nyepesi na  siyo  silaha za nyukilia.

Balozi Mwinyi amewahoji washiriki wa mkutano huo,   kwamba   ni  dunia ya aina gani  tunayotaka  kuwarithisha watoto wetu kwa kuendelea  kukumbatia silaha hizo za maangamizi.

 Akabainisha kwamba Tanzania  inaamini katika  Mkataba huo wa NPT kwa kile alichosema utekelezaji wake utaifanya dunia kuwa mahali salama. Na kwamba licha ya  kuridhia  mkataba huo, Tanzania pia   ni mwanachama wa mikataba mingine ya  kikanda  inayohusu uthibiti wa silaha za nyukilia. Hotuba Kamili ya Balozi Mwinyi>BOFYA HAPA

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages