Breaking News

Your Ad Spot

May 14, 2014

MZIGO MZITO ULIOMSHINDA KOFI ANNAN WAMSHINDA PIA LAKHDAR BRAHIMI

Na Mwandishi  Maalum,New York
Ban Ki Moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa  Mataifa,  kwa masikitiko makubwa ametangaza  kukubali kwake  kujiuzuru kwa mwakilishi maalum wa Umoja wa mataifa na Muungano wa nchi za Kiarabu, Lakhdar Brahimi aliyekuwa akisimamia mazungumzo ya kutafuta Amani nchini Syria.

Akitangaza mbele ya waandishi wa habari  kuhusu kujiuzulu kwa Bw. Brahimi ambaye pia alikuwapo kwenye mkutano huo, Katibu  Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  amesema mwanadiplomasia huyo  mzoefu ataachia wadhifa wake ifikapo  Mei 31.

Huku hali  ikiendelea kuwa ya sitofahamu na kutokuwapo kwa mwanga wowote wa maridhiano au kumalizwa kwa mgogoro nchini Syria, Ban Ki moon  anasema kujiuzuru kwa  Mwakilishi huyo maaulum ni  pigo kwa watu wa Syria na ni kielelezo  cha  kushindwa kwa Umoja wa Mataifa.

 Bw. Brahimi aliteuliwa  Agosti 17 mwaka 2012 akichukua nafasi ya   Katibu Mkuu  Mstaafu wa  Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan aliyeteuliwa  mwanzoni  kabisa mwa mgogoro huo na baada ya muda mfupi alitangaza kujiuzuru.

 Bw. Brahimi ameelezea masikitiko  ya kuondoka kwake huku akiiacha Syria katika hali mbaya. Lakini akaelezea matumaini yake kuwa, Katibu Mkuu, Ban Ki Moon, atafanya kila  ubinadamu  iwezekanavyo kufanya kazi na Baraza kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, pande zinazopigana  nchini Syria pamoja na  nchi jirani kumaliza mgogoro huo.

“ Ninahakika kuwa mgogoro huu utamalizika, lakini wadau wote wanatakiwa kulizingatia hili  je  ni vifo vingapi zaidi, ni uharibifu kiasi gani  utokee  kabla Syria haijawa Syria mpya” akasema Bw. Brahimi.

Naye  Katibu Mkuu  akasema, kwa miaka miwili Bw. Brahimi amejitahidi sana kumaliza ukatili na   vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria. “ Kwa kweli,  mwanadiplomasia huyo mwenye asili ya Algeria ( 80). Amepitia changamoto nyingi kuanzia  taifa lenyewe ya Syria,   eneo la Mashariki ya Kati na  Jumuiya ya Kimataifa kwa ujumla na  ambayo imegawanyika vibaya  juu ya namna ya  kuumaliza mgogoro wa Syria.

Takwimu  zinaonyesha kwamba tangu mgogoro wa Syria ulipoanza  mwezi  Marchi 2011 zaidi ya watu 100,000 wamepoteza maisha na zaidi ya 680,000 wakiwa ni majeruhi. Aidha zaidi ya watu  milioni 9.3 wanahitaji misaada ya kibinadamu  ndani ya  Syria,  ikiwa ni  pamoja na  watu milioni 6.5 ambao ni wakimbizi wa ndani. Vile vile mgogoro huo wa Syria  umesababisha kuwapo kwa wakimbizi zaidi ya  milioni 2.5 ambao wametafuta hifadhi katika nchi jirani.

Katika  kumuelezea zaidi Bw. Brahimi,  Katibu Mkuu amemtaja kama mmoja ya watu mashuhuri wanaotambuliwa duniani na mwana-diplomasia mwenye  uwezo mkubwa na mtetezi mkubwa wa Misingi na Katiba ya Umoja wa Mataifa.

Ban Ki moon akaongeza kuwa,  kwa Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa na ambalo ndilo limepewa dhamana ya kusimamia usalama na amani.  Pamoja  na nchi  zenye  ushawishi mkubwa kuhusu hali ya Syria kushindwa kumpatia ushirikiano wa kutosha Bw. Brahimi,  ni kushindwa kwetu sote.

Katibu Mkuu amesema ataendelea kutegemea uzoefu na ushauri wa Bw. Brahimi na kwamba kutoka na kazi nzuri aliyoifanya anastahili kupumzika.  Na  akazitaka pande zote zinazohusika na  mgogoro wa Syria  pamoja na mataifa yenye ushawishi kwenye mgogoro huo , kujiangalia upya na kutafakari nini kinachotakiwa kufanywa ili kuwarejeshea matumaini wananchi  wa Syria.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages