*Ataka viongozi wa dini wasichoke kuombea amani ya Taifa
*Mzindakaya agoma kumsamehe Mbunge wa Sumbawanga Mjini
WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali itaendelea kusimamia msimamo wake wa
kutokuwa na dini wala nchi kutokuwa na dini lakini itaendelea kuruhusu
watu wawe na dini zao.
Ametoa
kauli hiyo leo mchana (Jumapili, Mei 25, 2014) kwenye ibada ya kumuweka
wakfu Askofu Mteule Conrad Nguvumali wa Kanisa la Moravian Tanzania
Jimbo la Rukwa iliyofanyika kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, mjini
Sumbawanga.
Waziri
Mkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete ambaye
yuko nje ya nchi kikazi, alisema: “Leo tukiruhusu Serikali iwe na dini
na tayari katika dini zote kuna makundi madogo madogo, je wale wa upande
mwingine utawaacha wapi?”.
Pia
alitumia fursa hiyo kuwaasa viongozi wa dini nao pia waangalie
wasitumbikie kwenye mtego wa siasa na kuruhusu kanisa zima liwe la chama
fulani kwani miongoni mwa waumini wao wapo pia wapenzi wa vyama
vingine.
“Kama mtu binafsi, kiongozi wa dini anaweza kuwa mpenzi wa chama lakini kama Kanisa tusiruhu hali hiyo,” alionya.
Aliwaomba
viongozi wa dini waendelee kuliombea Taifa na hasa waombee amani ya
Taifa hili. “Ninawasishi viongozi wa dini msichoke kuombea amani ya
Taifa hili kwani amani ikipotea kama nchi hatuna mahali pa kukimbilia.
Katika tukio jingine,
Mbunge wa zamani wa jimbo la Kwela, Mzee Chrisant Mzindakaya amekataa
kumsamehe hadharani Mbunge wa sasa wa Sumbawanga Mjini, Bw. Aeshi Hilali
baada ya kupewa fursa ya kushikana mikono jukwaani na kusameheana.
Mzee
Mzindakaya alikataa kufanya hivyo akisema yeye ni mkristu lakini hakuwa
ameandaliwa kiroho kwa ajili ya tukio hilo. “Hapa ni shughuli ya kanisa
na si mkutano wa Chama. Lazima niwe mkweli leo sijajiandaa kwa jambo
hili… Mimi ni mtu mzima, nafsi ya msamaha inahitaji maandalizi, nahitaji
maandalizi ya kiroho,” alisema.
Hata
hivyo, alikiri kwamba amekubali msamaha alioombwa na Bw. Aeshi lakini
hawezi kuutoa katika shughuli ya Kanisa. “Nilishamwambia Mwenyekiti wa
CCM mkoa aitishe mkutano, wazee wa chama wawepo na sisi wawili tuwepo
kwa sababu nimetukanwa sana kama vile sijaifanyia jambo lolote nchi
hii,” alisisitiza.
“Niliwaeleza
pia waandae mikutano ya nje kule kwa wanachama ambako nilichafuliwa
sana. Nikisema nimemsamehe hapa nitakuwa mnafiki,” aliongeza.
Kwa
upande wake, Bw. Aeshi ambaye alipewa nafasi ya kwanza kuomba msamaha,
alisema anatambua kwamba bega haliwezi kukizidi kichwa na yeye kama
mtoto anamuomba msamaha Mzee Mzindakaya kwa yaliyopita ili waweze
kufanya kazi pamoja na kuleta maendeleo kwa wakazi wa jimbola Sumbawanga
Mjini.
“Natambua
kuwa mimi ni mtoto na siku zote mdogo atabaki kuwa mdogo lakini naomba
busara zake ili tushirikiane kuleta maendeleo ya mkoa wetu… yaliyopita
si ndwele tugange yajayo. Nimetamka maneno haya mbele ya viongozi wa
dini na mbele ya Mungu kwa kuwa najua yuko hapa,” alisema.
Mkuu wa
Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Stella Manyanya ndiye aliwaomba Mzee Mzindakaya
na Bw. Aeshi wapande jukwaani na kupeana mikono na kisha akawapa kila
mtu fursa ya kutoa neno.
Mhandisi
Manyanya alisema siku ya leo ni ya kipekee na akaona asipoteze fursa
hiyo bali aitumie kuwaomba viongozi hao ambao wamekuwa na uhasama wa
muda mrefu wayamalize kwa kupeana mikono hadharani.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, MEI 25, 2014
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269