Breaking News

Your Ad Spot

Jul 13, 2014

KAFULILA ABURUZWA MAHAKAMANI NA IPTL

NA FURAHA OMARY, UHURU
SAKATA la Kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania  (IPTL), kutuhumiwa kuchota fedha katika akaunti ya Escow, limechukua sura mpya baada ya kampuni hiyo sasa kutaka ikamue fidia ya sh. bilioni 310, Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi).

Hatua hiyo, inafuatia IPTL kwa kushirikiana na kampuni ya Pan African Power Solutions (T) Limited na Mtendaji Mkuu wa kampuni hizo, Harbinder Sign Seth, kufungua Kafulila (PICHANI), kesi Katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, kutokana na kashfa anazodaiwa kuzitoa juu yao kuchotwa fedha katika akaunti ya Escow isivyo halali.

Wakipitia wakili wao Augustine Kusalika, wamefungua kesi hiyo namba 131 ya mwaka huu, ambapo pamoja na mambo mengine wanaiomba mahakama katika hukumu yake kumuamuru Kafulila awalipe fidia ya kiasi hicho cha fedha cha sh. bilioni 310 kwa madai ya kutoa kashfa dhidi yao.

Kwa mujibu wa hati, wanadai kwamba kwa nyakati tofauti ndani na nje ya Bunge na kupitia mitandao ya kijamii, Kafulila ametoa maneno ya kashfa dhidi yao kwamba wamejipatia fedha katika akaunti ya Escow iliyoko Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwa njia zisizo halali.

Wadai hao kwa kupitia hati hiyo, wanadai kwamba IPTL iliingia mkataba na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) la kuisambazia umeme na imekuwa ikitekeleza majukumu yake kama walivyokubaliana.

Inadaiwa IPTL ilikuwa na mgogoro na kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited na TANESCO ambapo sh. bilioni 200 zilihifadhiwa katika akaunti ya Escow iliyofunguliwa BoT,  kusubiri kumalizika kwa mgogoro huo uliokuwa mahakama kuu.

Kwa kupitia hati hiyo inadaiwa kuwa baada ya kumalizika na kuhimitishwa kwa mgogoro huo,  mahakama ilitoa amri ya IPTL  kukusanya fedha hizo na BoT kutakiwa kuziachia.

Wadai hao wanadai kwamba katika hali ya kushangaza na bila ya uhalali wowote, Kafulika katika shughuli mbalimbali nje na ndani ya Bunge,  na kupitia mitandao ya kijamii ya Jamii Forum, Twitter na Facebok alimua kusambaza taarifa za kashfa kwa IPTL na Mkurugenzi Mtendaji wake.

Inadaiwa  Juni, 2014, mdaiwa alichapisha taarifa kwamba  IPTL na Seth   walijipatia fedha kutoka katika akaunti ya  Escrow isivyo halali, wakati si kweli.

Pia, Kafulila anadaiwa kusambaza taarifa za kwamba IPTL imehusika katika vitendo viovu vya kuchukua fedha katika akaunti hiyo.

Kwa kupitia hati hiyo, inadaiwa kwamba Kafulila amekuwa akitoa taarifa za kashfa, kwa kumtaja Seth kwa jina la singasinga, jambo ambalo si sawa na hivyo kumharibia sifa yake na kumsababishia uendeshaji wa biashara zake zinazotekelezwa na IPTL na Pan African kudorora.

Inadaiwa kutokana na taarifa zilizotolewa na Kafulila, ameisababishia jamii kuamini kuwa ni kweli IPTL imejipatia fedha hizo katika akaunti ya Escow bila uhalal na zimesababisha hasara au kupungua kwa hadhi ya kampuni hizo.

Hata hivyo, wadai hao wanadai Kafulila akiwa mbunge ana kinga ya kutochukulia hatia za kisheria kwa masuala ambayo ameyasema bungeni, lakini amekuwa akitoa taarifa za kashfa dhidi ya wadai ndani na nje ya shughuli za bunge.

Wadai hao wanadai taarifa zilizosambazwa na Kafulila mbali ya kuwashushia hadi pia kimesababisha hasara ya kibiashara na ameendelea kufanya hivyo licha ya kupewa  taarifa ya maneno na ya maandishi na kusababisha hadhi yao kushuka sio tu nchini bali hata kimataifa, hivyo kuwasabishia hasara kibiashara na  madhara ya kisaikolojia na usumbufu kwa menejimenti.

Wadai hao wanadai kitendo cha Kafulila kuelezea mambo yaliyotokea  katika mahakama za kisheria kuhusu maombi baina ya IPTL na  kampuni ya VIP Engineering and  Marketing Limited kimesabaisha si tu  kuingilia uhuru wa mahakama bali pia hasara kwa IPTL, wakati alikuwa akijua kilichoendelea mahakani.

Kwa kupitia hati hiyo, wanadai IPTL anatoa huduma ya kuisambazia umeme TANESCO, hivyo kutokana na taarifa za mdaiwa zimehatarisha uhusiano baina yake na shirika hilo hivyo kusababisha kudorora kwa uchumi na biashara yao.

Wadai hao wanaiomba Mahakama Kuu katika hukumu yake, imwamuru Kafulila awalipe sh. bilioni 210 kama fidia kutokana na kashfa hizo na hasara ya taswira ya biashara na hadhi yao.

Pia, aamriwe kuwalipa sh. bilioni 100 kama fidia ya madhara ya jumla kutokana na usumbufu walioupata kutokana na taarifa za kashfa zilizotolewa dhidi yao na awaombe radhi kutokana na taarifa hizo, gharama za kesi, riba kwa kiasi cha fedha yote wanayodai kwa kiwango cha  asilimia cha mahakama kutoka tarehe ya hukumu hadi tarehe ya mwisho wa malipo hayo. Aidha, wanaiomba mahakama kutoa amri nyingine itakazoona zinafaa.

Hivi karibuni Kafulila alinukuliwa na vyombo vya habari akitoa shutuma mbalimbali kuhusu kuchotwa sh. bilioni 200 katika akaunti hiyo kupitia kampuni ya IPTL na kuwataja baadhi ya watu wakiwemo mawaziri akiwahusisha na wizi huo.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages