Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mholanzi Mart Nooij amesema kikosi chake kipo tayari kwa ajili ya mchezo wa Jumapili dhidi ya Msumbiji hatua za awali Kombe la Mataifa ya Afika (AFCON).
Nooij ambaye amewahi kuifundisha Msumbiji amesema katika Mkutano na Waandishi wa Habari hoteli ya Coutyard, eneo la Sea View, Dar es Salaam kwamba wachezaji wake wote wapo fiti kwa mchezo huo.
Amesikitika kiungo Jonas Mkude ameshindwa kuhusika na mchezo wa Jumapili kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya goti, hata hivyo amesema ana matumaini m mchezaji huyo wa Simba anaweza kuwa fiti kwa ajili ya mchezo wa marudiano.
Ametaja kikosi alichoteua kwa ajili ya mchezo wa kesho, kuwa ni makipa Deo Munishi ‘Dida’ na Aishi Manula, mabeki Said Mourad, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Aggrey Morris, Kevin Yondan na Edward Charles, wakati viungo ni Erasto Nyoni, Shomary Kapombe, Shaaban Nditi, Simon Msuva, Himid Mao, Mwinyi Kazimoto, Khamis Mcha, Ramadhani Singano ‘Messi’, Haroun Chanongo, Amri Kiemba na washambuliaji Mrisho Ngassa, Thomas Ulimwengu, Mbwana Samatta na John Bocco,
Kwa upande wake, Nahodha wa Taifa Stars Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amesema kwamba anaomba Watanzania wajitokeze kwa wingi Uwanja wa taifa mjini Dar es Salaam kuisapoti timu yao.
“Tunashukuru hadi kufika hapa, ni matunda ya kupambana kwa juhudi na pia sapoti yenu, kwa hivyo tunaomba muendelee kuwa nasi Jumapili, watu waje kwa wingi wasapoti timu, ifanya vizuri,”amesema Cannavaro.
Aidha nahodha huyo wa taifa Stars amesema bado ana kumbukumbu za kipigo walichokipata dhidi ya Msumbiji mwaka 2007,wakati Nooij akiwa kocha mkuu wa Mambas, na kwa maana hiyo hivi sasa akiwa chini yake atafanya kila juhudi kwa faida ya Watanzania na yeye mwenyewe binafsi.
Stars itamenyana na Msumbiji Jumapili katika mchezo wa kwanza wa hatua ya mwisho wa mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya AFCON mwakani nchini Morocco, ambao kiingilio cha chini kitakuwa Sh. 7,000.
Stars ilifika hatua hii baada ya kuitoa Zimbabwe kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda 1-0 Dar es Salaam na kwenda kulazimisha sare ya 2-2 Harare.
Timu itakayofuzu hatua hii itaingia kwenye Kundi C ambalo lina timu za Zambia, Cerpe Verde na Niger zilizofuzu moja kwa moja hatua hiyo, kuwania tiketi ya Morocco mwakani.
Katika kuwania tiketi ya AFCON ya mwaka jana nchini Afrika Kusini, Tanzania ilitolewa na Msumbiji kwa penalti 5-4 baada ya sare ya jumla ya 2-2 Dar es Salaam na Maputo, Stars ikiwa chini ya kocha Mdenmark, Kim Poulsen.
Stars inaonekana kuwa na maandalizi mazuri safari hii chini Mholanzi, Nooi na uongozi mpya wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), chini ya Rais Jamal Malinzi.
Baada ya kuitoa Zimbabwe, wachezaji walipata mapumziko ya wiki moja, kabla ya kwenda Botswana kuweka kambi ya wiki, na waliporejea Mbeya kuweka kambi ya wiki moja na ushei.
Nchini Botswana, pamoja na mazoezi, pia Stars ilipata mechi tatu za kujipima nguvu, ambazo walifungwa mbili, moja dhidi ya timu ya taifa ya nchi hiyo, Botswana mabao 4-2 na nyingine dhidi ya timu ya jeshi la nchini humo, BDF walishinda moja 3-1 na kufungwa moja 2-1.
Tanzania imewahi kushiriki mara moja tu AFCON, mwaka 1980 nchini Nigeria ambako ilitolewa katika hatua ya makundi, ilipokuwa pamoja na wenyeji Nigeria, Ivory Coast na Misri, Kundi A. Ilifungwa 3-0 na Nigeria, 2-1 na Misri na kutoa sare ya 1-1 na Ivory Coast.
“Nafahamu sana mchezo utakuwa mgumu, hii ni timu yangu na timu yenu pia, naamini mshindi ni yule ambaye atacheza kitimu zaidi Jumapili,”amesema.
Kocha Mart Nooij kushoto akizungumza na Waandishi wa Habari leo, Kulia Msaidizi wake, Salum Mayanga |
Kutoka kulia Shomary Kapombe, Mbwana Samatta na Cannavaro |
Kutoka kulia Amri Kiemba, Thomas Ulimwengu na Mwinyi Kazimoto |
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269