Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuph Mwenda akizungumza, wakati wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Kinondoni walipokagua maendeleo ya ujenzi wa eneo la biashara mahsusi kwa machina na Mamalishe, Ubungo
Ujenzi wa kituo hicho cha biashara unaoendeleo
HABARI KAMILI
NA BASHIR NKOROMOManispaa ya Kinondoni, imetakiwa kuchukua thabiti kuhakikisha hakuna upendeleo utakaojitokeza wakati wa kugawa vizimba kwenye eneo la kisasa la biashara lililojengwa na Manispaa hiyo katika eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam.
Wametaka wakati wa kugawa vizimba kwenye eneo hilo la biashara lililopo nyuma ya jengo la Masiliano Tower, wapewe kipaumbele machinga na mamalishe ambao wamekuwa wakitaabika kwa muda mrefu kutokana na kukosa maeneo ya kufanyia biashara zao katika Manispaa hiyo.
Hayo yalisemwa jana, kwa nyakati tofauti na Wajumbewa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Kinondoni, walipotembelea eneo hilo la biashara ambalo ni pamoja na mradi wa Kituo kipya cha daladala kilichojengwa eneo hilo ambacho kinatarajiwa kuanza kazi mwishoni mwa mwezi huu.
Akijibu angalizo hilo Meya wa Manispaa ya Kinondoni Yusuph Mwenda, alisema, ugawaji huo utasimamiwa na yeye pamoja na wasaidizi wake wachake na kwamba hakuna upendeleo utakaopenyezwa wakati wa ugawaji huo.
"Ni kweli kabisa, eneo hilo tunalijenga mahsusi kabisa kwa ajili ya machinga na mamalishe wa manispaa hii, Wapo watu walishauri tuweke vitegauchumi mikubwa kama hoteli za kisasa lakini tulikataa, kwa sababu lengo kubwa na kusaidia walio wengi, kwa hiyo katika ugawaji vizimba hapa nitasimamia mwenyewe na Msaidizi wangu", alisema Mwenda.
Mwenda alisema, mradi wa ujenzi wa eneo hilo la biashara ambao umegharimu sh. bilioni 3, utawanufaisha watu wasiopungua 500 ambao watakuwa machinga na mamalishe.
Alisema, licha ya akwamba walengwa wakubwa ni machinga na mamalishe, watu wa kawaida watafikiriwa kupewa vizimba hivyo ingawa si kwa kipaumbele.
Mwenda alisema, mbali na mradi wa eneo la biashara na kituo cha kisasa cha mabasi, katika eneo hilo lenye ekari zaidi ya 15, Halmashauri inajenga pia eneo la huduma za burudani kama lilivyo eneo la Leaders' Club.
Alisema, pamoja na kujengwa eneo la burudani, pia Manispaa inajenga katika eneo hilo ukumbi mkubwa wa mikutano ambao utakuwa na uwezo wa kuchukua watu wengi kwa wakati mmoja ambao utakuwa tegemeo kubwa kwa shughuli mbalimbali zikiwemo za sherehe kama za harusi, kongamano na semina.
"Ukisikia mtu anasema CCM haiwapendi wamachinga, Mamalishe na wananchi wake kwa jumla ni muongo au ana ajenda yake ya siri. CCM inawapenda hao wote kwa vitendo ndiyo maana Halmashauri yetu ya Kinondoni kupitia ilani ya CCM imeamua kuwajengea kitu cha aina hii", alisema Mwenda. HABARI ZAIDI SOMA UHURU KESHO
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269