Breaking News

Your Ad Spot

Feb 18, 2015

MFUMO WA MTANDAO WA UPATIKANAJI TAARIFA ZA ARDHI ZANZIBAR WAZINDULIWA



1
Kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Zanzibar. Ali Khalid Mirza akiwasilisha Hotuba yake kwa mgeni rasmi Balozi wa Finland nchini Tanzania Bi Sinnika Antilla (Kulia) katika Uzinduzi wa Mfumo wa Mtandao wa Upatikanaji Taarifa za Ardhi Zanzibar unaojulikana kama (Zanzibar Land Information Service) (ZALIS) uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Ardhi iliyoko Forodhani Mjini Zanzibar.
2
Kulia ni mgeni rasmi wa Uzinduzi huo Balozi wa Finland nchini Tanzania Bi Sinnika Antilla akiwasilisha hotuba yake kwa katibu mkuu wa Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati (Kushoto) wakati wa uzinduzi huo.
3
Mgeni rasmi katika Uzinduzi huo Balozi Antilla akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Mfumo wa Mtandao wa Upatikanaji Taarifa za Ardhi Zanzibar.
4
Wa Tatu (Kulia) ni Meneja wa mradi wa ZALIS Nd. Moh’d Zahran akitoa maelezo ya kitaalamu kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi (Kulia) na Mgeni rasmi Balozi Antilla wa (Katikati).
5
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi akiwa katika Mkutano na Vyombo vya Habari mara baada ya kumalizika kwa uzinduzi huo.
…………………………………………………………………………….
(Picha na Miza Othman Maelezo-Zanzibar)
Balozi wa Finland nchini Tanzania Bi Sinnika Antilla amesema Zanzibar itaondokana na umasikini pindi itakua na utekelezaji juu ya Sera ya Utunzaji na Utumiaji mzuri wa Ardhi. Hayo ameyaeleza katika ukumbi wa Idara ya Ardhi iliyoko Forodhani Mjini Zanzibar wakati wa Uzinduzi wa Mfumo wa Mtandao wa Upatikanaji Taarifa za Ardhi Zanzibar unaojulikana kama (Zanzibar Land Information Service) (ZALIS). Amesema huo utakuwa na lengo la kushughulikia changamoto za Ardhi na kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi kwa kuweka sera nzuri za mazingira nchini Zanzibar. Aidha amefahamisha kuwa ZALIS ina lengo la kuhakikisha kuwa Ardhi inatumika vizuri pamoja na kuwepo uongozi ulio bora wa Ardhi nchini Zanzibar ili ije iwe ni urithi mzuri na wenye manufaa kwa vizazi vijavyo. Balozi Antilla ameipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuanzisha Mtandao wa Serikali (E-Government) uliorahisisha kufanikiwa kwa mradi huo pamoja na kuushukuru uongozi wa Idara ya Ardhi kwa ushirikiano wao katika kufanikisha mradi huo wenye malengo makubwa ya kijamii na kiuchumi kwa nchi hizo mbili. Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Zanzibar Nd. Ali Khalid Mirza amesema mradi wa ZALIS umepelekea kuwepo kwa matumizi mazuri ya maliasili hususan Ardhi na Misitu ambapo hadi sasa zaidi ya 40% ya Ardhi ya Zanzibar imefanyiwa usajili na asilimia zaidi ya 30% ya Ardhi hiyo inatumika kwa ajili ya kilimo jambo ambalo limeimarisha kilimo na kupelekea kukua kwa kiasi kikubwa uchumi wa wananchi wa Zanzibar. Amefahamisha kuwa mradi wa mtandao huo utasaidia kutunza kumbukumbu kwa njia iliyo salama ya mtandao na kuepusha kupotea kwa taarifa za wateja pamoja na kuwataka watendaji wa Idara hiyo kuwapa elimu wananchi wasio na uelewa juu ya matumizi na umuhimu wa mtandao huo. Ametanabahisha kuwa kuna changamoto nyingi zinazoikabili idara hiyo wakati wa usajili ikiwemo baadhi ya wananchi kutokuwa na vyeti vya kuzaliwa pamoja na baadhi ya Ardhi kuwa na migogoro ya mirathi hivyo kushindwa kuzifanyia usajili kwa wakati. Amesema usajili wa Ardhi ulianza mnamo mwaka 2013 ukianzia na Mji Mkongwe, Mikoroshoni, Miembeni na maeneo mengine mbalimbali Unguja na Pemba na hadi sasa bado unaendelea hivyo amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo ili kuzifanya Ardhi zao kuwa katika hali ya usalama kutokana na Dhulma na Wizi jambo ambalo kwa sasa limekithiri kwa kiasi kikubwa nchini.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages