0784482959, 0714047241 bashiryakub@ymail.com
Watu wengi wamenunua viwanja/nyumba lakini mali hizo zimeendelea
kubaki katika majina ya waliowauzia. Wapo ambao imepita hata miaka kumi
tangu wanunue maeneo lakini bado hawajabadili jina kuingia jina lake.
Zipo sababu nyingi zinazosababisha hali hiyo lakini moja ni watu
kutokujua umuhimu wa kubadili jina kwa haraka. Hapa sizungumzii tu
kubadili jina isipokuwa nazungumzia kubadili jina kwa haraka. Kupitia
makala haya napenda kuwaamsha watu kuhusu umuhimu mkubwa wa kubadili
jina kwa haraka iwapo umenunua nyumba/kiwanja kwa mtu. Ni muhimu sana
kufanya hivyo na itakuepusha na mambo mengi.
1.KAMA HUJABADILI JINA ALIYEKUUZIA BADO NDIYE MMILIKI.
Ikiwa kutatokea mgogoro wa umiliki wakati ambao umenunua
nyumba/kiwanja na hujabadili jina kwenda kwenye jina lako kuna hatari
kubwa zaidi ya kupoteza ulichonunua. Hii ni kutokana na ukweli kuwa
utapokuwa unatatuliwa mgogoro wa nani mmiliki swali la kwanza huwa ni
nani ambaye nyaraka ya umiliki ina jina lake.
Yule ambaye jina lake linaonekana kwenye hati au leseni ya
makazi ndiye hupewa kipaumbele na kwa mujibu wa sheria mwenye jina
kwenye hati au leseni ya makazi ndiye mmiliki. Wewe uliyenunua utakuwa
na mkataba na jina lako litakuwa kwenye mkataba lakini pamoja na kuwa na
jina kwenye mkataba bado huwezi kulinganisha mkataba na hati au leseni
ya makazi. Jina linalotokea kwenye hati au leseni ya makazi huwa na
nguvu zaidi kuliko lile la kwenye mkataba.
2.UMUHIMU WA KUBADILISHA JINA KWA HARAKA.
Upo umuhimu mkubwa mara tu baada ya manunuzi ya kiwanja/nyumba
kukimbilia hatua za kubadili jina. Ni vyema wakati unajipanga kununua
nyumba/kiwanja ukajipanga moja kwa moja na hatua za kuanza kubadili jina
mara baada ya kukamilika kwa mkataba wa manunuzi.
Mara nyingi tumekuwa tukiwashauri watu kuwa mkataba wa manunuzi
unapokuwa umekamilika leo basi hakikisha kesho unaanza taratibu za
kubadili jina( transfer). Ni utaratibu huu pekee utakaokufanya kujiamini
na ulichonunua. Pia unapotokea mgogoro kabla ya kubadili jina kuanzia
hapo unakuwa na nafasi ndogo ya kuweza kubadili jina kwakuwa kama
mgogoro utaenda mahakamani inaweza kutokea kuzuiwa kufanya hivyo mpaka
kesi itakapokwisha. Kesi yenyewe itaisha lini haijulikani . Kama ikiisha
baada ya miaka kumi, kumi na tano ina maana muda wote huo utakuwa una
mali ambayo ni kama si ya kwako.
3.UTARATIBU WA KUBADILI JINA( TRANSFER) BILA USUMBUFU.
( a ) Kwanza hakikisha una mkataba wako wa kununulia ambao una
muhuri wa wakili uliondaliwa kitaalam huku ukiwa na picha za wote
mnunuzi na muuzaji ikiwa ni pamoja na sahihi zenu wote. Kwa ufupi
hakikisha mkataba wako ni mzuri ambao una viwango vya kisheria ili
kuepuka kurudishwa rudishwa kwa ajili ya marekebisho au kukataliwa
kabisa uwapo mamlaka za ardhi.
( b ) Pili hakikisha una fomu namba 29 ambayo ni taarifa ya
kutoa umiliki .Fomu hii ni taarifa maalum ambayo aliyekuuzia anatoa
taarifa kwa kamishna wa ardhi kuwa anataka kutoa umiliki wake kwa wewe
mnunuzi. Atakuwa akizungumza kwa mtindo wa kiapo kuwa mimi fulani wa
sehemu fulani ninatarajia kutoa umiliki wangu wa ardhi wa eneo fulani
kwa fulani fulani.
Mwisho muuzaji ataweka sahihi yake na atakuwa ameichambua plot
anayotoa umiliki na anuani zake za makazi zitakuwa zimeoneshwa vyema.
Fomu hii hupatikana mamlaka za ardhi na kwenye ofisi za wanasheria.
( c ) Tatu ni kujaza fomu Namba 30 ambayo ni kudhibitisha nia ya
kutoa umiliki. Ile ya juu namba 29 inatoa umiliki wakati hii
inathibitisha nia ya kutoa au kuachia umiliki kwenda kwa mnunuzi. Hivyo
hii namba 30 ni msisitizo wa namba 29. Hii ni kutokana unyeti wa masuala
ya ardhi. Aidha taarifa nyingine katika fomu hii ni zilezile zilizo
katika fomu namba 29. Fomu hii nayo hujazwa na muuzaji tu na hupatikana
mamlaka za ardhi au ofisi za wanasheria.
( d )Nne baada ya fomu hizo hapo juu sasa inakuja fomu namba 35
ambayo ni fomu rasmi ya kuhamisha umiliki ( transfer of right of
occupancy). Katika fomu hii ndimo muuzaji anapotamka rasmi kuachia
umiliki na kuutoa kwa mnunuzi ikiwa ni pamoja na kuainisha bei ya mauzo.
Fomu hii itachambua nyumba/kiwanja ambacho kimetolewa umiliki na
hii itakuwa na majina yote mawili yaani muuzaji na mnunuzi. Pia itakuwa
na sahihi zao wote ikiwa ni pamoja na picha. Pia itakuwa na muhuri wa
wakili akiwa kama shahidi wa wote wawili muuzaji na mnunuzi. Fomu hii
nayo hupatikana mamlaka za ardhi na ofisi za wanasheria.
4.LAZIMA UWE NA RISITI ZA KODI.
Hiki ni kiambatanisho kingine kinachohitajika. Utatakiwa
kupeleka taarifa ya uthamini wa ardhi mamlaka ya mapato ambapo kupitia
taarifa hiyo watakupa hesabu za kodi utalipa na utapewa risiti na risiti
hiyo ndiyo utakayoambatanisha kwenye maombi yako.
5.USHAURI WA KITAALAM.
Hakikisha siku ya kununua nyumba/kiwanja inakuwa ndio siku ya
kuanza hatua za kufanya transfer. Kuchelewa kunapunguza hadhi yako ya
umiliki na kunakuweka karibu zaidi na mgogoro. Ni vigumu kumaliza
mgogoro kwa usalama pindi utakapotokea ukiwa haujafanya transfer.
Zingatia sana haya.
Your Ad Spot
Feb 20, 2015
Home
Unlabelled
UNATAKA KUFANYA TRANSFER (KUBADILI JINA) LA KIWANJA/NYUMBA,UTARATIBU WA HARAKA NI HUU.
UNATAKA KUFANYA TRANSFER (KUBADILI JINA) LA KIWANJA/NYUMBA,UTARATIBU WA HARAKA NI HUU.
Share This
About khamisimussa77@gmail.com
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Your Ad Spot
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269