Breaking News

Your Ad Spot

May 20, 2015

RIPOTI YA MKAGUZI NA MDHIBITI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI YAANIKA MADUDU

Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad
----------------------------------
RIPOTI ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, imetolewa na kuwasilishwa bungeni jana huku ikiendelea kuibua madudu katika matumizi ya fedha.
Moja ya madudu hayo yamebainika katika usimamizi wa rasilimali watu katika balozi za Tanzania, ambapo watumishi waliokoma kutumikia Taifa, wameendelea kugharimiwa katika maisha yao katika nchi hizo.
Moja ya gharama iliyotajwa na Profesa Assad wakati alipozungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Bunge ni Sh milioni 543 zilizotumika kulipa posho ya pango kwa watumishi hao baada ya kustaafu.
Katika Ripoti ya Ukaguzi ya Serikali Kuu, Profesa Assad alikwenda ndani zaidi na kutaja orodha ya balozi hizo ambazo watumishi wake wameendelea kulipwa ingawa wamestaafu, kwa madai kuwa hakukuwa na fedha za kugharimia urudishwaji wao nyumbani.
"Maofisa hawa wastaafu, walibakia wakifanya kazi bila kuwa na mikataba kwa kuwa Serikali ilikuwa na uhaba wa fedha, kwa ajili ya kulipia gharama ya kuwarudisha nyumbani baada ya kufikia umri wa kustaafu," ameeleza Profesa Assad katika ripoti yake.
*Balozi zenyewe
Ubalozi wa kwanza kuwa na maofisa wa aina hiyo ni wa Kinshasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambapo mtumishi alistaafu tangu Machi 28, 2014 na akalipwa posho ya Sh milioni 130.8, kutokana na kufanya kazi kwa miezi 10 zaidi.
Katika ubalozi huo huo, Profesa Assad alisema mtumishi huyo huyo alipewa Sh milioni 41.2 ya kodi ya pango kwa miezi kumi aliyofanya kazi akiwa amestaafu na hana mkataba na Serikali.
Ubalozi mwingine ni wa Maputo nchini Msumbiji, ambapo mtu alilipwa posho ya kufanya kazi akiwa amestaafu ya Sh milioni 204 kwa miezi 19 zaidi baada ya kustaafu.
"Kiwango hiki cha posho ni sawa na mara tatu ya gharama ya kumsafirisha yeye, mizigo na familia yake," ameeleza Profesa Assad katika taarifa hiyo.
Katika Ubalozi wa Ottawa nchini Canada, Profesa Assad alibainisha wazi kuwa ndiko angalau kulikokuwa na mstaafu ambaye alipewa mkataba wa miaka miwili, ingawa hakukuwa na maelezo ya sababu ya kuongezewa mkataba.
Mstaafu huyo wa Canada yeye alilipwa Sh milioni 137.5, huku katika Ubalozi wa Washington Marekani, mtumishi aliyefanya kazi ya miezi mitatu tu zaidi baada ya kustaafu, akiibuka na kitita cha Sh milioni 30.
Vyama vya siasa Wakati wanasiasa wakiwa vinara wa kushutumu watumishi wa Serikali na hata viongozi wengine kwa matumizi mabaya ya fedha za Serikali, Profesa Assad amebainisha kuwa vyama vinavyoongoza kwa kupokea ruzuku kubwa kutoka serikalini, baada ya ukaguzi vimepata hati yenye mashaka.
Vyama hivyo ni CCM, Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi huku chama kimojawapo kilichojiunga na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) cha NLD, kikiwa miongoni mwa vyama sita vilivyopata hati mbaya.
Akielezea sababu ya kutoa hati hizo kwa vyama hivyo, Profesa Assad alisema alibaini kuwa taarifa ya hesabu za vyama hivyo, zinatofautiana na misingi ya uhasibu na mfumo wa uandaaji wa taarifa za fedha.
Vyama vingine maarufu ambavyo hata havikupeleka taarifa zao za fedha kwa ajili ya kukaguliwa na CAG, ni pamoja na UDP na DP, huku chama cha ADC kinachotarajia kusimamisha mgombea urais Zanzibar, kikipata hati mbaya.
"Nashauri Msajili ya Vyama vya Siasa kwa kushirikiana na Mhasibu Mkuu wa Serikali, kuandaa mwongozo mzuri wa namna ya kuandaa taarifa za hesabu. Hii itawezesha kutoa taarifa za fedha kwa ubora unaotarajiwa," alieleza Profesa Assad.
Watumishi hewa Profesa Assad ameendelea kubainisha kuwa ndani ya Serikali kumeendelea kutolewa mishahara hewa, inayolipwa kwa watumishi waliostaafu, walioacha kazi na waliofukuzwa kazi.
"Nimebaini kuwepo kwa malipo ya shilingi milioni 141 katika taasisi saba...ambao hawakugundulika na kuondolewa katika orodha ya mishahara kwa wakati baada ya muda wao wa utumishi kufikia ukomo kinyume cha Sheria ya Umma kwa Wastaafu," amesema.
Malipo hayo yalikutwa katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Sh milioni 74, Sekretarieti ya Mkoa wa Shinyanga Sh milioni 24, Ofisi ya Waziri Mkuu Sh milioni 13 na Sekretarieti ya Mkoa wa Morogoro Sh milioni 10.
Mishahara mingine hewa imekutwa katika Sekretarieti ya Mkoa wa Tanga Sh milioni 10, Idara ya Huduma za Uhamiaji Sh milioni 6 na Wizara ya Mambo ya Ndani Sh milioni 1.9.CHANZO:HABARI LEO

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages