Breaking News

Your Ad Spot

May 19, 2015

WIVU WA MAPENZI WAPELEKEA MWANAUME KUMNYONGA MKEWE NA KUMNYOFOA JICHO

INAUMA sana! Katika kinachoonekana kama ni wivu wa kimapenzi, dada mmoja aliyefahamika kwa jina la Magdalena Lucas ( 23) ameuawa kikatili na ‘mumewe’ aliyetajwa kwa jina la Stephano Lucas (28) nyumbani kwao maeneo ya Mbezi Luis jijini Dar es Salaam wiki iliyopita baada ya kupigwa na kitu kizito kichwani na mwili wake kufungiwa chumbani kwa siku tatu.

Magdalena Lucas enzi za uhai wake.
Akizungumza na gazeti hili, mmoja wa majirani wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Benson Boaz alisema, imekuwa vigumu kwao kujua chanzo hasa cha kifo cha msichana huyo aliyekuwa mfanyabiashara ndogondogo, ingawa alikiri kuwa mara kwa mara wanandoa hao walikuwa wakizozana kutokana na wivu uliokithiri wa mwanaume.
MUME ALIKUWA NA WIVU

“Mwanaume ambaye alikuwa fundi ujenzi, alikuwa na wivu uliovuka kiwango kwa Magdalena, alikuwa akimuwekea mipaka kuzoeana hata na majirani, huyu kijana hakutaka na alipomuona mkewe anajichanganya na watu hakupendezwa kabisa,” alisema.

Aliongeza kuwa mara ya mwisho walimuona marehemu Ijumaa ya Mei 8 mwaka huu akiwa na mumewe lakini hawakuwaona tena na hawakuwa na shaka kwa kuwa mlango wao ulikuwa umefungwa kwa nje.
CHUMBA KUTOA HARUFU

“Jumapili jioni tukasikia chumba chao kikitoa harufu kali, ndipo tukapata hofu na kutoa taarifa polisi, walipofika na kuuvunja mlango, wakamkuta dada huyo ameuawa, akionekana kupigwa na kitu kizito kichwani maeneo ya usoni kiasi cha jicho lake kunyofoka. Hatujui kilichotokea maana hatukusikia kelele huenda kwa vile mvua nyingi ilikuwa inanyesha na mwanaume hajaonekana hadi leo,” alisema jirani huyo.
DADA HAMJUI SHEMEJIYE

Dada wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina moja la Asteria alisema kifo hicho ni pigo kubwa kwenye familia yao kwa kuwa tangu mdogo wake aanze kuishi na Stephano, hakuwahi kuwaonesha ndugu zake.
“Tangu mdogo wangu aanze kukaa na huyo shemeji,  sisi ndugu hatukuwahi kutuoneshwa tukamjua hata kwa sura, lakini majirani walijua kuwa ni mke wake, naumia sana, ni bora asingeamua kuishi naye kwani hakuwa na upendo wa kweli ndiyo maana kaweza kumfanyia ukatili wa aina hiyo,” alisema.
Marehemu ambaye hakubahatika kupata mtoto, alizikwa katika Makaburi ya Tandale kwa Ali Maua lakini ndugu na jamaa hawakupata nafasi ya kuuaga mwili wake kutokana na kuharibika.Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, ACP Camillius Wambura alisema habari hizo hazijamfikia lakini atafuatilia kwa kina tukio hilo ili hatua za kisheria ziweze kuchukua mkondo wake.
Credit: Gazeti la Uwazi

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages