Kaburi likiwa wazi baada ya kufukuliwa.
Jeshi
la Polisi Mkoa wa Pwani linawasaka watu wanaosadikiwa kuwa ni wezi
ambao wamebomoa kaburi la marehemu Napegwa Kishaluli (75), mkazi wa
Mailimoja Kibaha na kuutoa mwili wake kisha kuiba suti, viatu na soksi
alizokuwa amevalishwa.
Habari
za kipolisi kutoka mkoani Pwani zinasema kuwa, marehemu alizikwa
Aprili 20, mwaka huu lakini siku saba baadaye watu wasiojulikana
walikwenda kaburuni na kulivunja kisha kulitoa jeneza wakidhani kulikuwa
na mali kaburini kisha kumvua nguo zote marehemu wakidhani alikuwa na
dhahabu.
Tukio
hilo lilitokea Aprili 24, mwaka huu katika Kata ya Tangini jirani na
Soko la Loliondo, habari zinasema baada ya mazishi kaburi hilo
liliwekewa mlinzi kwa muda wa wiki moja kutokana na uvumi kuenea kuwa
marehemu alizikwa na vitu vya thamani ukiwemo mkufu wa dhahabu.
Watu
wa karibu na familia ya marehemu wamethibitisha kutokea kwa tukio hilo
na wakasema kuwa baada ya mazishi ulikuwepo uvumi kwamba marehemu
alizikwa na vitu vya thamani kama vile pete na mkufu wa dhahabu, kitu
ambacho siyo kweli.
Akizungumza
na mwandishi wetu, ndugu wa marehemu ambaye hakutaka jina lake
kuandikwa gazetini kwa kuwa siyo msemaji wa familia, alisema baada
kuzika walilazimika kuajiri mtu wa kulinda kaburi hilo la ndugu yao kwa
wiki moja lakini siku moja baada ya mkataba kumalizika kaburi hilo
lilivunjwa.
“Tuliweka
mlinzi alinde kaburi hilo kwa wiki moja tukiamini litakuwa limekauka
kwa sababu lilitengenezwa kwa zege. Tuliamini watu wenye nia mbaya
watashindwa kulivunja jambo ambalo limekuwa kinyume kwa vile baada ya
muda huo kumalizika kaburi lilibomolewa ‘ubavuni’ na watu wasiojulikana
ambao waliamini ndani ya kaburi kulikuwa na mali nyingi,” alisema.
Aliongeza
kuwa baada ya kuvunja kaburi hilo wahalifu hao walilitoa jeneza nje,
wakalifungua kisha kupekua ndani kwa kuligeuza na kuliweka tofauti na
lilivyokuwa awali.Baada ya kuona hakukuwa na mali zozote waliamua kumvua
marehemu nguo zote, viatu na soksi alizovalishwa wakaondoka nazo.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Pwani, ACP Jafari Mohamedi juzi alithibitisha kutokea
kwa tukio hilo na akaongeza kwamba watu hao hawajakamatwa.“Bado tupo
kwenye uchunguzi na watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria,”
alisema.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269