Zana za kivita zilizopatikana baada ya kuuawa kwa wavamizi wa Al Shabaab
Shambulizi hili linawadia siku ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu kutokea shambulizi la Mpeketoni Lamu
Inspekta Jenerali wa Polisi alitangaza hali ya tahadhari baada ya kupokea habari Al shabaab wanapanga shambulizi wakati wa Ramadhan
Wapiganaji 13 wa Alshabaab wameuawa baada yao kushambulia kituo cha kijeshi cha Baure kilichoko eneo la Lamu katika pwani ya Kenya.
Msemaji wa jeshi la Kenya kanali David Obonyo ameithibitishia BBC kuwa wapiganaji hao walivamia kambi hiyo ya kijeshi mwendo wa 5:45 alfajiri ya leo lakini wakazidiwa nguvu kabla hawajaingia ndani ya kambi hiyo.
Kanali Obonyo alisema kuwa wawili kati ya wale waliouawa ni wenye asili ya kizungu.
Hakuna aliyepatikana hai japo
washambuliaji wengine wa Al Shabaab wanasemekana kutorokea katika msitu
mkubwa wa Bony ambapo wanajeshi wanawafwata.
Kanali Obonyo amesema kuwa wamepata zana kali na za kisasa za kivita.
Aidha amethibitisha kuwa wanajeshi wawili wa Kenya waliokuwa wakishika doria waliuawa katika shambulizi hilo.
Shambulizi hilo limetokea huku wakenya
wakiadhimisha mwaka mmoja tangu wapiganaji wa Al shabaab
waliposhambulia mji wa mpeketoni na kuua zaidi ya watu sitini katika
eneo hilohilo la Lamu.
Hapo jana, Serikali ya Kenya
ilitangaza kuanzisha operesheni kukabili tishio la kigaidi wakati wa
mfungo wa kiislamu wa Ramadhan.
Inspekta Jenerali wa Polisi nchini
Kenya, Joseph Boinet alisesema japo sio wajibu wa Kenya kushika doria na
kulinda usalama ndani ya kambi za wakimbizi zilizoko nchini Kenya,
''imewalazimu kuchukua hatua kali
kudhibiti utovu wa usalama kufuatia habari za kijasusi zilizodai kuwa
wanamgambo wa Al Shabaab wanatumia kambi hiyo ya wakimbizi kubwa zaidi
nchini Kenya kupanga mashambulizi ya kigaidi nchini Kenya''. Alisema
Boinet.
Boinet alisema hali ya usalama
imeimarishwa vilivyo kufuatia vyanzo vinayoaminika kudai kuwa kundi hilo
la Jihad linapanga kutekeleza mashambulizi wakati wa mfungo wa dini ya
kiislamu wa Ramadhan.
''Wanataka kuvuruga amani wakati wa
kipindi hiki cha dua takakatifu kwa wakenya wasio na hatia kwa
kutekeleza mashambulizi na mauaji, lakini tumechukua tayadhari kubwa.''
''Tumeimarisha usalama katika taasisi
za umma ,vyombo vya usalama, taasisi za mafunzo, makanisa, masoko na
maduka makubwa hasa mjini Nairobi, Mombasa and Kaskazini kwa Kenya''
'' Inaumiza sana kuwa wakimbizi ambao
tumewapokea katika maeneo ya Kaskazini mwa Kenya wamegeuka na kuanza
kushiriki uhalifu na hata kuumiza wenyeji wao.''
Inspekta huyo mkuu alisema kuwa tahadhari hiyo inafuatia vyanzo kamilifu vya kijasusi.
''Sio wajibu wetu kulinda usalama
ndani ya kambi lakini sasa imetubidi kuwa waangalifu zaidi kujua nani
anaingia ndani ya kambi hizo na ni nani anayetoka humo'' aliongeza
Boinnet.
Amesema kuwa serikali ya Kenya
imeimarisha uwezo wake wa kupambana na shambulizi lolote la kigaidi
ikiwemo kudukua mawasiliano yao kupitia njia ya mitandao ya kijamii ya
Facebook na WhatsApp.
Serikali ya Kenya imekuwa ikilaumu kuwepo kwa wakimbizi wengi wenye asili ya Somalia ndani ya mipaka yake kwa utovu wa usalama
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269