Mratibu Mkazi Mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN) na
Mwakilishili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini,
Alvaro Rodriguez ambaye alikua mgeni rasmi katika Kongamano la
upatikanaji wa fedha za ndani za maendeleo akitoa hotuba yake kwa
washiriki kutoka Halmashauri za wilaya nchini lililofanyika jijini
Arusha.
Mkuu wa Mfuko wa Umoja wa mataifa wa Ukuzaji Mitaji
(UNCDF) nchini na Meneja wa LFI duniani, Peter Malika akizungumza wakati
Kongamano hilo.
Mkurugenzi wa Huduma(Tamisemi), Denis Bandisa akizungumza
wakati Kongamano ambalo pamoja na mambo mengine alizitaka halmashauri
nchini kubuni vyanzo vya ndani vya mapato badala ya kutegemea wafadhili.
Washiriki kutoka maeneo mbalimbali nchini na nje ya nchi wakifatilia kwa makini mada katika Kongamano hilo.
Washiriki kutoka maeneo mbalimbali nchini na nje ya nchi
wakiwa katika picha ya pamoja, Kongamano hilo limefanyika katika hoteli
ya Mount Meru jijini Arusha.
Na Mwandishi wetu, Arusha
MFUKO wa Umoja wa Mataifa wa Ukuzaji Mitaji (UNCDF) kwa
kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (TAMISEMI), umeitisha kongamano la siku mbili la upatikanaji wa
fedha za ndani kwa maendeleo.
Kongamano hilo linahusisha wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa nchini Tanzania na linashirikisha watu 110.
Pamoja na wakurugenzi hao, wapo na wawakilishi kutoka
Serikali Kuu na wawakilishi walioteuliwa kutoka serikali za mitaa za
Uganda, Senegal na Benin.
Kwa mujibu wa taarifa ya UNCDF, nia ya kongamano hilo ni
kuonesha mafanikio ya mfumo wa ukusanyaji wa fedha za ndani kuwezesha
ujenzi wa miundombinu ya kiuchumi ya kibiashara katika nchi za Tanzania
na Uganda.
Taarifa hiyo imesema kwamba baada ya kujifunza mafanikio hayo
washiriki watajadiliana na kujipanga kwa ajili ya utekelezaji wa mfumo
huo katika nchi zao wanaokotoka ili kupiga hatua mbele katika
uendelezaji wa miradi bila kutegemea fedha za nje.
Akizungumza wakati wa ufunguzi Katibu Mkuu Tamisemi, Jumanne
Sagini alisifu kazi inayofanywa na programu ya uwezeshaji wa fedha za
ndani kwa maendeleo ( Local Finance Initiative- LFI) chini ya
sekretarieti ya UNCDF kwa ubunifu wake unaowezesha kupatikana kwa
mitaji ya kuwekeza katika miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na serikali
za mitaa.
Aidha alielezea dhamira ya serikali ya kutumia mfumo huo
ulioasisiwa na UNCDF kwa kuufanya uwe wa kitaasisi zaidi ili kuweza
kusaidia kutekeleza mipango ya maendeleo na uwekezaji ya serikali za
mitaa.
Akizungumzia umuhimu wa kongamano hilo, Mgeni rasmi, Mratibu
wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Alvaro Rodriguez, aliipongeza
serikali ya Tanzania kwa kufuata mfumo wa utafutaji wa fedha za ndani
kwa ajili ya kukuza uwekezaji katika miundombinu ya kibiashara inayoleta
mabadiliko kwa umma.
Rodriguez alisema katika hotuba yake kwamba kwa kuwezesha
mfumo wa UNCDF LFI kwenye serikali za mitaa ndio jibu la uhakika la
uwekezaji wenye mafanikio endelevu kwa taifa zima.
Aidha alisema mpango huo wa LFI ambao umekuwepo nchini kwa
miaka mitatu na kuwezesha kuleta mabadiliko katika jamii, unafaa
kumilikiwa na jamii ili kuwezesha mafanikio ya juu katika uwekezaji.
Mratibu huyo alisema kwamba Umoja wa Mataifa kupitia UNCDF
utaendelea kufanyakazi na serikali ya Tanzania,kwa kuwa wanaamini kwamba
vita dhidi ya umaskini itafanikiwa kwa kuhamisha mitaji na kuipeleka
katika ngazi za chini kwa maendeleo ya wananchi.
Kongamano hilo ambalo ni mwendelezo wa uwezeshaji na
kubadilishana uzoefu na elimu kwa lengo la kuwezesha miradi ya umma na
binafsi inayochagiza maendeleo kujengwa; katika siku ya kwanza ya
kongamano hilo washiriki wataoneshwa miradi iliyotekelezwa manispaa ya
Busia Uganda na Kibaha nchini Tanzania.
Manispaa ya Busia imejenga kituo cha malori, ushuru wa
forodha na maeneo ya kufanyia biashara, wakati Kibaha wamejenga kituo
cha kisasa cha mabasi na soko.
Timu ya wataalamu wa UNCDF watawafundisha washiriki kwa siku
2 kuhusu miradi ya maendeleo, awamu za malipo ya fedha na mikakati ya
kupata fedha na malipo na mbinu za kupunguza hatari za kibiashara.
Akisisitiza umuhimu wa kongamano hilo Mkuu wa UNCDF nchini na
Meneja wa LFI duniani Peter Malika alisema kwamba kongamano hilo
linatoa nafasi kwa watumishi wa serikali za mitaa na wengine kujifunza
namna mpya ya kupata mitaji kwa kutumia vyanzo vya nyumbani ili
kufadhili miradi ya miundombinu ya kiuchumi inayohitajika kwa ajili ya
kutoa fursa za ujasiriamali , biashara, uwezeshaji, ajira, kuboresha
maisha ya watu, ukusanyaji kodi na utoaji huduma.
Kongamano hilo la siku 2 ni miongoni mwa juhudi kadha za
UNCDF za kuwezesha serikali za mitaa kufikia maendeleo endelevu na
kuleta athari chanya kwa jamii ili kuondoa umaskini.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269