Ofisa
Uhusiano Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Bi Etty Kusiluka (kushoto),
akizungumza na mwananchi Juma Nyingi aliyetembelea banda la MSD katika
maonyesho hayo.
Ofisa
Uhusiano wa MSD, Benjamin Massangya (kulia), akimueleza mkazi wa Utete
kutoka wilaya ya Rufiji, Omary Abdallah shughuli mbalimbali zinazofanywa
na MSD baada ya kutembelea banda la MSD leo mchana.
Vitanda vya hospitali vilivyopo katika banda la MSD.
Na Dotto Mwaibale
IDADI ya vidonge vinavyosambazwa na Bohari ya Dawa
(MSD) ambavyo vimewekewa nembo ya Serikali (GOT)
imefikia 42 hadi sasa huku wazabuni wanaoshinda tenda kwaajili ya dawa
na vifaa tiba vya MSD wakiendelea kuelekezwa kukidhi utaratibu huo wa kuweka
nembo ya GOT ili kuepusha uchepushaji wa dawa za serikali.
Bohari ya Dawa ilianza utekelezaji huo wa uwekaji wa nembo
ya GOT kwenye vidonge katika mwaka wa fedha uliopita, ambapo awali walikuwa
wakiweka nembo ya MSD kwenye vifungashio tu, na kusababisha dawa hizo kuishia
kuchepushwa.
Akizungumza wakati wa maonyesho ya Utumishi wa Umma,
yanayofanyika jijini Dar es Salaam Ofisa Uhusiano Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Bi. Etty
Kusiluka ameeleza kuwa zaidi ya vifaa tiba na dawa 650 za serikali ambazo zinasambazwa na Bohari ya Dawa
zinapaswa zote kuwa na nembo ya
MSD na GOT, na zoezi hili litakamilika kadri
wazabuni wanavyoendelea kupokea maelekezo.
Baadhi ya dawa ambazo tayari zina nembo hiyo ni pamoja na
Mgnesium, Amoxicillin, Pracetamol, Diclofenac, Ciprofloxacin na Cotrimoxazole.
Katika hatua nyingine, Bi Kusiluka ameeleza kuwa Bohari ya
Dawa (MSD) inaendelea na mipango ya kusogeza huduma karibu zaidi na mwananchi
kwa kuanzisha huduma ya uuzaji wa dawa katika maeneo ya hospitali na karibu na
maeneo yenye uhitaji wa dawa, ambapo mauzo hayo yatafanyika kwa saa 24. Huduma
hizi zitaanza katika miji mikubwa nchini ambayo ni pamoja na Mbeya, Dar Es
Salaam, Mwanza na Arusha. Mkoa wa Mbeya ndio utakuwa wa kwanza kutoa huduma hizi, ambapo hadi sasa
maandalizi yako katika hatua za mwisho.
Maduka haya yataiongezea Bohari ya Dawa wigo wa utendaji wa
utoaji huduma kwa wananchi, ambapo hadi sasa huduma ya usambazaji wa dawa na
Vifaa tiba na vitendanishi vya maabara inatolewa kupitia mali inayohifadhiwa
kwenye maghala ya MSD ya kanda zake nane zilizopo mikoa ya Mwanza, Tabora,
Mtwara, Mbeya, Iringa, Dar Es Salaam, Dodoma na Moshi pamoja na vituo vyake
viwili vya mauzo vya Muleba na Tanga.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269