Mholanzi
Mart Nooij alilazimika kusindikizwa na Polisi baada ya mchezo wa leo,
ili kumuepusha na 'adhabu' ya mashabiki wenye hasira
Na Mahmoud Zubeiry, ZANZIBAR
KAMATI ya
Utendaji ya Shirikishi la Soka Tanzania (TFF) imemfuta kazi kocha wa
Taifa Stars, Mholanzi, Mart Nooij na habari zinasema, Kocha Msaidizi wa
Yanga SC, Charles Boniface Mkwasa atashika timu kwa muda, akisaidiwa na
Suleiman Matola wa Simba SC.
Kamati ya
Utendaji ya TFF ililazimika kufanya kikao cha dharula baada ya Stars
kufungwa mabao 3-0 na Uganda usiku huu Uwanja wa Amaan, Zanzibar katika
mchezo wa kwanza Raundi ya kwanza kufuzu CHAN 2016.
“Katika
kikao cha leo pamoja na mambo mengine ilipitia mwenendo wa Timu ya Taifa
(Taifa Stars) ikiwa ni pamoja na kuhudhuria mchezo kati ya Tanzania na
Uganda, kama sehemu ya tathmini ya mwenendo wa timu,”imesema taarifa ya
TFF usiku huu.
“Kamati
ya utendaji kwa kauli moja imeamua yafuatayo: 1.Ajira ya Kocha Mkuu
Maart Nooij inasitishwa mara moja kuanzia tarehe 21/June/2015. 2.
Benchi lote la ufundi la Taifa stars limevunjwa kuanzia tarehe
21/06/2015. 3.Uongozi wa TFF utatangaza punde benchi jipya la ufundi la
timu ya Taifa,”imemalizia taarifa hiyo fupi iluyitolewa na Mkuu wa Idara
ya Habari na Mawasiliano ya TFF, Baraka Kizuguto.
Lakini mara baada ya mchezo huo, Nooij alisema hawezi kuondoka kwa matokeo ya uwanjani, kwa sababu ana Mkataba hadi mwaka 2016.
TFF
italazimika kumlipa Nooij dola za Kimarekani zisizopungua 125, 000 (Sh.
Milioni 250,000) kwa kumvunjia Mkataba, ambao ni mishahara yake ya miezi
10, kwa sababu kwa mwezi alikuwa analipwa dola 12,500 (Sh. Milioni 25).
Mabao mawili ya mshambuliaji Erisa Sekisambu na lingine la Farouk Miya yanahitimisha historia ya kocha huyo Mholanzi Tanzania.
Charles Boniface Mkwasa 'Master' (katikati) atashika timu kwa muda wakati TFF inasaka kocha wa kudumu wa Taifa Stars
Habari za
ndani zinasema Mkwasa na kocha Msaidizi wa Simba SC, Suleiman Matola
watapewa timu kwa muda- mtihani wao wa kwanza ukiwa ni kujaribu kushinda
mabao 4-0 ugenini wiki mbili zijazo ili kusonga mbele CHAN.
Matokeo
ya leo yamewakosesha wachezaji wa Taifa Stars donge nono la Sh. Milioni 1
kila mmoja ahadi iliyotolewa na Rais wa TFF, Jamal Malinzi jana.
Mchezo wa
leo unakuwa wa tano mfululizo, Taifa Stars inafungwa chini ya Nooij
aliyerithi mikoba ya Mdenmark Kim Poulsen Aprili mwaka jana na kwa
ujumla timu hiyo imecheza mechi tisa bila ya ushindi chini ya Mholanzi
huyo.
Kwa
ujumla, Nooij ameiongoza Stars katka mechi 18 tangu arithi mikoba ya
Mdenmark, Kim Poulsen Aprili mwaka jana, kati ya hizo ameshinda tatu tu,
sare sita na kufungwa tisa- akifunga mabao 17 na kufungwa 28.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269